31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAMSUBIRI RAIS AJAYE WA ZANZIBAR

MWISHONI mwa Oktoba, 2015, yalitokea maajabu mawili katika nchi yetu kwa upande wa Zanzibar.  Ajabu la kwanza lilikuwa kwa aliyekuwa mgombea Urais kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, kuamua kujitangaza kuwa mshindi wa kiti cha Urais.  Ajabu la pili lilitokea siku mbili tu baadaye, kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar.

Yalikuwa ni maajabu mawili ya kufungia mwaka 2015, kutokana na mambo makuu mawili: Kwa kujitangaza kushinda kiti cha Urais, Maalim Seif alikiuka utaratibu.  Hata hivyo, hatua yake hiyo ilisababisha wengi kuja na majibu yao wenyewe, kama vile inawezekana amejitangaza kwakuwa ana wasiwasi kwamba ZEC haitamtangaza, ikiwa kweli ameshinda.  Wengine walimdhihaki.

Waliomdhihaki Maalim Seif walidai kwamba alikuwa akigombea kiti cha urais kwa mara ya tano, na mara zote hajawahi kutangazwa mshindi kwa kuwa pengine kweli alikuwa ameshindwa.  Walidai kwamba huenda amegundua kwamba mwisho wake umekaribia na hivyo kuamua kujitangaza ili wale “wachache” waliobaki kumwamini, wasikate tamaa.

Ni kweli kwamba mwaka 2015, Maalim Seif alikuwa akigombea kiti hicho kwa mara ya tano chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Alifanya hivyo kwa mara kwanza mwaka 1995 dhidi ya Dk. Salim Amour, kisha mwaka 2000 na 2005 dhidi ya Amani Abeid Karume, halafu tena mwaka 2010 dhidi ya Dk. Ali Mohamed Shein na kwa mara hiyo ya tano mwaka 2015 dhidi ya Dk. Shein tena.  Mara zote hizo, Maalim Seif alikuwa ndiye mgombea mkuu wa upinzani, kutokana na nguvu ambayo chama cha CUF ilikuwa nayo kisiwani humo.

Pengine kosa kubwa kuliko yote lililowahi kufanywa na CUF ni kuususia Uchaguzi wa Marudi wa Machi 20, 2016.  Walijitahidi kulalamika kabla ya uchaguzi huo na mazungumzo yalianza kufanyika.  Hata hivyo, maandalizi ya uchaguzi yaliendela na uchaguzi huo ulifanyika bila ya wao kushiriki.

Matokeo yake yakawa ni kwa mgombea kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein kutangazwa kushinda uchaguzi huo kwa asilimia 91, huku Maalim Seif akipata asilimia 1.9.  Wote tunafahamu kwamba matokeo kama hayo hayajawahi kutokea tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi na kisa hasa cha mgombea wa CCM kupata asilimia 91, ni kutokana na wale wa upinzani kutokwenda kupiga kura.  Wachache sana walioamua kwenda kupiga kura licha ya chama chao kususia, ndio waliosababisha ile asilimia 1.9 ya Maalim Seif.

Kususia uchaguzi kwa chama cha CUF kumesababisha chama hicho kutoweza kujinadi kwa lolote jema tangu kuanza kwa mwaka 2016 hadi sasa, kwani kukosa kwao uwakilishi kumesababisha wasiwe na popote pa kutolea sauti kwa upande wa Zanzibar.  Sana sana tunachowakumbuka kwalo, ni mgogoro mkubwa uliopo kati ya wale walio waaminifu kwa Maalim Seif Shariff Hamad na wale walio waaminifu kwa Ibrahim Lipumba, ambaye ni Mwenyekiti aliyetangaza kujiuzulu uenyekiti, lakini baadaye akaamua kujirejesha.

Kabla ya uchaguzi wa Zanzibar kupita, chama cha CUF kilikuwa na sauti kubwa sana kutokana na kuwa na uwakilishi wa kutosha.  Kwanza kilikuwa na uwakilishi ndani ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kutokana na Katiba yao Zanzibar kuruhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa.  Katika Serikali iliyopita, Maalim Seif alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na baadhi ya wanachama wa CUF walikuwa mawaziri.

 

Hali kadhalika, Baraza la Wawakilishi lilikuwa na uwakilishi wenye uwiano sawia kati ya CCM na CUF.  Lakini kutokana na kususia uchaguzi wa marudio CUF haina hata uwakilishi.  Kilichobaki ni kwa wabunge wachache wa CUF walio katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kusemea mambo yao  huko.  Hata hivyo, haitoshi.

Pengine swali ambalo wengi wetu bado tunajiuliza hadi leo, ni endapo kweli kulikuwa na ulazima wa kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.  Yalikuwa maajabu kwa kuwa sababu zilizotolewa na Mwenyekiti wa ZEC ya kwanini matokeo yote yanafutwa, ni sababu ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele miaka yote – kwa upande wa visiwani hata Bara – na bado matokeo huwa hayafutwi.

Mwenyekiti Jecha alidai kwamba uchaguzi ule haukuwa wa haki na kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria za uchaguzi.  Kwamba baadhi ya makamishna wa ZEC walikuwa ni wawakilishi wa vyama vyao, badala ya kutekeleza majukumu yao inavyotakiwa kikatiba.  Pia kwamba kuligundulika kuwapo kwa kasoro nyingi, ikiwamo kubainika kwa baadhi ya vituo, hasa Pemba, ambavyo vilikuwa na kura nyingi kuliko Daftari la Wapiga Kura wa kituo husika.

Jecha alitoa sababu nyingine kwamba vijana huko Pemba walivamia vituo vya kupigia kura kwa lengo la kutaka kuzua ghasia na kwamba vyama vilionekana kuingilia majukumu ya Tume ikiwamo kujitangazia ushindi na kusababisha mashinikizo kwa Tume.  Hizo ndizo zilizokuwa sababu zake za msingi za kuufuta uchaguzi mzima na kutangaza Uchaguzi wa Marudio miezi kadhaa baadaye.

Huenda zikawa sababu za msingi kabisa, lakini wakati huo huo, sababu hizo hizo zimeshawahi kuripotiwa mara nyingi sana nyakati za uchaguzi na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.  Si Zanzibar, si Bara, mambo hayo yamekuwa yakitokea, lakini bado ‘washindi walitangazwa’.  Pengine hatua ya Jecha itasaidia malalamiko ya namna hiyo kushughulikiwa, kama yeye alivyolishughulikia.

Bahati mbaya ni kwamba tangu wakati huo, umaarufu wa CUF umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ‘kutoonekana’ kwa namna ambayo wanachama wake pamoja na wananchi walivyotaka chama hicho kionekane.  Kwa sasa ukiitamka CUF, wengi tunakuwa hatuna uhakika wa Mwenyekiti hasa wa chama hicho ni nani na vile vile Katibu Mkuu anafanya majukumu yapi.

Wakati tukiyakumbuka yote hayo, habari njema ni kwamba huenda nyanja ya kisiasa Zanzibar ikarejea kwenye uchangamfu wake tuliouzoea.  Ule uchangamfu wa vyama vikubwa viwili kushindana kwa hoja na kwa misimamo na sisi wasikilizaji kupeleka masikio yetu yote visiwani humo kwa ajili ya kufuatilia kwa shauku kubwa yanayoendelea.

Naam, umebaki mwaka mmoja na nusu tu kabla ya uchaguzi mkuu mwingine.  Uchaguzi mkuu huu utakuwa kwa nchi nzima – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.  Hata hivyo, shauku yetu kubwa zaidi itakuwa kwa upande wa Zanzibar, kutokana na Rais wa sasa, Dk. Ali Mohamed Shein, kumaliza muda wake ifikapo mwaka 2020.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutamka kwamba ushindani wa kweli utatoka ndani ya CCM na hakukosea.  Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa,  tumekuwa tukishuhudia ushindani wa hali ya juu ndani ya chama tawala wakati wa chaguzi, huku wanachama mbalimbali wakiwa na uhakika kwamba wao ndio wanaostahili kupokea kijiti.

Baada ya Dk. Salmin Amour kumaliza uongozi kwa awamu mbili, Amani Abeid Karume ndiye aliyepokea kijiti hicho.  Haikuwa rahisi.  Enzi hizo, Dk. Mohamed Gharib Bilal alikuwa na ushawishi mkubwa sana huko Zanzibar  na mpambano kati yake na Karume ulikuwa ukifuatiliwa na karibu kila mtu.

Baada ya Rais Karume kumaliza uongozi kwa awamu mbili, ushindani mwingine mkubwa ulitokea ndani ya CCM, wakiwapo watu kama Ali Juma Shamuhuna kutaka kukisogelea kiti hicho.  CCM kilimpitisha Dk. Ai Mohamed Shein kuwa mgombea Urais wa kiti hicho  na ndio  anamalizia awamu yake ya pili ya uongozi.

Lakini  licha ya ushindani mkubwa kuwamo ndani ya CCM, bado wagombea wa CCM wakivuka kigingi hicho hukutana na wagombea kutoka vyama vya upinzani. Na kwa Zanzibar, imekuwa ikijulikana kwamba mpinzani mkubwa wa CCM ni chama cha CUF na mpinzani  wa miaka yote wa wagombea Urais wa CCM, ni Maalim Seif Shariff Hamad.

Sasa wakati tukiwa tumebakiwa na mwaka mmoja na nusu tu ili kuelekea uchaguzi mkuu, macho yetu yote yanageukia Zanzibar.  Wakati tukielekea  Oktoba 2020, swali kubwa zaidi ya yote, ni nani atakayekuwa Rais ajaye wa Zanzibar.

Lakini yapo maswali mengine madogo tunayojiuliza kuhusu Oktoba 2020.  Nani atakayekuwa mgombea wa Urais kupitia CCM?  Ndani ya CCM Zanzibar, ni nani aliye machachari kwa sasa?  Licha ya umachachari wa baadhi ya wanachama waliopo huko, ni yupi hasa mwenye nafasi nzuri zaidi ya kupitishwa na chama tawala kuwa mgombea?

Wakati huo huo, yapo maswali mengine pia kwa upande wa wapinzani.  Umaarufu wa CUF visiwani humo kwa sasa ukoje?  Je, wataibuka na kuwa ile CUF tunayoijua?  Watashiriki uchaguzi au watasusia tena?  Wakishiriki, nani atakayekuwa mgombea wa kiti cha Urais?  Maalim Seif atataka kugombea tena kwa mara ya sita?  Kama si yeye, nani anayeweza kuvaa viatu vyake?  Hata wakitaka kushiriki, mgogoro wa kambi ya Maalim na kambi ya Lipumba utaathiri ushiriki wao kwa kiwango gani?  Lipumba naye anapanga kufanya ‘kituko’ gani safari hii?

Wakati bado tukijiuliza maswali hayo, jambo kubwa kabisa tunalotakiwa kulijua, ni kwamba Zanzibar inahitaji Rais wa tofauti.  Ni kweli kwamba wakati akiondoka madarakani, Rais Amani Abeid Karume alitimiza ahadi ya kuwapa Wazanzibari Katiba Mpya.  Ni Katiba hii ndiyo iliyozungumzia kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na ni Katiba hii iliyofanikisha Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, kilichotokea Zanzibar wakati wa uchaguzi uliopita, kimeacha doa na mpasuko wa aina fulani.  Mpasuko ambao hauwezi kuondoka kwa kuitisha tu uchaguzi na kuchaguliwa kwa Rais wa aina yoyote.  Mpasuko ambao ukiendelea kudharauliwa kama ilivyo sasa, utazidi kupanuka na kufika hatua ambayo baadaye tukigeuka nyuma na kujiuliza kulikoni, tutabaki na majuto tu.

Ndiyo maana Zanzibar inahitaji Rais wa tofauti, Rais ambaye atasaidia kuondoa mpasuko uliopo.  Rais ambaye ataiheshimu Katiba ya Zanzibar na kuisaidia kusonga mbele.  Rais ambaye atatambua kwamba Zanzibar ni ya Wazanzibari wote na ili wafanikiwe  katika yoyote wanayoyataka, lazima wawe wamoja.  Lakini Je, chama kipi kitakachotupa Rais wa namna hiyo?

Wakati wagombea wa vyama vingine wakiwa wameanza kujitokeza kutangaza nia ya kugombea Urais wa Zanzibar, nasi kwa hamu kubwa tunasubiri kusikia watakaoanza kutangaza nia kutokea CCM, CUF na vyama vingine vikubwa visiwani humo.

Ombi letu kubwa kwa watangaza nia hao, ni kuwakumbusha tu kwamba Urais si sawa na kuongoza familia – ni kuongoza nchi na inahitaji ujasiri mkubwa.  Yeyote anayetaka kutangaza nia akumbuke kwamba anaingia katika kazi kubwa yenye lawama kubwa, inayohitaji ujasiri mkubwa wa kuwaleta watu pamoja.

Naam, tunamsubiri kwa hamu Rais ajaye wa Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles