33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tshisekedi aomba msaada Sadc kudhibiti ebola, kikundi cha MTN

NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

NCHI wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) zimeombwa kuchukua jitihada kukabiliana na matishio ya ugaidi na ugonjwa wa Ebola.

Maombi hayo yaliwasilishwa na rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati wa mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo unaoendelea nchini.

Rais Tshisekedi alisema nchi yake bado imeendelea kukabiliwa na matishio ya usalama hasa katika eneo la Mashariki kutokana na kuwapo kwa kikundi cha MTN ambacho kinatumia mfumo wa kushambulia kwa mtindo wa ugaidi.

“Ndiyo maana nilitengeneza mkakati wa kuimarisha mamlaka ya serikali ili kuzuia kundi hili kuendelea na tumeweka mfumo wa mapatano kwa makundi yote ili kusaidia kurejesha amani.

“Mtusaidie tuwe na mshikamano ili kupitia kwenu tutoke na tamko litakalosaidia kuimarisha kundi la Monusco (Majeshi ya walinda Amani ya Umoja wa Mataifa) ili liweze kukabiliana na makundi hasimu,” alisema Rais Tshisekedi.

Pia aliziomba nchi wanachama kuunda kundi la kikanda litakalosaidia kutokomeza vikundi vya kigaidi ambavyo vimekuwa tishio kwa baadhi ya nchi.

Kuhusu ugonjwa wa Ebola alisema wanashirikiana na Shirika la Afya duniani  (WHO) na tayari wamechukua hatua mbalimbali kuudhibiti na kutaka nchi wanachama kuendelea kuwasaidia kuudhibiti.

Pia alizihimiza nchi wanachama kuendeleza ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ili kuwa na nishati ya kutosheleza mahitaji ya Sadc.

“Katika suala la kilimo nchi zetu zina fursa nyingi sana na sisi tuko tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali, naamini mkutano huu wa marais na viongozi wa serikali utafikia uamuzi thabiti wa kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya kuimarisha viwanda ili kuwa na maendeleo jumuishi,” alisema.

Naye Andry Rajoelina wa Madagascar alisema ni muhimu nchi wanachama kuwa na malengo ya kukuza ukuaji wa uchumi na viwanda ili kutoa fursa nyingi za ajira na kuboresha uchumi ndani ya nchi zao.

“Sisi Madagascar tumefanya mabadiliko ya sera mbalimbali ili tuweze kufikia ndoto yetu ya pamoja kama Afrika. Tunahakikisha kunakuwa na usalama wa chakula na lishe, elimu kwa wote, kukuza ujasiriamali na kuongeza kiwango cha bidhaa tunazosafirisha nje ili tulitumie vizuri soko la Sadc.

“Sadc isiwe taasisi ya kutukutanisha tu, tunachotarajia ni kupata matokeo kamili, iweke msisitizo kwa nchi wanachama na kuwa chombo kitakachokuza uchumi wetu na kuhakikisha bara la Afrika linaendelea,” alisema Rais Rajoelina.

Alisema yeye ni kiongozi kijana kuliko wote lakini nia ya kutaka kutenda haiangalii umri wa mtu huku akitaka Afrika isijikite zaidi kwenye midahalo bali utekelezaji wenye vipimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles