25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

TUJIREKEBISHE KAMA TUNATAKA NCHI YETU IBAKI KUWA KISIWA CHA AMANI

BADO nchi imezizima kutokana na tukio la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kumiminiwa risasi 32 huku tano zikipenya mwilini mwake.

Tukio hilo lililovuta hisia za wengi, lilitokea mchana wa Alhamisi iliyopita katika eneo la Area D mjini Dodoma.

Wengi wameelezea kulaani tukio lile ambalo ni wazi lililenga kumuua mwanasheria mkuu huyo wa Chadema ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

MTANZANIA Jumapili tunaungana na Watanzania wote wenye mapenzi mema kumwombea Lissu apone haraka ili arudi kuja kulitumikia taifa lake.

Tunazidi kuvitaka vyombo vya dola kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na tukio hilo.

Jambo hili limeleta hofu na kila mtu anazungumza lake. Wako wanaolihusisha na masuala ya kisiasa. Wengine wanadai msimamo wake usioyumba juu ya kile anachokiamini huenda ukawa umemjengea maadui wengi.

Ni kazi ya polisi kuwasaka waliohusika kumdhuru Lissu ili watueleze kwa nini walitaka kumuua, nani aliwatuma, na kwa sababu gani. Polisi wakifanya kazi yao vizuri watasadia kuondoa hisia zilizojaa mitaani.

Kushambuliwa kwa Lissu kumetonesha madonda ya matukio yaliyopita. Bado Watanzania wanakumbuka jinsi Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alivyotishiwa kwa bastola mchana kweupe jijini Dar es Salaam, Machi mwaka huu.

Nape alikuwa akitaka kuzungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wake wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Matukio ya watu kutekwa nayo yamekuwa yakishamiri. Sasa imefikia hatua vijana wanawateka watoto wadogo na kisha kuwataka wazazi kutoa fedha. Hii yote ni viashiria kuwa nchi imegubikwa na matukio ya kushangaza.

Ni matukio ya kushangaza kwa sababu hatukuzoea kusikia watu, tena wengine viongozi wakitishiwa kwa silaha. Tuna kazi kubwa kama jamii kuangalia tumekosea wapi ili tujirekebishe kama tunataka nchi yetu iendelee kuitwa ‘kisiwa cha amani’.

Tukio la kushambuliwa kwa Lissu limelaaniwa kote duniani. Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa mfano, ulilitaja shambulio hilo kuwa ni la kijinga. Watu wa mataifa ya nje wameanza kutushangaa kwa kuanza kuchezea tunu ya amani.

MTANZANIA Jumapili tunaunga mkono kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Dk. Jacob Chimeledya, aliyesema matukio yanayotokea sasa ni kiashirio tosha kwamba nchi inahitaji kuwa na utawala bora ambao utaongeza haki kwenye makundi ya watu.

Kama anavyosema Askofu Chimeledya, tofauti ya kimawazo tuliyonayo isitufanye tufikie hatua za kuumizana. Badala ya kujenga uadui, tofauti zetu tuzitumie kama fursa.

Jeshi la Polisi limetangaza kujipanga ili kuwakamata wale wote waliotaka kuitoa roho ya Lissu, tuko nyuma yao.

Heshima ya jeshi hili siku zijazo itategemea sana jinsi watakavyolimaliza jambo hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles