27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TPA YALIPA FIDIA BILIONI 5.6/- BANDARI KAVU MISUNGWI

Na JUDITH NYANGE

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imezilipa fidia Sh bilioni 5.6  kaya 144  zilizopisha eneo  la ukubwa wa  ekari 1,178 kwa ajili ya  bandari kavu ya mizigo inayotarajia kujengwa katika vitongoji  vya Nyakilingi na Budo katika Kijiji na Kata ya Fela wilayani Misungwi.

Meneja  wa Bandari ya Mwanza, Daniel Sira, alikuwa akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela aliyetembelea eneo hilo na kuwakabidhi hati  baadhi ya wananchi juzi.

Alisema  kaya 111  zinatoka katika Kitongoji cha Nyakilingi na 33 Budo.

Alisema baada ya kuzungumza na halmashauri, viongozi wa kijiji na  wananchi wote  wa maeneo hayo kuhusu mradi huo walionekana kuupokea kwa shangwe  kutokana na faida zitakazopatikana wakati wa ujenzi na hata baada ya kukamilika   bandari hiyo.

“Katika eneo hilo lililochukuliwa tulikuta  nyumba 372 zilizojengwa kwa matofali ya tope na kuezekwa   nyasi, 22 za matofali ya saruji na mchanga na kuezekwa kwa bati.

“Nyumba  nane za matofali ya kuchoma na zimeezekwa kwa bati, tulikuta misingi sita ya nyumba iliyojengwa kwa  mawe, mazao, miti ya asili   na ile ya kupandwa.

“Watu  668 wanaotokana na kaya 144  watapata malipo   kutokana na mtu moja kumiliki zaidi ya eneo moja,  tayari  wananchi 651 wameshakabidhiwa hundi zao za malipo ya fidia  na wamebaki 17 tu.

“Hao hawakujitokeza lakini malipo yao yapo na tumetoa maelekezo kwa mwenyekiti wa kijiji watakapojitokeza wafike katika ofisi zetu kulipwa,” alisema Sira.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema atamshauri waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano,  Profesa Makame Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA,   Deusdedit Kakoko,  kuliwekea  uzio eneo hilo   litambulike na  mipaka yake kuepusha  wananchi kulivamia na kuanzisha  upya mgogoro wa kudai upya fidia.

“Kuna nguzo nyingi za mipaka kwenye viwanja zimeanza kuibuka kama mchwa, nimepita hapa mwezi mmoja uliopita nilikuwa sioni nguzo nyingi kama nilizoziona leo.

“Maana yake ni watu wameshaona bandari inakuja kila mtu anataka kuhamia huku ni lazima  uwepo utaratibu mzuri,” alisema Mongela.

Mongela  alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo  na mkurugenzi kuweka mpangilio  wa makazi katika maeneo ya jirani na bandari hiyo  kwa kutenga maeneo ya barabara, shule, vituo vya afya  na huduma nyingine za   jaamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles