26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TULIKOTOKA: Tujikumbushe chaguzi chini ya chama kimoja zilivyokuwa

HILAL K SUED

WAKATI wa kipindi cha mfumo wa demokrasia ya chama kimoja, wabunge walikuwa wanaweka utii wao kwa chama na serikali. Na ni sahihi kusema kwamba huko ndiko walitakiwa kuelekeza utii na uwajibikaji wao.

Na kama ilivyokuwa kwa urais, chama ndicho kilikuwa kinamchagua mtu inayemtaka awe mbunge. Tofauti ilikuwa kwamba katika chaguzi za wabunge chama huteua wanachama wake wawili katika kila jimbo la uchaguzi ambao hupigiwa kura siku ya uchaguzi na mara nyingi ilikuwa kwamba katika wawili hawa, yule anayetakiwa kuwa mbunge hupambanishwa na mgombea mbovu ili kuhakikisha ushindi wake.

Hapo awali wagombea hupewa alama jembe au nyumba na katika majukwaa wakati wa kampeni, kila mgombea husimama (katika mkutano huo huo mmoja) na kujinadi kwa wapiga kura. Hufanya hivyo zaidi kwa kutumia alama zao kwa mfano mgombea wa alama ya jembe husema “bila jembe mtu hawezi kupata mazao ya chakula ya kumwezesha kuishi,” Naye mwenye alama ya nyumba husimama na kusema “bila nyumba familia zenu zitalelewa vipi? Suala la kunadi sera lilikuwa halipo.

Kwa mtazamo wowote ule yalikuwa ni mambo ya kipuuzi kweli kweli katika chaguzi hizo ambazo zilikuwa ni geresha tu ya demokrasia na hasa ikizingatiwa kuwa idadi kubwa sana ya wagombea (karibu asilimia 80) wa alama ya jembe ndiyo walikuwa wanashinda. Na haikuwa kwamba mgombea alikuwa anajichagulia alama mwenyewe tu, au kwamba alama ziligawiwa kwa njia ya kurusha shilingi.

Alama hizo zilikuwa zinatolewa kwa njia za upendeleo tu, mara nyingi mgombea yule anayetakiwa na chama kuwa mbunge (labda kama Rais alikuwa anamtaka amteue kuwa waziri) ndiyo hupewa alama ya jembe. Hata hivyo mara kadhaa hutokea kwamba mgombea wa nyumba akashinda.

Katika uchaguzi wa rais hakukuwapo mpinzani yeyote kwa mgombea aliyeteuliwa na chama, karatasi ya kupigia kura ilikuwa na vyumba viwili lakini picha moja tu ya huyo mgombea, wakati huo Mwalimu Julius Nyerere. Mpiga kura alitakiwa kuweka alama ya vyema katika chumba kimojawapo cha huyo mgombea au kile kingine kitupu iwapo hamuafiki Nyerere.

Halafu wapiga kura wengi walikuwa hawajui kitu kimoja, kwamba karatasi ya kupigia kura kwa rais ilikuwa ina namba, huchanwa kutoka kwenye kitabu ambapo kipande chake (counterfoil) chenye namba hiyo hubaki kwenye kitabu na kina jina la mpiga kura.

Hii ina maana kwamba iwapo wakitaka, watu wa Tume ya Uchaguzi baadaye wanaweza kufahamu Fulani alimpigia kura Nyerere au la. Inadaiwa katika uchaguzi mmoja miaka ile ya 70 utawala wa Nyerere ulikuwa na wasiwasi na kigogo mmoja wa chama na serikali kwamba alipiga kura vipi katika uchaguzi wa rais. Ikagundulika hakumpigia kura Nyerere, na kilichotokea dhidi yakje msomaji anaweza mwenyewe kuhisi.

Kwa hivyo ni dhahiri kwamba mbunge anayepatikana kwa njia hii hawi mbunge wa wa wananchi, bali ni wa chama na serikali na ndiyo maana wale wabunge waliyokuwa wanakwenda kinyume na sera za chama, wabunge wakorofi na wasiyokuwa na nidhamu kwa chama na serikali hutimuliwa, kwa kunyang’anywa kadi za uanachama.

Katika siasa za demokrasia ya upinzani wa vyama vingi uliyoingia mwanzoni mwa miaka ya 90 hali kama hii ilitakiwa isiwepo kabisa kwa sababu mbunge anachaguliwa moja kwa moja na wananchi, kwa hiyo anatakiwa, kwa kiasi kikubwa kuwajibika kwa wapiga kura wake, na kwa hivyo utii auweke kwao – na siyo kwa chama chake.

Chama chake kinakuwa kama mdhamini wake tu, na ndiyo maana vikao vya uteuzi vya chama husika vinatakiwa viwe vya kidemokrasia na huru kabisa. Lengo hapa ni kumpata mgombea anayekubalika na wapiga kura wa chama hicho katika jimbo la uchaguzi husika na ambaye akifanikiwa kukinyakuwa kiti katika uchaguzi, basi ndiyo anakuwa mwakilishi wa wananchi anayekubalika na wengi kwani ndiye wanayemuona anafaa.

Hutokea mgogoro pale mgombea anapotumia njia chafu kupata uteuzi — kama vile kutoa hongo kwa wajumbe n.k. Mara nyingi haya yamekuwa yakijitokeza kwa chama tawala (CCM) kama ilivyokuwa inaripotiwa mara kadha. Mgombea asiyekubalika huingizwa tu katika kinyang’anyiro na hii bila shaka hapo awali lilitokana na kurithi mambo ya wakati wa siasa za chama kimoja mambo ambayo yalikuwa yanashindikana kuondoka.

Kwa hali ya kawaida, kitu muhimu kinachotakiwa ni kwa serikali inayokuwapo madarakani na inayojali misingi halisi ya demokrasia kuheshimu maamuzi ya wapiga kura wa majimboni, yaani kuwaheshimu wawakilishi wote wa wananchi bila kujali vyama vyao.

Ni sawasawa tu na pale serikali ya CCM inaposisitiza kwa wapinzani kwamba kwa kuwa ndiyo iliyoingia madarakani kwa njia ya demokrasia, basi ni wajibu waikubali na kuiheshimu.

Vinginevyo ni kurudi kule tulikotoka — tabia ya serikali kupenda kujiona ni ya chama kimoja tu na kwamba wawakilishi wa kambi ya upinzani wanapochaguliwa huwa ni makosa makubwa wapigakura wanayofanya, makosa ambayo yanahitaji kuadhibiwa.

Na adhabu yenyewe ni kuyanyima au kuwacheleweshea ruzuku kutoka serikali, misaada au utoaji wa huduma muhimu za kijamii majimbo na wilaya zenye wawakilishi wapinzani (madiwani na/au wabunge), na hasa zile halmashauri za wilaya na za miji zinazodhibitiwa na vyama vya upinzani.

Mara kadha hii imetokea kuwa ni mojawapo ya mbinu chafu za kampeni – mbinu ambazo ni za kunyongana mikono (arm-twisting) na vitisho kwa wapiga kura kule majimboni – kwamba wasirudie kuifanya makosa ya kuwachagua wapinzani kuwa wawakilishi wao.

Tabia hii, ilianza sambamba na mfumo wa vyama vingi na ilishamiri sana katika Awamu ya Tatu ya urais wa Benjamin Mkapa. Tuliona kwa mfano, jinsi halmashauri kama vile za Moshi, Karatu, Kigoma-Ujiji na Bukoba zilivyokuwa zinazibwa pumzi na serikali kuu, mtu angedhani hazikuwa sehemu ya Tanzania.

Alipoingia Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alitangaza kuwa serikali yake kamwe haitawabagua wapinzani na waziwazi akasisitiza kuwa haitazibagua halmashauri zilizochagua wawakilishi wa kutoka kambi ya upinzani kwa maana ya kupatiwa ruzuku na huduma mbalimbali kutoka Serikali Kuu.

Bila shaka hayo yalikuwa ni maneno tu yasiyokuwa na dhamira halisi na huenda aliyatamka hayo baada ya kuubaini ukweli – kwamba ushindi wake wa “kishindo” (wa 2005) kwa kiasi kikubwa ulisukumwa na kura za wapinzania pia.

Kuna baadhi ya majimbo, kwa mfano lile la Tarime, Kikwete alipata kura nyingi za urais kuliko zile kura za mpinzani wake wa karibu, Freeman Mbowe wa Chadema. Lakini wapiga kura wa jimbo hilo walimchagua mbunge wa Chadema badala wa yule wa CCM.

Lakini pia kulikuwapo hili: alipokuwa Rais Kikwete aliwahi kudaiwa kuwatangazia wananchi wa jimbo la uchaguzi la Kigoma Kaskazini lililokuwa (wakati ule) linashikiliwa na Mbunge Zitto Kabwe wa Chadema kwamba walifanya makosa kuchagua upinzani na ndiyo maana wanakosa maendeleo.

Hata hivyo msemaji wa serikali alikanusha kwamba Rais hakusema hivyo. Lakini hata kile kinachosemekana ndicho alikisema, kwamba “pamoja na wananchi hao kuchagua upinzani serikali itawaondolea tabu zao” ni kitu ambacho hakupaswa kukisema.

Kama Kikwete alishatamka tangu awali kabisa kwamba alikuwa tayari kuyahudumia majimbo yote bila ubaguzi wa kisiasa, kule kuwakumbusha tu wananchi wa Kigoma-Kaskazini kwamba pamoja na jinsi walivyopiga kura, serikali yake haitawabagua, ni namna moja ya kuwaambia kwa njia isiyo bayana kwamba walikosea kuchagua upinzani.
Aidha ni kitu kisichoingia akilini sawasawa, kwani hadi leo hii idadi kubwa ya halmashauri ambazo zinadhibitiwa na CCM zimezama katika rushwa na ufisadi, hali inayofanya wananchi wa maeneo hayo kukosa maendeleo ya maana.

Kikwete mwenyewe alikuwa anazilalamikia halmashauri hizo kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na kuzionya baadhi kwamba alikuwa tayari kuzifuta iwapo hali hii isingebadilika.

Kwa hivyo pamoja na ubovu huu mkubwa ndani ya halmashauri hizo, bado chama tawala kingependa kuzidhibiti halmashauri zote nchini, yaani haiko tayari kuaibishwa na zile zinazodhibitiwa na upinzani pale zinapoonekana kufanya vizuri.

Kutokana na hili na yanayoendelea sasa hivi katika medani ya demokrasia, kama vile kupungua wigo wa kufanya demokrasia (shrinking of democracy space) hivi karibuni kumetokea wito, hasa kutoka kwa baadhi ya viongozi na makada wa upande wa upinzani kwamba ni vyema kupitisha marekebisho ya Katiba ili nchi irudi tu kwenye mfumo wa chama kimoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles