24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TUJIFUNZE KUPITIA MAKOSA YA WENZETU

 

LEO hii ukitaka kutoa mfano kama darasa la kujifunza kuhusu uchumi kwa nchi za Afrika, hutaacha kuitaja Zimbabwe.

Vilevile hutaacha kuitaja nchi ya Ethiopia kama darasa la kujifunza, baada ya kupita kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa uliosababishwa na watawala waliopita, ambao  wenyewe wanakiri walikanyaga juu ya migongo ya watu wakati wakisema wanapandisha kuta za uchumi wa nchi hiyo.

Nchi hizi mbili namna zilikotoka, zilipo na zinakoelekea, tunadhani ni darasa tosha kwetu na funzo kubwa kwamba hatupaswi kupitia njia kama zao.

Watu wanaofuatilia mwenendo wa mambo katika nchi ya Zimbabwe watakubaliana na sisi kwamba, Rais wa sasa, Emmerson Mnangagwa,  anapambana kuitoa nchi kwenye mtanzuko wa anguko la uchumi ambalo msingi wake ni msimamo wa kiongozi wao, Robert Mugabe.

Baada ya miaka ya mgogoro mkubwa wa kiuchumi uliosababisha mfumuko uliopitiliza wa bei, yote hayo yakiwa msingi wa maandamano mitaani, Mnangagwa anaonekana kupambana kubadili sura na hali ya uchumi wa Taifa hilo kwa kutafuta njia bora za kidiplomasia ndani na nje ya Taifa hilo.

Vilevile watu wanaofuatilia masuala ya kimataifa watakuwa wanafahamu jinsi ambavyo Waziri Mkuu mpya wa Taifa hilo, Abiy Ahmed, naye anavyopambana kurejesha nchi kutoka kwenye utawala hadi kwenye uongozi.

Viongozi wa Taifa hilo la pili kwa idadi ya watu barani Afrika, licha ya kufanya vyema kujenga uchumi wa nchi hiyo, wametambua makosa yao ambayo waliona wasiporudi nyuma uchumi walioujenga kwa nguvu kubwa unaweza usilete maana.

Baada ya miaka kadhaa ya hasira kali dhidi ya serikali, hali ya hatari, watu kukamatwa ovyo na kufungiwa kwa huduma za intaneti, Abiy sasa anaonekana kama mtu ambaye amekuja kufanya mageuzi baada ya kuanza kuwaomba radhi raia wake kwa kusababishiwa maumivu na serikali ya nchi hiyo kwa miaka mingi.

Abiy aliingia madarakani baada ya Februari 15, mwaka huu, aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hailemariam Desalegn, kujiuzulu.

Hailemariam alitangaza kujiuzulu ili kusaidia kile

alichokiita kusuluhisha mzozo wa kisiasa uliopo nchini humo ambao ulikuwa ukitishia uwekezaji.

Wakati akitangaza kujiuzulu, Hailemariam alisema chama tawala cha Ethiopia Peoples Revolutionary Democratic Front na serikali ilifikia uamuzi huo kwa nia ya kutaka kupata ufanisi wa mabadiliko katika wakati ambao nchi ilikuwa na mgogoro na matatizo ya kisiasa, huku watu wengi wakiwa wamepoteza maisha yao, wengine makazi, huku mali zao zikiharibiwa na wengine wakifanya juhudi za kulipa kisasi kwa kuharibu uwekezaji uliofanyika.

Tunakumbuka vyema maneno ya Hailemariam kwamba ili kupata suluhu ya mtanziko huo, njia pekee ilikuwa ni kuleta mabadiliko ya uongozi.

Tumeyasema haya ili wale waliopewa mamlaka ya kiuongozi wanapotekeleza wajibu wao wa kuwaletea maendeleo Watanzania kamwe wasitumie migongo ya watu kama ngazi ya kupandisha kuta za uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles