29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tuendako: Absalom Kibanda auona ukakasi mkubwa katika uteuzi, utumbuaji wa wakuu wa taasisi nyeti…

Na Absalom Kibanda          


NIMEKUWA nikifuatilia kwa namna ya kutafakari na kujiuliza mara kadhaa juu ya maana hasa ya mamlaka makubwa ya kiuteuzi ambayo yamewekwa katika mikono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ufuatiliaji wangu wa jambo hili hauna tofauti na ule ambao umekuwa ukifanywa kwa miaka mingi na watu wengi ambao wamekuwa wakichambua juu ya misingi ya utawala bora na wa sheria katika taifa letu.

Pengine ninapaswa kulisemea hili mapema kwamba tafakuri yangu haina sababu wala nia ya kuishia katika kuhoji juu ya mamlaka makubwa aliyonayo Rais, ambayo amepewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano aliyoapa kuilinda, bali pia kujifunza madhila ya maamuzi hayo.

Katika siku za hivi karibuni tafakuri yangu juu ya hili ilirejeshwa tena na matukio ya majuzi tu hapa, ambayo pamoja na mambo mengine, tulishuhudia Rais John Pombe Magufuli akifanya mabadiliko makubwa yaliyoigusa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Katika mabadiliko hayo, kwa mara ya pili tangu alipoingia madarakani, miaka mitatu iliyopita Rais amemwondoa tena Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru na kumwingiza mtu mpya na akifanya kile kile alichofanya awali, kumchukua mtendaji mkuu mpya kutoka nje ya taasisi hiyo.

Akionesha dhahiri dhamira yake ile ile ya mara ya kwanza ya kutaka kuona Takukuru pengine ikiendeshwa kwa mchakamchaka wa kiaskari kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita, Rais Magufuli amemteua Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani kuiongoza taasisi hiyo huku akimwondoa kamishna mwingine wa polisi, Valentino Mlowola aliyemteua awali.

Katika mazingira hayo hayo, tukio hili limekuja miezi kadhaa baada ya Rais kumteua Brigedia Jenerali anayetoka katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo.

Sitakuwa nimekosea iwapo nitaandika bayana kwamba uteuzi wa Rais katika Takukuru pamoja na sababu zote nyingine, ikiwamo ile ya mchakamchaka wa kiaskari, unaonesha dhamira yake pengine kuongeza nidhamu ya kazi na pengine uwajibikaji na uadilifu kijeshi katika taasisi hiyo.

Kilichonigusa na kunifikirisha katika hili la Rais kulazimika kufanya mabadiliko mara mbili katika Takukuru hata baada ya yeye mwenyewe kutaja sababu zake, ni athari za utendaji na uwajibikaji ambazo zinaweza kutokana na hatua hiyo.

Kwa maoni yangu, utendaji wa kazi na uwajibikaji wenye tija kitaasisi katika taasisi nzito kama Takukuru unategemea sana pamoja na mambo mengine, ujuzi na uzoefu wa kazi wa mkuu au wakuu wake, sambamba na uelewa wao mpana wa changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa hapo.

Desemba mwaka 2015, ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya kuapishwa kuwa Rais, JPM alimteua Kamishna Mlowola kuwa Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, akiwa msaidizi mkuu wa aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, Dk. Edward Hoseah.

Siku chache tu baadaye, wakati ndiyo kwanza ana siku 42 tu Ikulu, alitangaza kutengua uteuzi wa Dk. Hoseah na akamteua Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu kabla ya kumthibitisha Machi 13, mwaka juzi.

Hoseah aliondoka Takukuru akiwa ameshika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo kwa muda wa takriban miaka tisa, tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006.

Ikumbukwe tu kwamba kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Hoseah ambaye katika uongozi wake alikabiliana na changamoto nyingi kubwa kubwa, alikuwa Mkurugenzi wa Operesheni katika taasisi hiyo hiyo akifanya kazi chini ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wake, Meja Jenerali Anatory Kamazima enzi hizo ikiitwa Takuru.

Hadi wakati Meja Jenerali Kamazima anaondoka Takuru (baadaye Takukuru) mwaka 2006, alikuwa ameiongoza taasisi hiyo tangu mwaka 1990, akifanya kazi kwa mara ya kwanza chini ya uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi, akadumu kipindi chote cha Rais Benjamin Mkapa na kwa miezi kadhaa na Rais Kikwete.

Kwangu mimi, kipindi kirefu ambacho Meja Jenerali Kamazima na Hoseah walifanya kazi katika taasisi hiyo, kiliwapa fursa ya kulifahamu kwa mapana na marefu tatizo la rushwa katika taifa letu na kimsingi muda wote huo ulikuwa darasa zuri kwao, kwa taasisi na kwa taifa katika kujua mwelekeo wa kukabiliana na tatizo hili la kihistoria.

Naamini wasomaji wengi wa safu hii wanajua kwamba Mkapa aliingia madarakani mwaka 2005 akiwa amebeba ajenda ya rushwa mabegani mwake kwa kiwango cha marafiki na mashabiki zake kumpachika jina la ‘Mr. Clean’, akitanabahishwa na usafi usio na doa.

Wakati Mkapa akiingia madarakani, alikuta taifa likihitimisha miaka 10 ya kaulimbiu ya ‘fagio la chuma’ iliyobuniwa na Rais Mwinyi kama chagizo la Serikali yake kukabiliana na rushwa pasipo hiyana.

Wengi tunajua kuwa kelele za rushwa ndizo ambazo zilimfanya Mkapa alipoingia madarakani tu aunde Tume ya Kuchunguza Mianya ya Rushwa iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ambayo ilipokamilisha kazi yake, Kamazima na Hoseah walipewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa matokeo ya uchunguzi wake.

Ilikuwa hivyo hivyo pia wakati Kikwete alipoingia madarakani na kumpandisha cheo Dk. Hoseah, wakati Kamazima akistaafu na akaendeleza mapambano ya rushwa ambayo yalizaa sheria mpya ya rushwa na taasisi mpya ya rushwa ambayo ndiyo leo inaitwa Takukuru.

Historia hiyo niliyoiandika kwa muhtasari tu, ni ushahidi wa wazi kwamba safari ya mapambano dhidi ya rushwa si ya leo, jana au juzi bali pengine ina umri sawasawa na maisha ya taifa hili kabla na baada ya Muungano wa mwaka 1964.

Kwa sababu hiyo basi, Rais na wasaidizi wake wakuu ambao leo hii ndio majemedari vinara wa mapambano ya rushwa, wanapaswa kutambua kwamba taasisi nyeti ya kupambana na rushwa inapaswa kufanya kazi katika misingi tulivu na isiyo na misukosuko hasa hii ya kiuteuzi.

Wakati nikilisema hili kwa Rais na wasaidizi wake, ujumbe huu unapaswa pia kuwagusa viongozi wanaopewa dhamana ya kuteuliwa kuwa wakuu wa taasisi hiyo, kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ipasavyo kwa viwango na kasi ya Rais aliyewateua.

Katika hili pamoja na mafindofindo yote ya kihistoria, nina kila sababu ya kuwaamini watangulizi watatu wa JPM ambao waliiacha Takukuru na kabla yake Takuru ifanye kazi kwa weledi na kwa utulivu wakati wote walipokuwa madarakani katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Ninapogeuka nyuma leo na kutafakari historia ya mapambano ya rushwa katika taifa hili na kuangalia kile kinachoendelea Takukuru leo, ambako tayari katika kipindi cha miaka mitatu tu ya Rais ameshafanya kazi na wakuu watatu wa taasisi hiyo na akifanya uteuzi mara mbili, napata ukakasi mkubwa kifikra.

Ikumbukwe tu kwamba Dk. Hoseah aliondoka kwa Rais kutengua uteuzi wake kwa namna ile ile ilivyofanyika kwa Mlowola ambaye alidumu Takukuru kwa miaka miwili na ushee.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwa mtendaji mkuu wa kariba ya Dk. Hoseah aliyefanya kazi kwa miaka tisa kama mtendaji mkuu na kabla ya hapo kama ofisa wa juu wa taasisi ya kupambana na rushwa, kumaliza kazi ngumu na yenye majaribu mengi kwa uteuzi wake kutenguliwa na si kwa kustaafu.

Ni jambo linalosikitisha na linaloibua maswali zaidi inapotokea mtendaji mkuu mwingine, Kamishna Mlowola naye akidumu katika nafasi yake kwa miaka miwili na miezi saba tu kabla ya Rais kumwondoa madarakani kwa sababu ambazo kazieleza bayana – kutoridhishwa na utendaji kazi wa kitaasisi.

Yaliyowapata Dk. Hoseah na Kamishna Mlowola yanapaswa yawe fundisho kubwa kwa Kamishna Diwani ambaye ndiye aliyerithi mikoba ya watangulizi wake ambao yumkini mwisho wao haukuwa mzuri.

Utamaduni wa kuweka jicho kali na tulivu katika Takukuru tuliouona ukifanywa na marais wastaafu, ulifanywa hivyo hivyo pia kwa taasisi nyingi nyingine nyeti kama Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mifuko ya hifadhi ya jamii na kwingi kwingineko.

Wakuu wa Polisi, IGP Said Mwema (2013 – 2013) na kabla yake IGP Omar Mahita (1995 – 2006) ni mfano mzuri wa wateule waliodumu katika nafasi zao kwa muda mrefu na kuleta tija kubwa katika jeshi hilo.

Wakati nikitamani kumwona IGP Simon Sirro akijifunza namna ya kudumu na kuepuka kadhia iliyomkuta mtangulizi wake IGP Ernest Mangu aliyedumu kwa miaka takriban mitatu tu, ni matamanio yangu kumwona JPM ambaye ndiye aliyeshika mpini akigeuka nyuma na kutazama mbele ya safari kwa kujiuliza kulikoni!

Nina kila sababu ya kuamini pia kwamba matukio ya namna hii yanazidi kumpa funzo kubwa na uzoefu zaidi Rais JPM ambaye ninawiwa kumwasa kufanya marejeo na kujifunza si kwa kuiga bali kwa kuhakikisha watu anaowateua katika nafasi nzito na nyeti kama hizo ni wale ambao watakidhi matakwa na matarajio yake.

Itoshe tu kueleza kwamba yanapotokea mambo ya namna hii ya utumbuaji wa wateule wazito katika kipindi kifupi,  inakuwa rahisi kukubaliana na wadadisi wa mambo na magwiji wa sayansi ya siasa ambao siku zote wamekuwa wakitaka kuona wanapoteuliwa watendaji wakuu wa taasisi na mamlaka nyeti kama Jaji Mkuu, Mkuu wa Takukuru, Mkuu wa Jeshi la Polisi na wengi wa aina yao wanapata baraka za Bunge kabla ya kuanza kazi.

Wakati tukiendelea kusubiri mchakato mrefu wa ndoto hizo za wachambuzi wa mambo kutimia, fikra na matamanio yetu yanapaswa kuelekezwa kwa Rais aliye madarakani ambaye bado Katiba inampa nguvu kubwa na mamlaka hayo ya uteuzi na utumbuaji ambao wala sipati shida kusema una ukakasi mkubwa.

Kwa sababu hizo basi, wakati tukibakia kujifunza mema na makosa yaliyotendwa na marais wastaafu – Kikwete, Mkapa, Mwinyi na hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, basi Rais Magufuli na wasaidizi wake wanapaswa kuanza mapema kuandika historia iliyotukuka ya uwajibikaji na maamuzi kabla haujafika wakati ambao kila kidole kitaelekezwa kwao huko TUENDAKO.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles