29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tuendako: Absalom Kibanda amkumbusha JPM, hekima za Martin Luther King Jr juu ya ukimya wa marafiki na usaliti…

Na Absalom Kibanda

ACHA nianze makala yangu ya leo kwa kurejea maneno ya kiongozi wa kidini na mwanaharakati maarufu wa Marekani, Martin Luther King Jr. aliyosema takriban miaka 50 iliyopita.

Kwa nyakati mbili tofauti, mwanaharakati huyo alizungumzia juu ya dhana ya ‘ukimya’.

Alifanya hivyo kwa mara ya kwanza Aprili 30 mwaka 1967 alipozungumza katika hadhara moja ya kichungaji na kutoa maoni yake dhidi ya uamuzi wa taifa lake kupigana vita Vietnam.

Akihubiri katika hadhara hiyo, Luther King Jr. ambaye alikuwa ni mchungaji wa Kanisa la Baptist, alianza kwa kusema; ‘a time comes when the silence is betrayal. That time has come to us’. Kwa kifupi alisema ‘kuna wakati unafika ukimya hugeuka na kuwa usaliti. Wakati huo umefika’.

Akizungumza katika hadhara nyingine, alizungumzia pia juu ya athari ya ukimya huo huo na akaenda mbele zaidi kwa kusema; ‘at the end we will remember not the words of our enemies but the silence of our friends.’

Ujumbe ulio nyuma ya maneno hayo ndio hasa ulionisukuma kufikia uamuzi wa kuandika waraka mrefu wa ushauri wenye sehemu sita ambao ninauhitimisha leo, nikiuelekeza kwanza kwa Rais wangu na kaka yangu, Daktari wa Falsafa (PhD) katika masuala ya kemia, John Pombe Joseph Magufuli.

Mbali ya kujaribu kumshauri Rais, waraka huu kwa makusudi ulijaribu kumkumbusha JPM mwenyewe na Watanzania wenzangu kwa ujumla kwa ufupi, safari ndefu ya kisiasa iliyoanza mwaka 1995, zama Benjamin Mkapa akiwa rais, ambayo hatimaye imemfikisha kiongozi huyo katika kilele cha mamlaka ya juu ya umma.

Wakati nikifikia tamati si kwa ushauri, bali katika kumuasa Rais JPM kuyaangalia mapito yake na kuzingatia darasa la umakini, uthubutu, ujasiri, woga na ushupavu kutoka kwa mwalimu wake Mkapa.

Ninaguswa kumuasa Rais wangu na Serikali yake kutafakari upya na kwa umakini mkubwa mwelekeo wa kisera na kimaamuzi ambao Serikali imeuchukua na inaendelea kuuchukua tangu alipoingia madarakani Novemba 5, 2015.

Kwanza, napenda kumwomba Rais kwa dhati, atafakari upya uamuzi ambao chimbuko lake si yeye bali Serikali na CCM ya Kikwete ya kulibana Bunge kwa kiwango cha baadhi ya watu kufikia hatua ya kuona na kuamini kwa makosa au kwa usahihi kwamba mhimili huo wa dola umepoteza maana.

Katika hili, JPM anapaswa kutambua kwamba pamoja na udhaifu wa Bunge au makosa ya wabunge, mhimili huo ndio hasa uliomwibua yeye kwa kiwango cha kumtofautisha na wenzake tangu akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi (1995-2000) na ukamjenga na ukamuimarisha hata kufikia hatua ya kuonekana anafaa kuwa Rais.

Wakati akitafakari kuukubali au kuukataa ushauri wangu huu, JPM anapaswa kukumbuka namna alivyopata umaarufu mkubwa alipokuwa akipambana kwa hoja na wabunge makini wa upinzani wa kariba ya Mabere Marando, Masumbuko Lamwai na wengine wakati akiwa kijana mdogo.

Si hilo tu, JPM anapaswa kukaa chini na kutafakari namna safari yake ya kisiasa na ile ya uongozi ilivyopata changamoto nzito na nyingi ndani na nje ya Bunge wakati taifa lilipokuwa likielekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 wakati alipokuwa Waziri wa Ujenzi.

JPM ambaye ni mmoja wa wanasiasa wenye kumbukumbu nzuri ya mambo mengi hata yale madogo, naamini bado anakumbuka mwaka 2005 alilazimika kutangaza mapema kwamba alikuwa hana mpango wa kugombea urais.

Baadhi yetu bado tunakumbuka vyema kwamba ushawishi mkubwa aliokuwa nao bungeni ndio ambao uliwatia hofu kubwa makada wenzake ndani ya CCM, ambao baadhi yao walifikia hatua ya kumwona kama mwanasiasa tishio kwa urais, aliyepaswa kuzuiwa kwa namna yoyote iliyowezekana.

Ni wakati huo uliokuwa na majaribu mengi, siku moja akiwa bungeni, JPM aliugua ghafla na akakimbizwa hospitali, kwanza Dodoma, baadaye Dar es Salaam na mwishoni nje ya nchi kutibiwa, hali ambayo baadaye ilihusishwa na harakati za urais wa mwaka 2005.

JPM na sisi wachambuzi wa masuala ya siasa tunapoona Bunge likiminywa leo na Watanzania kunyimwa fursa ya kufuatilia kwa ukamilifu vikao muhimu vya mhimili huo, tuna kila sababu ya kujiuliza tutawezaje kuwajua akina JPM wengine, marais wajao wa taifa hili?

Fikra hizo zinanirudisha nyuma na kunifanya nitafakari, hivi ingetokea Rais Mkapa na baadaye Kikwete wakaliminya Bunge kwa kiwango cha leo hii, Watanzania tungewajuaje akina Magufuli!

Bado naamini kwa dhati kwamba JPM japo yuko Ikulu leo katika jumba takatifu, kwa maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, anayo kumbukumbu ya mazungumzo juu ya uongozi na hatima ya taifa ambayo mara kadhaa miye na yeye tulipata kuyajadili wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Nitashangaa iwapo JPM atakuwa amesahau kwamba alipopelekwa katika wizara hiyo na baadaye Wizara ya Mifugo na Uvuvi kulikuwa na maneno mengi nyuma, kwamba lengo lilikuwa ni kufuta ‘legacy’ yake aliyoijenga wakati akiwa Wizara ya Ujenzi kwa miaka 10 ya Mkapa.

Naamini JPM anatambua kwamba vijana wa aina ya Anthony Mtaka ambao walianza mapema sana kumshauri agombee urais mwaka 2015 tangu mwaka 2011/2012, walifanya hivyo kwa sababu ya rekodi aliyoiweka bungeni.

Si hilo tu, JPM anapaswa kutambua pia kwamba fikra zilizochochewa tangu mwaka 2014 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye alianza kuwashawishi watu wake wa karibu ndani ya chama hicho kuanza kumfikiria kwa urais, hazikutokana na lolote zaidi ya rekodi yake ya uwaziri iliyobainishwa akiwa bungeni.

Ni dhahiri kwamba kama lisingekuwa Bunge, Kinana ambaye alimjengea JPM uhalali kwa wasaidizi wake wakuu hata ukawashawishi marais Kikwete, Mkapa, Mwinyi na makada wengine wengi ambao kabla walionekana na kudhaniwa kuwa mateka wa makundi makubwa mawili ya urais ndani ya CCM ya wakati huo ya Edward Lowassa au Bernad Membe asingefanikiwa.

Siku mbili kabla sijaanza kuandika sehemu ya mwisho ya ushauri wangu huu kwa JPM, nilisikiliza hotuba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliyoitoa siku chache baada ya Tume ya Nchi za Kusini ambayo yeye mwenyewe alikuwa mwenyekiti wake kukamilisha kazi.

Katika hotuba yake hiyo ambayo nina kila sababu ya kumuasa JPM kuirejea, Mwalimu alizungumzia misingi ya maendeleo ambayo ilisababisha mataifa ya kusini kukwama wakati yale ya kaskazini yakipiga hatua.

Mwalimu katika hotuba yake hiyo alisema bayana kwamba maendeleo sharti yawe ya watu na nje ya hapo hakuna maendeleo.

Katika moja ya misingi ya maendeleo ambayo Tume ya Kusini ilikuja nayo ni lile lililohusu uhuru wa watu, ambalo kwa maneno yake mwenyewe Mwalimu alizungumzia demokrasia.

“Watu hawawezi kusema wana maendeleo wakati katika nchi yao hawawezi kutembea kwa uhuru, wanaogopa, wanahofu, wanadhani asubuhi wakisikia mlangoni kwao mtu anagonga  wanajua kuna mtu kaja kuwachukua anakwenda kuwafunga. Nchi ya namna hiyo haiwezi kusema ina maendeleo,” alisema Mwalimu katika hotuba hiyo.

Japokuwa Tanzania bado haijafikia hatua hiyo aliyoizungumzia Mwalimu, lakini ni wazi kwamba katika siku za karibuni kumekuwa na sheria kali kali kama zile za makosa ya mitandao, takwimu na nyingine ambazo mbali ya kupitishwa na Bunge ambalo wananchi hawana fursa ya kulifuatilia kwa ukaribu kama ilivyokuwa awali, zina viashiria vya kuminya uhuru wa watu hata kuwajengea hofu.

Katika hili, ushauri wangu haupaswi kwenda kwa Rais wangu tu, bali pia kwa washauri wake na wanasheria wetu ambao nao wanapaswa kutambua kwamba kuminya uhuru wa watu kufikiri pasipo hofu ni moja ya mambo ambayo kwa utamaduni wa mataifa yetu, tulipaswa kuwa tumeshaachana nayo miaka mingi iliyopita.

Uhuru huu ambao Tume ya Nchi za Kusini iliuweka katika mwamvuli mpana wa pili, unanifikisha katika suala langu la pili kwa kumuasa Rais JPM kutafakari upya juu ya mwenendo wa siasa na demokrasia ya hapa nchini inayogusa si tu vyama vya siasa, bali pia uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa habari Tanzania.

Katika hili, nina kila sababu ya kumweleza waziwazi Rais wangu kwamba Watanzania wenye akili timamu tunakerwa na hatua ya madiwani na wabunge waliochaguliwa kujivua uanachama wa vyama vyao na kisha kujiunga na vyama vingine na kisha kugombea nafasi zile zile.

Katika hili, Mheshimiwa Rais anapaswa kunielewa kwamba wala siungani na wale wanaodai kwamba hamahama ya wawakilishi hao wa kuchaguliwa ni mzigo mkubwa kwa nchi.

Hoja yangu ni rahisi. Matendo haya ni ya fedheha, dhihaka na matusi kwa demokrasia ambayo msingi wake ni kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi katika kipindi cha miaka mitano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwingine.

Binafsi nilianza kukerwa na hatua hii ya kipuuzi katika historia ya demokrasia ya vyama vingi nchini tangu nilipomsikia aliyekuwa Mbunge wa Singida Kusini kwa tiketi ya CCM, Lazaro Nyalandu alipotangaza kujivua ubunge na siku chache baadaye akahamia Chadema.

Kwa maono yangu, Nyalandu kama ilivyo kwa wanasiasa wenzake waliokuwa wabunge wa upinzani kabla ya kujiunga na CCM na kisha wakarudi tena bungeni, huko tuendako wataingia katika kundi la wasaliti wa demokrasia na maendeleleo ya wananchi.

Jambo la tatu na la mwisho ambalo nimeligusia mara kadhaa katika safari yangu ya ushauri kwa Rais kupitia mfululizo huu wa makala, ni lile linalogusa mustakabali mwema wa mhimili wa nne wa dola, vyombo vya habari.

Nilipata kuandika. Mkapa hakufanya vyema sana katika hili kwa sababu ya woga. Hata hivyo woga huo wa Mkapa kuwaogopa akina Reginald Mengi, Jenerali Ulimwengu, Salva Rweyemamu na wanahabari wengine kadhaa, ulimfanya afikie uamuzi wa kumshawishi Aga Khan kuwekeza katika vyombo vya habari nchini, uamuzi ambao uliliimarisha gazeti la Mwananchi na Mwanaspoti, ukazaa gazeti la Kingereza la The Citizen na kujenga Kampuni ya Mwananchi Communications kwa ujumla.

Ni dhahiri kwamba woga wa Mkapa ulikuwa chachu muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini kwa kuongeza wigo wa uhuru wa habari na kuchochea maendeleo ya demokasia kwa ujumla wake. Ni bahati mbaya kwamba Mkapa aliishia hapo na hakutaka kufanya zaidi ya hilo alilofanya.

Pamoja na woga wa Mkapa, mbegu aliyopanda kwa kuimarisha sekta binafsi ilistawisha vyombo vya habari na kimsingi ikaimarisha weledi wa kitaaluma wa tasnia hiyo.

Ni bahati mbaya kwamba msingi alioujenga Mkapa wa kuvijengea imani vyombo vya habari hata katika mazingira ya kunangwa na kunyoshewa vidole vingi, ndiyo uliotumika kama ngazi ya kumwingiza Kikwete madarakani mwaka 2005.

Mbegu hii iliyojengwa wakati wote wa Kikwete, kwa kiwango kikubwa ndiyo ilizaa chuki na dharau kwa vyombo vya habari kabla na baada ya Serikali ya JPM kuingia madarakani. Hili ni tukio la bahati mbaya.

Kwa sababu hiyo basi, nina kila sababu ya kumuasa JPM kukaa chini na kuanzia pale alipoishia na kukwama Mkapa kwa kuamsha upya uhuru na weledi wa kitaaluma kwa wanahabari na vyombo vya habari.

Katika hili, kama tunaweza leo tukamkumbuka na kumuenzi Mkapa kwa kuchochea kuanzishwa kwa gazeti la The Citizen na kuimarishwa kwa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti sambamba na kustawi kwa magazeti kama ya Mtanzania, Nipashe, Rai, televisheni na redio nyingi wakati wake, basi JPM anapaswa kufanya vyema zaidi.

Nitakuwa msaliti wa aina ile aliyosema Martin Luther Jr. iwapo nitakaa kimya wakati ninapowasikia wachambuzi na watu makini wakiihusisha Serikali ya JPM ninayemfahamu kwa miaka mingi ni vijigazeti pendwa kadhaa vya hovyo ambavyo leo hii ndivyo vinavyoonekana kushabikiwa na wakubwa waliopewa dhamana ya kuliongoza taifa.

Hakika huu haupaswi kuwa urithi ambao JPM atauacha wakati atakapomaliza kipindi chake cha urais. Ikulu ni mahali patakatifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles