27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Tumuenzi Mwalimu Nyerere kivitendo

julius_nyerereNa FRANK MDIMI

OKTOBA 14 mwaka 1999, miaka 17 iliyopita, nikiwa katika maagizo ya kawaida na mwandishi wa gazeti la The African, nilibahatika kupangwa kufuatilia matukio ya habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo.

Nakumbuka siku hiyo niliwahi kufika hapo,  nilikuwa na waandishi wa vyombo vingine vya habari. Rais wa Awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa alikuwa akisoma taarifa akiueleza umma kuhusu kifo cha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilichotokea Hospitali ya St. Thomas, Uingereza alipopelekwa kwa matibabu ya Kansa ya Damu, Leukemia iliyogunduliwa .

Tukiwa tumeketi mbele ya Televisheni kubwa pale ukumbi wa Habari Maelezo, Rais Mkapa, alielezea hatua kwa hatua kuhusu msiba mkubwa uliolikabili Taifa. Aliwatoa hofu wananchi na kuwahakikishia kuwa Mwalimu aliacha misingi imara ya umoja na ushirikiano na hivyo viongozi wote wa nchi hii wameapa kuilinda na kuiendeleza na watafanya hivyo.

Aidha alielezea umuhimu wa kuungana katika kipindi hicho kigumu na kutangaza kuwa Mwalimu atazikwa kwa heshima zote za kitaifa na Serikali ingeendelea kutoa taarifa kuhusu taratibu za mwili kuwasili pamoja na mazishi.

Taarifa za kuugua kwa Mwalimu zilizaa vikundi vya hapa na pale huku kila mmoja akiwaza jinsi Tanzania itakavyomudu kusonga mbele bila uwepo wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Katika kipindi chote hicho bado sikuweza kuamini kuwa Mwalimu Nyerere hatunaye tena Duniani.

Nakumbuka siku ya kuupokea mwili nilipangwa kufuatilia matukio ya habari maeneo ya Manzese ambapo mwili wa Mwalimu ungepita ukitokea Uwanja wa Ndege, Bararabara ya Mandela na kisha hiyo ya Morogoro na baadaye kuendelea na msafara hadi Msasani.

Watu walikuwa wamejaa sana pande zote za barabara wengi wakiwa kama mimi, hawaamini kuwa Baba wa Taifa ambaye alipanda ndege mwenyewe akielekea kwenye matibabu nchini Uingereza, sasa anarudi akiwa Marehemu, sandukuni, hapumui na akielekea kwenye nyumba ya pumziko la milele.

Mara tukasikia msafara wa ving’ora na magari mengi ukipita, kisha likapita gari lililojaza waandishi wa habari wengi wa ndani na nje ya nchi. Nakumbuka kumuona kaka yangu Moshy Kiyungi na kamera yake wakati huo akiandikia gazeti la Guardian.

Nakumbuka kuwa gari la waandishi lilikuwa mbele na kisha gari lililobeba mwili wa Mwalimu katika “Gun Carriage” likifuata nyuma likiwa limefunikwa kwa bendera.

Ni hapo nilipoamini kuwa sasa kweli zile taarifa zilizokuwa zikitangazwa kuwa Mwalimu hatunaye, kweli hatunaye. Nikaanza kuiwaza upya Tanzania bila Mwalimu na kufarijiwa na maelezo aliyoyatoa Rais Mkapa katika hotuba ile.

Nikakumbuka siku Mwalimu alipong’atuka katika kiti cha urais pale Ikulu ya Magogoni mwaka 1985. Kwamba ilikuwa asubuhi nikiwa na wanafunzi wenzangu wa Shule ya Msingi Bunge iliyokuwa jirani na Ikulu hiyo, tulikuwa tumejipanga kumuaga Mwalimu ambaye alitoka akiwa katika gari ya wazi na alitupungia mikono na sisi tulimpungia pia.

Nikakumbuka alipolitangazia Taifa kuhusu kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu na ambaye alifariki kwa ajali ya gari mkoani Morogoro mwaka 1984. Nikakumbuka matukio mengi ambayo yalipita ghafla na kunifanya kwa muda kuduwaa. Lakini ilikuwa ni kweli.

Nakumbuka  baada ya siku chache kulikuwa na zoezi la kutoa heshima za mwisho pale uwanja wa taifa ambapo watu kwa maelfu waliendelea kutoa heshima zao.

Baadaye kukafanyika mazishi ya kitaifa pale uwanja wa Taifa, Shamba la Bibi ambapo nakumbuka Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walikuwa ni wazungumzaji wakuu katika tukio lile.

Viongozi wa Kitaifa na Kimataifa walimiminika katika mazishi ya kitaifa ya Mwalimu na wengi wao walibebwa kwa mabasi maalumu hadi uwanja wa taifa kuhudhuria mazishi hayo ya kitaifa.

Pia nakumbuka mmoja wa viongozi aliyepita kutoa heshima za mwisho akiwa na wakati mgumu sana alikuwa ni mzee Yusuph Makamba. Mzee huyu hakuweza kujizuia alilia kwa huzuni sana na alisaidiwa hata kutembea kwa kushikiliwa.

Hata hivyo yapo mambo ambayo pia yamenisukuma kuweka kumbukumbu hii ambayo ni pamoja na dhana potofu iliyowahi kujengwa kuwa Mwalimu hakutaka mabadiliko.

Mwalimu ndiye aliyeasisi siasa za vyama vingi licha ya kuwa maoni ya wananchi yalitaka tuendelee kuwa na chama kimoja. Mwalimu alitaka mabadiliko chanya yaliyolenga kulinufaisha Taifa kwa kuhakikisha kuwa viongozi wanasimamia masuala ya kupiga vita umasikini wa wananchi wanaowaongoza.

Taifa linaendeshwa kwa misingi ya haki na si kwa ubaguzi wa kikabila, viongozi wanachukia na wanapiga vita rushwa.

Lakini pia alituasa kuwa yapo mambo ambayo yawezekana aliyakosea kama binadamu na kutuasa hayo tuyaache na tuendelee na yale ambayo ni mazuri. Lakini aliwahi kuelezea kusikitishwa kwake kuwa yale mazuri yake yalikuwa yakibomolewa.

Changamoto iliyo mbele yetu ni kuendelea kuyaenzi maendeleo mengi aliyochangia kililetea Taifa. Tuhakikishe kuwa tunakuza uchumi na tunaweza kutimiza ndoto ya itikadi ya “Ujamaa na Kujitegemea” kwa kuitafsiri kuwa ni kuzingatia misingi ya “Uchumi wa soko. Mabadiliko ya Serikali kujiondoa katika kufanya biashara aliyaishi walau miaka mitano ya uhai wake. Yalianza mwaka 1993 na yaliwezesha sekta nyingi kufunguka ili kuruhusu sekta binafsi kushiriki katika uchumi. Mabadiliko yaliweka mfumo bora zaidi wa udhibiti na huduma kuboreshwa.

Shime tumuenzi Mwalimu kwa kujenga Tanzania yenye uchumi imara unaowanufaisha wananchi wote ambao kwa kasi tunayokwenda nayo chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya Tano, inayoendeleza mafanikio ya serikali za awamu zilizotangulia, tutafika na tutafanikiwa kuijenga Tanzania yenye neema kwa wote.

Mola ailaze roho ya Baba wa Taifa mahala pema peponi. Tumuenzi, tulijenge na kulistawisha Taifa aliloliasisi likiwa Taifa lenye umoja, upendo, mshikamano na uchumi imara unaotunufaisha sote na unaozingatia maendeleo na mafanikio ya kizazi kijacho.

 

Frank Mdimi alikuwa mwandishi wa gazeti la The African katika kipindi cha matukio ya kifo cha Mwalimu Nyerere. Kwa sasa ni Afisa Mwandamizi wa Mawasialiano na Mahusiano ya Umma katika Tume ya Ushindani (FCC). Anapatikana kwa simu Na. 0784762437 na barua pepe [email protected]

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles