28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YATUNISHIA MSULI VITUO VYA MAFUTA

NA AZIZA MASOUD -DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wamiliki wa vituo vya mafuta kutekeleza agizo la kununua na kufunga mashine za kielektroniki za risiti (EFP’s) na si kutafuta visingizio vya bei.

Kauli hiyo imetolewa wakati TRA ikiwa imevifungia vituo vya mafuta ambavyo havina mashine hizo, huku baadhi ya wamiliki wakilalamikia kuuzwa kwa bei ya juu kati ya Dola za Marekani 2,500 na 3,000.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, alisema vituo ambavyo watavifungulia ni vile ambavyo vitafunga mashine hizo na si vinginevyo.

Kayombo alisema wafanyabiashara wanapaswa kutekeleza agizo la kununua mashine hizo  bila kutafuta visingizio kwa kuwa walishafanya mazungumzo na TRA  na kutoa changamoto  zao ambazo zimekwishafanyiwa kazi.

“Wafanyabiashara  waache kutafuta sababu, mwaka jana tulikutana nao na walituambia changamoto zao na tulishazitatua, walikuwa na muda mzuri wa kujiandaa kufunga mashine hizi,” alisema Kayombo.

Alisema suala la bei nalo lilishazungumziwa na kufanyiwa kazi na sasa hakuna mashine ambayo inauzwa kwa bei iliyotajwa awali.

Ingawa Kayombo alikataa kutaja bei ya sasa, lakini alisisitiza kuwa hiyo haiwezi kuwa sababu ya wao kushindwa kufunga mashine hizo.

Alisema mbali na changamoto ya bei, TRA pia ilibadilisha mfumo wa matumizi kutoka mashine moja kutumia pampu moja  ya mafuta hadi kufikia nne.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya upatikanaji wa mashine hizo, Kayombo alisema  kwa sasa mamlaka hiyo imetoa zabuni kwa wasambazaji watano ambao wanapatikana nchi nzima.

“Wasambazaji hawa wapo nchi nzima, lakini kwa muda tulioweka pia endapo kutakuwa na mfanyabiashara ambaye alishindwa kupata mashine, alikuwa na uwezo wa kufanya mawasiliano na ofisi za TRA, tungeweza kumsaidia,” alisema Kayombo.

Mbali na hilo, Kayombo pia alitolea ufafanuzi vituo vilivyofungwa kwa kutofunga mashine hizo kulikofanywa Jumatano ya wiki hii, akisema kwa sasa vimeshaanza kufunguliwa.

“Tumeshaanza kufungua vituo vya mafuta ambavyo vimeanza kutekeleza  agizo la kufunga mashine na wengine wanaendelea na taratibu  watafunguliwa mara tu baada ya kukamlisha,” alisema Kayombo.

Alisema vituo vya mafuta 71 vilifungwa katika wilaya tatu za Mkoa wa Dar es Salaam na kati ya hivyo, 52 vimeshaanza kufunguliwa baada ya kuonyesha ushirikiano  wa kuanza kufunga mashine hizo.

Kwa mujibu wa Kayombo, katika Manispaa ya Ilala, kati ya vituo 31 vilivyofungwa, 20 vimefunguliwa wakati  Manispaa ya Kinondoni, kati ya vituo 28 vilivyofungwa 23 vimefunguliwa na Wilaya ya Temeke vituo tisa vimefunguliwa kati ya 12.

Uamuzi wa TRA kufunga vituo vya mafuta ulisababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa nishati hiyo, hasa kwa siku ya juzi na hivyo kushuhudiwa foleni kubwa katika vituo vichache vilivyokuwa wazi.

Pengine kutokana na hali hiyo, siku ya jana kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam hakukuwa na foleni tofauti na Jumamosi nyingine zote.

Mapema mwaka jana TRA ilikutana na Chama cha Wauzaji Mafuta Rejareja (TAPSOA) na kukubaliana kuwa  ufungaji wa mashine  ufanywe kwa mchakato badala ya kuisha Machi Mosi.

Kikao cha TRA na mawakala hao kilifanyika baada ya kuwapo kwa tangazo lililowataka wenye vituo vya mafuta  nchini kuweka mashine hizo. Mwisho wa kufanya hivyo ilikuwa Machi Mosi, mwaka jana na ilidaiwa kitendo hicho kingesababisha mgomo kwa wenye vituo hivyo.

Katika kikao hicho, Katibu wa TAPSOA Taifa, Tino Mmasi, alizitaja baadhi ya changamoto wanazozilalamikia kuwa ni EFDs kuuzwa Dola za Marekani 2,500 hadi 3,000.

Pia alitaja changamoto ya kiteknolojia kuwa inaweza kuwakwamisha kwa kuwa mashine hizo zinapoharibika, huchukua muda mrefu mfanyabiashara kupata msaada kutoka kwa wataalamu.

Kutokana na malalamiko hayo, TRA na TAPSOA  walikubaliana kuwa wakati changamoto hizo zikiendelea kufanyiwa kazi, EFDs nazo zifungwe kwa awamu tatu na kusiwe na muda maalumu wa kukamilisha ili kuwapa nafasi wenye vituo vya mafuta kujiandaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles