TPSF YALAUMIWA KUDHARAU SEKTA UVUVI

0
910

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


SEKTA ya uvuvi ni moja ya nguzo kubwa za uchumi wa nchi ambayo imesahauliwa na wadau wake ikiwamo uwekezaji mkubwa.

Iwapo jamii ikiwekeza vya kutosha katika sekta hii inaweza kuzalisha idadi kubwa ya ajira, fedha za kigeni na kuongeza pato la taifa kama ilivyotokea mwaka jana ambapo mapato yake nje yalipita mazao makubwa matano ya kilimo.

Sekta hii inatoa ajira kwa watanzania zaidi ya milioni nne kwa wavuvi na watu wanaojihusisha na masuala ya uvuvi huku wavuvi pekee wakiwa ni zaidi ya 400,000.

Kwa mujibu wa Takwimu za taifa za uchumi za mwaka 2009(National Economic Survey, 2009). zinaonesha kuwa sekta hiyo iliweza kuchangia asilimia 1.3 katika pato la taifa.

Wastani wa Matumizi ya samaki nchini ni kilo nane kwa mtu mmoja kwa mwaka huku ikifanya asilimia 30 ya protini hapa nchini hutokana katika ulaji wa samaki.

Pamoja na umuhimu wake bado inakabiliwa na changamoto ya wadau kushindwa kuwekeza vya kutosha katika sekta hiyo ili iwe ya kuridhisha  kwani kwa kiasi kikubwa inategemea uwekezaji wa nje.

Mbarouk Ali Mbarouk ni mvuvi anayefanya shughuli zake Zanzibar anaelezea kwa undani changamoto hiyo kuwa ni kubwa.

Anasema tangu ameanza kuvua samaki amekuwa akitumia zana duni ambazo hazimwezeshi kupata samaki wengi na wakubwa.

Mbarouk anasema wamekuwa wakitumia zana zikiwamo nyavu na boti ambazo zimetengenezwa kienyeji jambo ambalo linawafanya kushindwa kwenda katika maji marefu(Deep sea) kuvua ambako kumesheheni samaki wa haja wa minofu wakiwamo johari.

“Kama unavyoona mitumbwi tunayotumia kuvua samaki ni duni ambayo hatuwezi kwenda nayo katika maji marefu kupata samaki wakubwa,” anasema Mbarouk.

Anasema wamekuwa wakivua samaki katika maeneo yaliyokaribu na ufukwe kwa kuhofia kusombwa na maji kutokana na mitumbwi kuwa duni na kinachohitajika ni meli za uvuvi.

Anasema iwapo wangeweza kupata fedha za kununua meli za uvuvi wangeweza kushindana na wavuvi wakubwa wanaotoka katika mataifa ya mbali kuvua katika maji marefu nchini.

Anasema jamii ya uvuvi imekuwa haiaminiwi na taasisi za kifedha kiasi ambacho hawawezi kupatiwa mikopo kirahisi kwa kuwa ni masikini.

“Changamoto kubwa hapa ni upatikanaji wa fedha za kuwekeza katika sekta ya uvuvi kwa kuwa hatuna uwezo wa kupata mikopo ya muda mrefu kwa kuwa hatuna dhamana ya kuweka katika taasisi za kifedha,” anasema Mbarouk.

Anasema hata kwa upande wa matajiri na wawekezaji wakubwa nchini hawajafikiria kuwekeza katika sekta hiyo amabayo ina hazina kubwa na rahisi kuivuna.

Kauli hiyo ya Mbarouk inaungwa mkono na mtaalamu wa masuala ya Uvuvi kutoka katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), DK. Bennaiah Benno ambaye  anasema hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta hii na hivyo kusababisha sekta kushindwa kuchangia kwa kiwango kikubwa katika pato la taifa.

“Idadi kubwa ya wavuvi ni masikini ambao hutumia  boti zilizotengenezwa kwa teknolojia duni katika kuvua samaki.

“Hii haiwawezeshi kufika katika kina kirefu cha maji ambako ndiko waliko samaki wakubwa na kuishia pembezoni mwa bahari na maziwa,” anasema Dk. Benno.

Anasema uvuvi huu unaofanywa na jamii za uvuvi nchini husababisha kuvua sehemu moja na kujikuta wakikosa mazao ya samaki kutokana na kuwamaliza kwa kuharibu mazalio (Over fishing).

Dk. Benno anasema sekta hii inahitaji uwekezaji mkubwa ili kuwakwamua kiuchumi wavuvi na kuongeza pato la taifa.

“Wavuvi wanahitaji kupata vifaa bora vya uvuvi ikiwamo majokofu ya kuhifadhia samaki  kwenye boti na boti  kubwa zenye uwezo wa kufika katika maji marefu,” anasema Benno.

Anasema kutokana na kukosekana uwekezaji katika sekta hii, wavuvi wengi hushindwa kuvua kibiashara na hivyo jamii zao kuwa ni masikini .

Anaongeza pia uhifadhi na usambazaji wa samaki wabichi wenye bei nzuri unawawia ugumu wavuvi kutokana na ukosefu wa majokofu na magari ya kusafirishia samaki.

“Kunahitajika kuboresha miundombinu ya masoko na sehemu za kuhifadhia samaki kama kuwa na maabara nzuri na maeneo ya kuhifadhia samaki kabla ya kuwauza,” anasema Dk. Benno.

Dk Benno anasema ili kuimarisha sekta ya masoko ya samaki uwekezaji katika teknolojia mpya zikiwamo za vifungashio na masoko unahitajika ilikupata masoko ya nje.

Anasema pamoja na uhitaji wa uwekezaji huo, changamoto kubwa ni ukosefu wa rasilimali fedha.

“Jamii za wavuvi hushindwa kuaminika na taasisi za kifedha kutokana na kukosa dhamana kwani asilimia kubwa wao ni masikini,” anasema Benno.

Hata hivyo anasema kukosekana kwa elimu ya fedha miongoni mwa wavuvi kusababisha kushindwa kujua wapi watapata rasilimali fedha kwa ajili ya kuwekeza kwani mabenki yanayokopesha yapo.

NMB yakopesha wavuvi

Upande wake Mkuu wa Kitengo cha wateja wadogo na wa kati wa benki ya NMB, Abdulmajid Nsekela anasema benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wateja wengi wadogo na kati wakiwamo wavuvi.

Anasema wavuvi wamekuwa wakipatiwa mikopo kuanzia Sh 500,000 hadi milioni 50 kulingana na mahitaji yao.
“Tuna wateja wengi ambao ni wavuvi wanaochukua mikopo midogo na ya kati katika maeneo mbalimbali ya nchi,” anasema Nsekela.

Anaongeza kuwa wavuvi wanapendelea kuchukua mikopo kutoka katika benki hiyo kwa kuwa ni rahisi kuomba na hutumia siku nne tu kupata.

“Katika benki ya NMB tunawaamini wateja wadogo na kati kwani hawasumbui kurejesha mikopo yao hivyo wasiogope kuja kuomba,” anasema Nsekela.

TPSF yakosa ushirikiano

Kwa zaidi ya miezi miwili tuliomba kauli toka Wakfu ya Wafanyabiashara Binafsi (TPSF) kuhusu maelezo ya uwekezaji wamekataa kujibu pamoja na kuwafuatilia sana;  ikiwa ni dalili kuwa hawana jipya na hawatilii maanani sekta hiyo. Ni kweli usilolijua huwezi kulithamini na hivyo wanaukosa utajiri.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here