25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Trump, Hillary watoana jasho majimboni

0412trumpclintonmissouri

Na Justin Damian, North Carolina

ZOEZI la upigaji kura za mapema (early voting) linaendelea katika majimbo (States) mbalimbali ya hapa Marekani. Tofauti na Tanzania, Wamarekani hupewa muda wa kupiga kura kabla ya siku ya uchaguzi ili kuepukana na foleni ndefu siku hiyo na pia kuwapa watu muda wa kutosha kupiga kura. Wakati uchaguzi wa Tanzania ukiwa unafanyika siku ya Jumapili ambayo si siku ya kazi, kwa hapa Marekani hali imekuwa tofauti. Wamarekani hufanya uchaguzi siku ya kazi na siku hiyo haina mapumziko. Watu hupanga muda wao vizuri ili waweze kwenda kazini lakini pia wapate muda wa kupiga kura.

Kwa kawaida, majimbo huwa na taratibu tofauti tofauti. Yapo baadhi ya majimbo ambayo hutoa muda wa wiki mbili kwa watu kupiga kura kabla ya siku ya uchaguzi na mengine hutoa mwezi mmoja mpaka mwezi mmoja na nusu kabla ya uchaguzi

Majimbo mengi hapa Marekani likiwamo Jimbo la North Carolina, huruhusu watu kupiga kura za mapema bila kutoa sababu za kwanini wanataka kupiga kura mapema wakati majimbo machache huwataka wanaopiga kura za mapema kuwa na sababu maalumu kabla ya kuruhusiwa kupiga kura.

Mwandishi wa MTANZANIA aliyepo katika jimbo lenye ushindani mkubwa (swing state) la North Carolina, alipata nafasi ya kutembelea baadhi ya vituo vya kupiga kura katika mji wa West Asheville uliopo jimbo la North Carolina ambako alipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wapiga kura pamoja na wagombea.

Mengel Randell

Nasikitika sikuweza kupiga kura kwa ajili ya wagombea wa chama changu ambacho ni Green Party kwa ngazi ya seneta, majaji, makamishna na wengine. Ni mara yangu ya kwanza kupiga kura hapa North Carolina. Kabla ya kuhamia hapa West Ashiville, nilikuwa nikiishi Washington ambako niliweza kuwachagua viongozi wanaotoka katika chama changu. Nilipouliza kwanini wagombea wa Green Party hawapo kwenye uchaguzi nilijibiwa kuwa kuna vigezo ambavyo chama hakikutimiza na ndiyo maana hakikuweza kusimamisha wagombea.

Kwa ngazi ya urais sikumchagua Jill Stein ambaye ni mgombea wa chama changu cha Green Party. Kwa kumchagua Stein, ningekuwa nimepiga kura ya kumkataa Hillary Clinton na kwa maana hiyo ningekuwa nimemwongezea nguvu Trump ambaye nimekuwa nikipingana naye siku zote. Nimempigia Clinton kwa sababu sitaki Trump ashinde.

Kwa kipindi kirefu cha maisha yangu nimeishi Afrika kwenye nchi kama vile Congo-DR, Morocco na Cameroon ambako wazazi wangu walikuwa wakifanya kazi na Shirika la Misaada la Marekani. Demokrasia ya nchi za Kiafrika ambazo nimeishi si kama ya hapa Marekani. Hapa Marekani uchaguzi ni huru na wa haki tofauti na nchi nyingi za Kiafrika. Nafurahi kuwa kupitia kura yangu naweza kuleta mabadiliko.

Theo Noel

Nafurahi kuwa nimeweza kufika hapa na kupiga kura yangu mapema kwa urahisi na bila usumbufu. Jambo la kusikitisha ni kuwa sijamchagua rais kwa sababu  hakuna mgombea ambaye ameweza kunishawishi. Nimeona ni bora niwachague wagombea ambao nimewaona na kuwauliza maswali wakanijibu na nikaridhika nao.

Nikiwa kama Mmarekani mwenye asili ya Afrika, nilikuwa na imani kubwa sana na Rais Barack Obama, wakati anagombea na nilimpa kura yangu nikiamini angetusemea sisi weusi ambao tumekuwa tukibaguliwa kwenye kila kitu, kuanzia elimu mpaka ajira. Tangu Obama achaguliwe hajafanya chochote kwa ajili ya sisi weusi na hata hajaenda nyumbani kwao Chicago ambako ni chimbuko lake.

Nimefika hapa kupiga kura si tu kwa ajili yangu, nimekuja kuwawakilisha na wengine wengi wenye mtizamo kama wangu ambao kwa namna moja au nyingine wameshindwa kufika kupiga kura.

Chuck Arched

Mimi nagombea nafasi ya Mwenyekiti wa County ya Buncombe hapa North Carolina kwa kupitia chama cha Republican. Nipo hapa kwa ajili ya kuwaomba wapiga kura wanaokuja kupiga kura za mapema  wanichague ili niweze kuwa msimamizi katika County yao.

Matarajio yangu ni kuibuka mshindi. Kwenye ngazi ya urais sisi Republican tuna nafasi ndogo ya kushinda kutokana na aina ya mgombea ambaye tumemchagua. Binafsi namuunga mkono mgombea wetu wa urais na nitampigia kura japokuwa ni mgombea ambaye simkubali sana.

Katika ngazi ya urais chama chetu kimefanya makosa ambayo yanaweza kutugharimu. Kwa sasa hakuna tunachoweza kufanya kikubwa ni kuwa tumejifunza kutokana na makosa.

Lawrence Hines

Kura yangu ya urais nimempa mgombea wa Chama cha Democrat, Hillary Clinton. Nimemchagua Hillary kwa kuwa kwa kipindi chote ambacho amekuwa katika nafasi mbalimbali za uongozi amekuwa akisimama kwa ajili ya watu wasio na sauti kama wanawake na watoto.

Kwa mtizamo wangu naona Democrat wana sera nzuri ambazo zinajaribu kuwagusa watu masikini pamoja na kutoa kipaumbele kwenye elimu kuhakikisha kuwa elimu inapatikana kwa urahisi kwa Wamarekani wote.

Pamoja na kwamba hapa Nort Carolina ushindani ni mkali kati ya vyama hivi viwili vikubwa, watu wengi wamevutwa na sera za  Hillary Clinton na bila shaka atapata kura nyingi kutoka katika marika mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles