23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP ADAIWA KUITUKANA AFRIKA

NEW YORK, MAREKANI

RAIS wa Marekani, Donald Trump, amedaiwa kuwashutumu wahamiaji wanaoingia nchini humo kutoka Haiti, El Salvador na Bara la Afrika kwa kuwafananisha na uchafu kwa madai wanaharibu nchi hiyo hivyo wanapaswa kuzuiliwa.

Kwa mujibu wa gazeti la The Washington Post, limesema Trump alizungumza hayo juzi wakati alipokutana na Kamati ya Bunge katika majadiliano yao Ikulu na kuhoji ni kwanini Marekani inapokea wahamiaji kutoka nchi hizo badala ya nchi kama Norway.

“Wanasiasa fulani wa Washington hupendelea kupigania mataifa ya kigeni, lakini Rais Trump atawapigania raia wa Marekani pekee. Kama mataifa mengine ambayo yana wahamiaji wanaofaa kuwa nchini humo, Rais Trump anapigania suluhisho la kudumu linalofanya taifa hilo kuwa thabiti kwa kuwakaribisha wale ambao wana mchango katika jamii, hukuza uchumi wetu na kuingiliana na raia wa taifa letu,” ilisema taarifa ya Msemaji wa Ikulu, Raj Sha.

Aidha, kauli ya Trump ilidhihirisha kikwazo cha kupokea mamia ya wahamiaji pamoja na kuvurugwa mapendekezo ya maseneta 6 wa vyama vya Republican na Democrat ya kupokea wahamiaji zaidi kutoka mataifa ya kigeni.

Trump alithibitisha kuwa kamwe hatakubali mkakati wa muda mfupi ambao ni dhaifu na hatari kwani unahatarisha maisha ya raia wa Marekani, mbali na kutowaruhusu wahamiaji wanaotaka maisha mazuri wakiwa ugenini ijapokuwa kwa kupitia njia halali.

Seneta wa Democrat, Richard Durbin, alikuwa akizungumza kuhusu vibali vya muda wa kuishi vinavyotolewa kwa raia wanaotoka katika mataifa yaliyokumbwa na majanga, vita ama milipuko ya magonjwa.

Mtandao wa Shirika la habari la CBS la nchini humo, ulisema Trump aliwaambia wabunge kwamba Serikali badala yake inachukua wahamiaji kutoka Norway, ambayo waziri wake mkuu, Erna Solberg, alimtembelea rais huyo katikati ya wiki hii.

Seneta Lindsey Graham, ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican kutoka Jimbo la Carolina Kusini, pia alihudhuria mkutano huo lakini hakuweza kuzungumzia kuhusu matusi hayo yaliyotolewa na Rais Trump.

Miaka mitatu iliyopita gazeti la New York Times liliripoti kwamba, Trump alidai kuwa raia wa Haiti wote wana “Ukimwi” wakati wa mkutano kuhusu wahamiaji.

Mbunge wa Jimbo la Maryland kupitia chama cha Democrat, Elijah Cummings, amechapisha ujumbe katika mtandao wa Twitter akisema: “Nayashutumu matamshi hayo yasiyosameheka na yanayoshusha hadhi ya ofisi ya rais.”

Mbunge mwingine mweusi kutoka chama cha Democrat, Cedric Richmond, alisema matamshi ya Trump ni dhihirisho tosha kwamba sera yake ya kuliimarisha taifa la Marekani ni sawa na kulifanya taifa hilo kuwa la watu weupe pekee.

Aidha, matamshi hayo yamedaiwa kumchefua Mbunge wa Jimbo la Utah kupitia chama cha Republican, Mia Love, amesema kauli ya Rais Trump si yakiungwana wala ubinadamu, pia si kisomi kwani inachafua taswira ya nchi hiyo.

Love alimtaka Rais Trump kuomba radhi wananchi wa Marekani haraka iwezekanavyo pamoja na nchi zilizotukanwa. Mia Love ni mbunge wa pekee mwenye asili ya Haiti nchini Marekani.

Muungano unaopigania haki za watu weusi, NAACP umemshutumu rais Trump kwa kuzidi kuegemea katika ubaguzi wa rangi. Lakini Ikulu ya Whitehouse imepuuza shutuma hizo zinazomkabili rais.

Ofisa mmoja wa Trump, alinukuliwa na Kituo cha habari cha CNN akisema: “Ijapokuwa hili litawakasirisha watu wa Washington, wafanyakazi wanadhani kwamba matamshi hayo yanatokana na mizizi yake, sawa na matamshi yake dhidi ya wachezaji wa NFL waliopiga goti wakati wa kuimbwa kwa wimbo wa taifa.”

Msemaji wa ubalozi wa El Salvador mjini Washington, amekataa kuzungumzia kuhusu matamshi hayo.

Mhadhiri wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alitoa maoni yake kutokana na kauli hiyo kuwa pamoja na kwamba Trump kama kiongozi wa nchi hiyo ana haki ya kusema anachotaka, lakini anapaswa kuwa na mtazamo chanya.

“Dunia hivi sasa ni kijiji, utandawazi umetufanya tuwe sawa, tuingiliane.  Inawezekana ndio kwa hali zetu Waafrika na kuonekana tuko nyuma lakini anatakiwa kuwa na mtazamo chanya kwani Marekani imekuwa kimbilio la watu wengi,” alisema Dk. Bana.

Dk. Bana alisema kila nchi ina taratibu zake za kuruhusu wageni na Marekani ni kimbilio la wengi hivyo ni kauli ambayo haipendezi.

“Ni kauli ambayo haitupendezi Waafrika ambao bado tunatafuta fursa huko Marekani, lakini ambacho angesisitiza ni utaratibu ufuatwe, sheria zirekebishwe ili zifuatwe lakini si kutubeza kiasi hicho,” alisema Dk. Bana.

Alisema anadhani watunga sheria wa nchi hiyo wanapaswa kuliona hilo na kutunga sheria zisizobagua au kuonesha Trump ana chuki ya pekee na watu wenye ngozi nyeusi.

Trump akanusha

Jana, Rais Trump, alikanusha suala hilo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

“Maneno niliyoyatumia katika kikao changu na wabunge kuhusu masuala ya uhamiaji (DACA) yalikuwa makali, lakini sikutumia lugha ya aina hiyo dhidi ya nchi yoyote. Kilichochangia maneno makali ni kutokana na mpango wenyewe uliowasilishwa, unairudisha nyuma DACA.”

Katika Twiti nyingine, Trump aliandika: “Sikusema chochote cha kuwadhalilisha Wahaiti au Haiti, ni nchi masikini yenye matatizo. Sikusema wafukuzwe. Hiyo habari imetungwa na Democrat. Nina uhusiano mzuri na wananchi wa Haiti. Pengine tutashuhudia mkutano kati yetu huko mbele, bahati mbaya sina imani.”

Hata hivyo, Ikulu ya White House haikuwa tayari kuzungumzia maneno hayo yaliyoandikwa na Rais Trump kupitia mtandao wa kijamii.

Serikali ya Rais Trump ilitangaza mwaka jana kuwa itafuta vibali vya muda vya kuishi nchini Marekani ambavyo vilitolewa kwa watu 60,000 kutoka Haiti kutokana na tetemeko la ardhi la mwaka 2010 kuharibu jamii ya nchi hiyo. Pia ilisema watu waliopewa vibali hivyo waliruhusiwa kufanya kazi.

KUJENGA UKUTA

Seneta Dick Durbin wa Jimbo la Illinois kupitia chama cha Democrat, amesema sehemu ya mpango wa uhamiaji unaopigiwa upatu ni kama kamari ambayo inafaidisha zaidi watu kutoka Afrika na baadhi ya mataifa unapaswa kusitishwa ingawa wataruhusiwa kuomba tena vibali vya kuishi.

Durbin amesema watu watakaoruhusiwa kuishi Marekani ni wale waliokumbwa na majanga na kukosa makazi hususani kutoka El Salvador, Guatemala na Haiti.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo kati ya Seneta Durbin na Seneta Lindsay Graham wa chama cha Republican, wamemweleza Trump kuwa unajumuisha kwenye mpango wa maombi ya fedha dola bilioni 1.6 za awamu ya kwanza ya ujenzi wa ukuta mpakani na misaada kwa wanafamilia walioathirika.

Serikali ya Trump imeomba kiasi cha dola bilioni 18 ili kujenga ukuta mipakani wenye urefu wa kilomita 119 ambao utajengwa kwa kipindi cha miaka 10. Wabunge wa Democrats wamesema wanakubali mpango wa kulinda mipaka, wa kuwarejesha kwao wahamiaji 800,000 lakini si ujenzi wa ukuta. Hata hivyo, bado hakujapatikana mwafaka.

Botswana yamwita balozi wa Marekani kufafanua

Wakati huo huo, Serikali ya Botswana kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa taarifa ya kulaani matamshi ya Rais Donald Trump dhidi ya wahamiaji kutoka Bara la Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Serikali imeamua kumwita balozi wa Marekani nchini humo ili kutoa ufafanuzi juu ya matamshi ya Trump na kueleza nafasi ya Botswana katika kundi lililomaanishwa na rais huyo wa Marekani.

“Leo (jana) Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imemuita balozi wa Marekani hapa nchini kutoa ufafanuzi dhidi ya matamshi ya Rais Trump kuwa nchi za Afrika na nyingine ni kama uchafu, katika kikao cha Kamati ya Wabunge wanaoshughulikia masuala ya uhamiaji.

“Serikali ya Botswana pia imetaka ufafanuzi kutoka Serikali ya Marekani kupitia Balozi huyo na kuthibitisha kama nchi yetu ni miongoni mwa uchafu unaotajwa.

“Botswana inaziomba nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na nchi zinazoendelea kote duniani kulaani matamshi ya Rais Trump.”

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles