30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TUENDAKO: ABSALOM KIBANDA AENDELEZA USHAURI WAKE KWA JPM. SASA AMUASA KUUKATAA WOGA WA MKAPA…

Na Absalom Kibanda                                   |                                       


NAANDIKA makala hii leo wakati Rais John Magufuli akiwa ziarani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako tayari ameshatembelea mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu na sasa Singida.

Hakuna shaka kwamba, ziara hiyo ya Rais katika mikoa ya Kanda ya Ziwa imeacha alama nyingi kubwa na muhimu si tu kwa mustakabali wa mikoa ya Kanda ya Ziwa bali pia hata kwa maeneo mengine mengi nchini.

Ninao uhakika kwamba, ziara hiyo ya Rais ambayo pia ilihusisha mawaziri wake kadhaa itakuwa chachu kwa viongozi na wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Lakini pia itakuwa ni maandalizi ya msingi kwa viongozi wa mikoa mingine ambao nao wanajiandaa kukutana na rais atakapofika katika maeneo yao.

Katika safu hii na hususani kwa kuzingatia muktadha wa mfululizo wa makala hizi ambazo zinamgusa mkuu wetu wa nchi, ziara yake imekuwa ni ufunguo muhimu na rejea muhimu kabisa kifikra.

Kauli na maamuzi aliyotoa Rais akiwa ziarani kwa namna kubwa yamezidi kutoa mwelekeo wa aina yake kwa kile ambacho kila siku amekuwa akikiita ‘Tanzania Mpya’ ya ndoto zake.

Kwa namna kubwa, kupitia katika ziara yake hiyo, JPM ameendelea kujipambanua kuwa Rais ambaye ameamua kuchukua mwelekeo wa kimaamuzi unaotofautiana na ule wa watangulizi wake.

Kauli na maamuzi ambayo amekuwa akiyatoa akiwa ziarani, japo mengine yamekuwa yakibeba ukakasi mkubwa akilini, yanazidi kumfanya kila siku, aendelee kujipambanua kuwa Rais aliyekataa katakata kuongoza kwa mazoea.

Sijui ni kwa bahati mbaya au kwa makusudi, ziara hiyo ya Rais ambayo inafanyika katika kipindi kile kile ambacho vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano vinaendelea mjini Dodoma imejumuisha pia mawaziri wanaotoka katika mikoa aliyotembelea.

Kama hiyo haitoshi, ziara hiyo ya JPM ambayo kwa mara ya kwanza anaifanya akiwa peke yake pasipo kuongozana na mkewe, Mama Janeth Magufuli ambaye katika siku za karibuni, mama huyo kipenzi cha watu, hajaonekana hadharani.

Binafsi, kupitia ziara hiyo ya Rais, nimejifunza mengi yanayohusu uongozi na uwajibikaji miongoni mwa viongozi ukianzia rais hadi watendaji wa mitaa na kata ambao JPM kwa makusudi amewashirikisha moja kwa moja kila alipopita.

Kwa namna ya pekee, JPM ameonesha ujasiri wa kuchukua maamuzi ya papo kwa papo, kutoa kauli za miongozo na maamuzi, kukataa hoja za mawaziri, wabunge na watendaji mbalimbali waliojitokeza katika ziara yake.

Hulka hiyo ya JPM ilinirejesha katika moja ya maeneo ambayo kwa kiwango kikubwa yanafanya rais wa sasa kujipambanua na kujitofautisha sana na kiongozi aliyemuibua katika siasa za kitaifa, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

Kama kuna eneo ambalo nililenga kumshauri JPM ambalo nimekuwa nikitamani siku zote awe kinara wa kulikataa kama urithi kutoka kwa baba yake wa kisiasa basi hilo si jingine bali hulka ya woga.

Mkapa ambaye katika sehemu tatu za awali nilimwelezea kama kiongozi shupavu aliyejenga misingi imara ya uchumi na kusimamia ipasavyo nidhamu ya utendaji wa kazi wa Serikali yake, hata kufikia malengo kadha wa kadha ya kutukuka aliondoka akiacha nyuma doa kubwa la woga.

Sina shaka hata kidogo kuandika kwamba, Ben, kama alivyokuwa akijulikana miongoni mwa marafiki zake wa karibu, anaweza akaingia katika historia ya marais waoga kupata kutokea.

Katika makala zilizotangulia, niliutaja kwa sehemu woga wa Mkapa pasipo kuunyumbulisha na kuuelezea kwa kina kwa sababu mbalimbali.

Hulka ya Mkapa ya ‘kusalimu amri’ kila wakati alipokutana na mashinikizo ambayo yaliyosababisha mawaziri wake kadhaa kuanguka kwa kujiuzulu au yeye kulazimika kuwabadili pamoja na sababu zote nyingine.

Kama asingekuwa mwoga, Ben alikuwa hana sababu ya kuruhusu mawaziri wake wawili, Profesa Simon Mbilinyi na Juma Ngasongwa kujiuzulu uwaziri kwa kashfa ambazo zilihitaji Rais mwenye ujasiri wa JPM kuzijibu na kuwagomea wabunge.

Mkapa angekuwa Rais mwenye uthubutu wa kariba ya JPM asingeweza kukubali kuona Waziri wa Viwanda na Biashara, Iddi Simba aliyeshinikizwa na Bunge kwa hoja nyepesi kuwajibika apoteze uwaziri hata kusababisha mabadiliko ya shuruti ya Baraza la Mawaziri.

Woga wa Mkapa ndiyo uliomfanya akose ujasiri wa kuisimamia vilivyo Serikali yake katika kuitekeleza Ripoti ya Tume ya Kuchunguza Mianya ya Rushwa maarufu kwa jina la Tume ya Warioba aliyoiunda mwenyewe siku chache tu baada ya kuingia madarakani.

Ni wazi kwamba, iwapo Mkapa angekuwa na ujasiri wenye tija na wa kufumba macho kuhusu kadhia ya rushwa huenda leo hii kilio cha ufisadi ambacho kimeendelea kuzitafuna serikali za CCM tangu wakati huo hadi leo kingekuwa kimeshakoma.

Kigugumizi alichopata Mkapa katika kulifumua na kuliunda upya Jeshi la Polisi, Idara ya Mahakama na taasisi nyingi nyingine za umma ambazo zilitajwa kuwa vinara wa rushwa wakati wa muhula wa kwanza wa urais wake ndiyo msingi wa matatizo ambayo JPM anakabiliana nayo leo hii.

Itoshe tu kueleza kwamba, woga wa Mkapa kwa vyombo vya habari ambavyo viliitikisa Serikali yake katika kipindi chote cha uongozi wake, ndiyo msingi mama wa mkwamo wa weledi wa kitaaluma wa wanahabari wengi na tasnia hiyo nzima kwa ujumla hadi leo hii.

Kama kuna kipindi ambacho taaluma ya habari ilipaswa ikue na ikomae si kibiashara bali kiweledi, basi kilikuwa ni kipindi ambacho Mkapa ambaye ni mwanahabari kihistoria alikuwa Rais.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba, katika kipindi chote akiwa madarakani, Mkapa aliishia kuvisuta vyombo vya habari na wanahabari wa Tanzania akisema walikuwa ni watu ambao siku zote walikosa weledi na uwezo wa kuchambua mambo kwa kina.

Wakati akivisuta vyombo vya habari vya ndani na kuvisifia vile vya nje kwa weledi na umakini, taifa lilipigwa na butwaa wakati Mkapa huyo huyo alipohamaki wakati fulani alipokuwa akihojiwa na mmoja wa wanahabari nguli duniani Tim Sebastian wa Kituo cha Televisheni cha CNN.

Kwa namna ya kustaajabisha na ile ile aliyokuwa akiwafanyia wanahabari wa Kitanzania, Mkapa alimtuhumu mwanahabari huyo wa CNN kwa kuchukua taarifa nusu nusu na zisizo sahihi na kuziamini.

Kitendo hicho cha Mkapa ambacho JPM anapaswa kukikataa mapema leo akiwa madarakani, kilikuwa ni jibu bayana kwamba, kumbe kwake tatizo halikuwa ubora wa wanahabari au vyombo vya habari vya Tanzania bali, hulka yake ya woga kwa tasnia hiyo kwa ujumla wake.

Katika hili la vyombo vya habari, JPM anapaswa kuendeleza hulka aliyokuwa nayo wakati akiwa waziri ya kuwa na imani na ujasiri wa kufanya kazi na vyombo vyote vya habari vya umma na binafsi ambavyo vinatimiza wajibu kwa kuzingatia weledi wa kitaaluma.

JPM ambaye katika ziara yake Kanda ya Ziwa na tangu akiwa Rais ameonesha ujasiri wa kufanya na kutenda hata kile ambacho wasaidizi na washauri wake hawakitaki. Ana kila sababu ya kuitokomeza mbegu ya woga iliyopandwa na Mkapa na ikamea na kustawi wakati wa Rais Jakaya Kikwete.

Ni jambo la bahati mbaya kwa maoni na mtazamo wangu kwamba, kuna kila dalili na viashiria kwamba, wasaidizi wengi wa Rais ambao wao ndiyo hasa walichochea na kupanda mbegu za hofu na woga dhidi ya vyombo vya habari wakati wa Mkapa na Kikwete ndiyo hao hao ambao leo wana nafasi na mamlaka katika taasisi za umma.

Katika orodha ya watu wa namna hiyo, yuko kaka na ndugu yangu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa  na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye yeye mwenyewe tangu akiwa mbunge, amekuwa kinara wa kuwananga waandishi na vyombo vya habari vya Tanzania kwa kiwango kile kile cha Mkapa.

Wakati nikieleza wasiwasi wangu dhidi ya woga wa Rais Mkapa, Dk. Mwakyembe na watendaji wengine serikalini dhidi ya vyombo vya habari na wanahabari wa Tanzania, napenda nieleweke mapema kabisa, ziko hoja za msingi ambazo watu hao pamoja na hofu zao wamekuwa nazo.

Nasema hivi kwa sababu ninajua kwa uhakika kabisa kwamba, vyombo na tasnia nzima ya habari inao udhaifu mwingi wa kitaaluma, kiweledi na kihulka ambao viongozi akiwamo Rais JPM na wasaidizi wake wakuu wana kila sababu ya kuuelezea, kuunyooshea vidole, kuukosoa na ikibidi kuchukua maamuzi ya kujenga.

Rais JPM anapaswa kutambua tu kwamba ni jambo la bahati mbaya kwamba, hulka ya woga iliyozaa chuki imekuwa ndiyo msingi na mwongozo wa kauli na maamuzi mengi ya viongozi wakuu na wa juu serikalini kila mara vyombo vya habari au waandishi wa habari wanapofanya makosa ya kitaaluma au ya kibinadamu.

Woga uliozaa chuki huua. Tutaendelea wiki ijayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles