TRUMP: MAZOEZI YA KIJESHI NA KOREA KUSINI YATATISHA

0
460

 

WASHINGTON, MAREKANI


Rais Donald Trump amesema kutokana na Korea Kaskazini kutotimiza ahadi zake kuhusu silaha za nyuklia, nchi yake inatarajia kufanya mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi na Korea Kusini.

Pia aliikosoa China kwa kile alichosema kuhujumu jitihada zake na Korea Kaskazini kipindi hiki, ambacho kuna malalamiko Kaskasini kutoonyesha dalili za kuharibu silaha zake za nyuklia.

Kupitia ujumbe wa Twitter, Trump alisema hakuna sababu ya kutoendelea tena na mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini ambayo yamekuwa yakiikasirisha Kaskazini.

Mkutano kati ya Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un uliofanyika Juni mwaka huu, ulikamilika kwa ahadi kutoka Korea Kaskazini kuharibu silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea.

Baadaye Trump alitangaza kuwa hakukuwa tena na tisho kutoka Korea Kaskazini.

Lakini tangu wakati huo, waangalizi wengi wanasema Korea Kaskazini haionyeshi kutimiza ahadi ya kuachana na silaha za nyuklia.

Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa Twitter, Trump alisema Kaskazini iko chini ya shinikizo kutoka China kwa sababu ya mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na taifa hilo.

China ndiyo mshirika pekee wa Korea Kaskazini na inatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kwenye maamuzi yake na ndiye mshindani mkubwa wa Marekani na wa muda mrefu eneo hilo.

Marekani na China ziko kwenye mvutano mkubwa wa kibiashara na kila upande umeziwekea ushuru bidhaa za mwingine.

Tangu mkutano wa Juni, Korea Kaskazini imesitisha majaribio yake ya nyuklia, ikidai kuharibu kituo cha kufanyia majaribio hayo na ikarudisha mabaki ya wanajeshi wa Marekani waliouawa wakati wa vita ya Korea mwaka 1950-53.

Lakini Trump ameilaumu Korea Kaskazini kwa kile alichokitaja kuwa kutokuwepo maendeleo katika makubaliano yake ya kuharibu silaha za nyuklia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here