33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAHITAJI KUFAHAMU WALIPO KINA ROMA

NA CHRISTOPHER MSEKENA

TASNIA ya burudani imepigwa na butwaa, inashangaa na imejaa hofu kuu kufuatia tukio la kutekwa kwa wasanii wa Bongo Fleva katika miondoko ya hip hop, Roma Mkatoliki, Moni Central zone na vijana wengine waliokuwepo kwenye studio za Tongwe, Dar es Salaam Jumatano jioni kisha kupelekwa kusikojulikana.

Hili ni geni kwetu, halijawahi kutokea ndiyo maana hofu imezidi kutanda hasa ukizingatia muda unakwenda na vyombo vya usalama vikisema havina taarifa za kukamatwa kwa wasanii hawa.

Ukubwa wa tukio la kutekwa kwa wasanii hawa kumeficha shamra shamra za kumbukumbu za kifo cha Steven Kanumba ambaye alifariki siku kama ya jana miaka mitano iliyopita.

Wapo wapi Roma na Moni? Ni swali lililochukua nafasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii mpaka kwenye mitaa ambako watu wana kiu ya kujua walipo wasanii hawa.

Maana hata simu zao zinaita lakini hazipokelewi hata jumbe kwenye mtandao wa Whatsapp zinasomwa lakini hakuna majibu, hofu inazidi na inafanya tutamani kupata majibu ya uhakika.

Jambo hili lina maswali mengi kuliko majibu na hakuna anayeweza kuwa na majibu ya kutosha ndiyo maana tumekuwa watu wa hofu tukisubiri uchunguzi wa vyombo vyetu vya usalama utoe jawabu.

Mastaa mbalimbali bila kujali wanatoka kwenye sekta ipi wameonyesha kuguswa na jambo hili. Kupitia kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii waliandika jumbe za kutaka kujua walipo Roma na wenzake.

Hali kadhalika jana wasanii mbalimbali walikutana kwenye fukwe za Coco, Dar es Salaam kujadiliana namna gani wanavyoweza kuwarudisha wasanii wenzao ambao hawajulikani walipo.

Tunategemea sana Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Waziri Dk. Harrison Mwakyembe, kufanya kitu kwenye hili ili kuondoa hofu zilizojaa kwenye miili ya wasanii na mashabiki wao.

Nimeona maoni ya mashabiki huko kwenye mitandao ya kijamii yakianza kuwatuhumu baadhi ya viongozi kusimama nyuma ya sakata hili. Si busara na haipendezi kwani itatutoa kwenye msingi wa kuhoji wapo wapi kina Roma.

Huu ni wakati wa kutulia na kusubiri vyombo vya usalama kufanya kazi yake ili ukweli ubainike na si kutupiana lawama, tunapaswa kuwa wamoja mpaka mwisho wa tukio hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles