24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YAWAONYA WANAOKWEPA KODI MAJENGO

NA CHRISTINA GAULUHANGA-

DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewataka wananchi kuhakikisha wanalipa kodi ya majengo kwa wakati ili kuepuka adhabu ifikapo Juni, mwaka huu.

Pia wameitaka jamii kushirikiana na TRA kuwafichua wananchi wanaokwepa kodi kwa makusudi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Waandishu wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa Kodi kwa Umma wa TRA, Richard Kayombo, alisema tangu Julai mosi 2016 wamepewa mamlaka ya kukusanya kodi kwa mujibu wa ainisho la Sheria ya mabadiliko ya Fedha ya mwaka 2016.

Alisema wamiliki wa majengo watatambuliwa kwa namba ya mlipa kodi, hivyo jamii ione umuhimu wa kuwafichua wakwepa kodi waliopo katika maeneo yao.

"Serikali za mitaa zimepewa jukumu la kuchagua wathamini wa kodi za majengo kwa kuandaa orodha itakayoonesha uthamini pamoja na makadirio ya kodi ya majengo," alisema Kayombo.

Alisema hadi sasa wamefanya tathmini ya thamani ya baadhi ya nyumba na kupanga viwango vinavyotakiwa kwa kila jengo ambalo limekamilika na watu wanaishi na kufanya biashara.

Alisema hata hivyo, ni baadhi tu ya maeneo ambayo TRA wamepewa jukumu, ikiwamo majiji ya Mwanza, Tanga, Arusha na Dar es Salaam.

Pia kwa manispaa ni Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo, Kigamboni, Morogoro, Iringa, Dodoma, Songea na maeneo mengine.

Kwa upande wa miji ni Bariadi, Geita, Kibaha, Njombe, Korogwe, Mpanda na Babati.

"Malipo ya kodi za majengo yapo kwenye mfumo na hayana kiwango sawa, yanaendana kulingana na sheria ndogondogo," alisema Kayombo.

Alisema hata hivyo, Serikali imeagiza gharama za kodi hizo zisiwe kubwa ambazo zinaweza kuwaumiza wananchi.

Pia alisema yapo baadhi ya majengo ambayo yamesamehewa, ikiwamo nyumba ya rais, majengo ya umma, nyumba ya mlemavu na mtu aliyefikisha miaka 60, maktaba za umma, majengo ya makumbusho, makaburi na nyinginezo.

Aliwataka wananchi kuona umuhimu wa kulipa kodi ili kufanya maisha yawe bora, ikiwa ni pamoja na kuwafichua wasiopenda kulipa kodi.

Kayombo alitaja viwango kwa maeneo yasiyopimwa kuwa ni kuanzia Sh 3,000, 5,000 hadi 25,000.

Naye, Mwenyekiti wa DCPC, Jane Mihanji, aliwashauri waandishi wa habari nchini kutumia kalamu zao kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

Alisema ni vyema kalamu zitumike kuijenga nchi kwa kulipa kodi ambayo itasaidia kuondoa changamoto zilizopo ndani ya jamii, ikiwamo huduma za maji, barabara, umeme, afya na nyinginezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles