24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSU SHULE ZA MSINGI ZA BWENI -5

Na Christian Bwaya


KATIKA makala iliyopita, tumeona kuwa shule za msingi za bweni zinachangia kuwanyima watoto fursa ya kujifunza ujuzi wa kujitegemea. Uwezo hafifu wa kujifunza stadi za maisha, kwa kiasi kikubwa, unachangiwa na matarajio makubwa ya kitaaluma waliyonayo wazazi kwa watoto wao.

Wamiliki na waendeshaji wa shule za bweni, kimsingi, wanaitikia wito wa wazazi wanaotarajia watoto wao kujifunza maarifa ya shule zaidi hata ikibidi kwa gharama ya kuduma za maeneo mengine muhimu ya kimakuzi.

Katika makala haya, tunaangazia mifano michache ya namna shule hizi za bweni zinazovyochangia kuwaathiri watoto kitabia. Mifano hii inatokana na ulinganisho wa tabia za watoto wanaosoma shule za bweni na wale wanaorudi nyumbani kila siku.

 

Tabia zilizolinganishwa

Watoto walilinganishwa kwa tabia kadhaa chanya na tabia hasi zilizochaguliwa. Tabia chanya ni zile zinazomfanya mtoto ajichukulie vyema yeye mwenyewe na hivyo kuwachukulia wengine vizuri. Mfano ni kucheza na kushirikiana na wenzake, namna anavyoweza kufuata maagizo anayopewa na watu wazima, anavyojiamini, anavyoheshimu watu wazima na kuwapenda watoto wenzake.

Tabia hasi ni zile zinazotokana na mtoto kujisikia vibaya kihisia na hivyo kushindwa kuishi vizuri na watu wengine wanaomzunguka ikiwa ni pamoja na ndugu aliowaacha nyumbani.

Mfano wa tabia hizi ni hisia za upweke na kutegwa na watu wake wa karibu; kuwa na aibu na woga wa kufanya mambo; tabia ya kupenda kudeka, hasira zisizo na maelezo; udokozi wa vitu visivyo vyake; kuonekana anakosa amani na kulia lia bila kuwa na sababu za msingi.

 

Tabia za watoto wa bweni

Watoto wa bweni, kwa kiasi kikubwa, walionekana kuwa na changamoto nyingi za kitabia kuliko wenzako wanaoishi nyumbani. Ingawa kwa haraka haraka watoto hawa walionekana kuwa wachangamfu zaidi kuliko wenzao wanaoishi nyumbani, uchunguzi wa kina ulionesha kuwa walikuwa wamejenga tabia hatarishi kuliko wenzao. Kwa mfano; wengi wao hasa wa darasa la kwanza walikuwa wapweke na walikuwa na tabia ya kuwadekea walezi wao.

Tabia hii inaweza kuelezwa kama matokeo ya kukaa mbali na familia zao kwa muda mrefu, hali inayoweza kutafasiriwa na mtoto kama kutelekezwa. Mathalani, watoto hawa walionekana kujenga imani kwa watu wengine zaidi kuliko wazazi au ndugu zao. Wenzao walioishi nyumbani, walionekana kuwa na imani na mzazi au ndugu wa karibu kuliko mtu mwingine yeyote akiwemo mwalimu.

Kadhalika, watoto wa bweni walionekana kuwa na tabia ya kuwa na hasira zisizo na maelezo ya msingi. Kwa mfano, mtoto wa bweni angeweza kukorofishana na mwenzake kwa jambo dogo kuliko mwenzake anayeishi nyumbani.

 

Changamoto ya malezi ya bweni

Tofauti hiyo ya kitabia kati ya watoto wa bweni na wale wa kutwa inaonekana kuchangiwa, kwa kiasi kikubwa na aina ya malezi yaliyopatikana katika mazingira hayo ya bweni yanayomwathiri mtoto kwa namna kadhaa.

Mosi, mtoto wa bweni anakosa mtu wa karibu anayeweza kumsikiliza kibinafsi na kujua ana shida gani, ana wasiwasi na matarajio yapi na mambo mengine binafsi. Ukaribu huu kati ya mlezi na mtoto unakosekana katika mazingira ya bweni kutokana na idadi kubwa ya watoto wanaoangaliwa na walezi wasiokidhi mahitaji halisi.

Itaendelea…..

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles