TUNAHITAJI WAWEKEZAJI WA KILIMO, UVUVI-MAJALIWA

0
801

Na MWANDISHI MAALUMU

-CHINA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Tanzania inahitaji wawekezaji wakubwa kutoka China ambao watawekeza kwenye viwanda vya mazao ya kilimo, samaki na mifugo.

Aliyasema hayo jana, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo wa China,  Han Changfu, jijini Beijing.

Alisema  katika kipindi hiki ambacho Tanzania imeamua kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda, China ni nchi sahihi kushirikiana nayo kwa sababu ina wawekezaji wa kutosha.

“China ni rafiki yetu na pia imepiga hatua kubwa kwenye teknolojia ya viwanda, hivyo tunahitaji kuendelea kushirikiana nayo ili tuweze kupata na teknolojia sahihi ya viwanda mbalimbali,” alisema

Waziri Mkuu alisema Serikali zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ziko tayari wakati wowote kuwapokea wawekezaji kutoka China.

Alisema wawekezaji hao watapatiwa ardhi ya kujenga  viwanda ambavyo vitatumia mazao ya kilimo, mifugo na bahari, hasa samaki, ambayo mengi yanapatikana kwa wingi nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Tanzania inahitaji kupata soko la mbaazi na soya nchini China, ili kuwawezesha wakulima wake kuwa na soko la uhakika la mazao hayo.

Alisema hivi sasa inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa soko la mazao hayo, baada ya wakulima kuitikia wito wa Serikali  wa kuwataka walime mazao hayo kwa ajili ya chakula na biashara.

“Tumelazimika kutafuta masoko ya mazao hayo hapa China ili kutowakatisha tamaa wakulima wetu, kwani itakuwa vigumu kwao kuendelea kulima mazao hayo kwa wingi bila ya kuwa na uhakika wa soko,” alisema

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa China alisema nchi yake iko tayari kutoa elimu na mafunzo kwa Watanzania, hasa kwa kuandaa semina zitakazowawezesha washiriki kuongeza ujuzi wao, hatua ambayo itawasaidia Maofisa Ugani wetu kufanya kazi zao vizuri zaidi.

Katika mazungumzo hayo, Tanzania na China zimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika maeneo ya uvuvi, ambapo Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, Rashidi Ali Juma, alitia saini kwa upande wa Tanzania na China iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Eudong  Yu .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here