23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

TRA: Biashara ya magendo ina madhara katika jamii

BENEDICT LIWENGA-SONGWE

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)imesema biashara ya magendo ina madhara katika jamii na kwamba inaweza kuharibu ulinzi na usalama wa raia uliopo.

Hayo yamezungumzwa jana na Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi wa TRA makao makuu Julius Mjenga wakati akitoa elimu kwa Wafanyabiashara wa Mji wa Tunduma mkoani Songwe kuhusu madhara ya kufanya biashara za magendo mipakani.

TRA inafanya kampeni ya Elimu ya Kodi mkoa kwa mkoa na hivi sasa kampeni hiyo inaendelea katika mikoa ya Songwe na Mbeya.

Mjenga alisema biashara ya magendo ikiachwa iendelee ina madhara ya kiafya kutokana na kuwa wafanyabiashara hao wanaweza kuingiza bidhaa zilizopitiliza muda wake ambazo zinaweza kuwasababishia walaji magonjwa mbalimbali ikiwemo kansa.

Alisema pia biashara ya magendo inaweza kuchangia kuharibu ulizi na usalama kutokana na baadhi yao wanaweza kuingiza nchini silaha kama mabomu na bunduki nk.

“Serikali imeamua kuchukua hatua na ndio maana tumekuja kuzungumza na wadau wa serikali mlioko maeneo ya mpakani kwamba msifanye biashara za magendo na kwamba mizigo mnayochukua mnatakiwa kuipitisha kwenye maeneo ya forodha yanayokubalika ambako mtalipa kodi lakini pia wao watajua kama bidhaa imekubaliwa kuingia nchini au imepigwa marufuku au inatakiwa kufuata utaratibu gani kwa mujibu wa sheria,” alisema Mjenga.

Naye Valentina Baltazar Afisa Msaidizi Msimamisi wa Kodi wa TRA, alisema kuwa bidhaa zinazotoka katika nchi mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwemo Zambia zinatakiwa kulipia VAT pekee na kwamba ushuru wa forodha haulipiwi.

Alisema kama mzigo utakuwa mkubwa lazima mfanyabiashara huyo apitie ofisi za TRA ili kuonyesha cheti cha uasili kinachopatikana hapo hapo mpakani ambacho kinathibitisha kuwa mzigo huo umetoka katika nchi mwanachama wa SADC na sio nje ya nchi hizo.

“Kuhusu uingizaji wa sukari nchini, kuna utaratibu na kibali maalumu cha kuingiza bidhaa hiyo  na kwamba wabunge walikubaliana kuwa iwapo kutakuwa na upungufu wa sukari watakaoruhusiwa kuiingiza ni wale wenye viwanda kwa wale watakaoingiza bila kibali hicho bidhaa hiyo itataifishwa huku wale watakaokuwa na kibali watatakiwa kupita katika ofisi ya forodha ili wakadiliwe kodi kwa mujibu wa sheria,” alisema Valentina.

Robert Sipungwe ambaye ni mfanyabiashara wa chuma chakavu Tunduma alisema kuwa elimu ya kodi inayotolewa na TRA ina umuhimu na kwamba ulipaji wa kodi ni muhimu kutokana na kuwa kodi hiyo hivi sasa inatumika vizuri.

“Pamoja na elimu hiyo kodi, sisi wafanyabiashara wa chuma chakavu tunanunua vyuma chakavu, leseni tunazo na mapato tunalipa lakini kero tunayokutana nayo ni wakati wa kivisafirisha tunakutana tena na kikosikazi cha TRA ambacho kinatufata wakati tumeshafuata taratibu zote, tunaomba mamlaka iliangalie hili hasa hapa Tunduma”, alisema Sipungwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles