30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TMA sasa mnawatendea haki Watanzania

Mwandishi Wetu

MOJA ya mambo ya kujivunia katika siku za hivi karibuni, ni kuwapo taarifa za uhakika kuhusu mwenendo wa hali ya hewa nchini.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  (TMA), imeonyesha mabadiliko makubwa katika taarifa zake za utabiri ambazo hazikuwapo miaka mingi nyuma.

Mamlaka hii sasa inaanza kuonekana kuwa na uhalisia kila inapotoa taarifa zake za utabiri wa hali ya hewa kwa wananchi, iwe ni ujio wa mvua, joto kali au janga lolote.

Hatua hii ni kubwa ambayo inapaswa kuungwa mkono na kila mzalendo wa nchi hii.

Tunasisitiza hili kwa sababu mamlaka hii kwa miaka ya nyuma ilizoelekea kwa misemo yake ya kusikia, bahari itakuwa na mawimbi madogo madogo, ngurumo na radi zitakuwapo pia.

Sasa maneno haya yalionekana wazi yanakera Watanzania ambao hawakuwa na uhakika wa nini kitatokea.

Hatuisemi vibaya mamlaka hii, bali tumeguswa na mabadiliko makubwa ambayo yanaonekana katika taarifa zake za utabiri.

Tunapongeza mamlaka kwa kutoa taarifa sahihi ambazo sasa, hata wakazi wa mabondeni na wasiokuwa wa mabondeni, wameanza kuzifanyia kazi kwa kuchukua tahadhari zinapotoka.

Kwa mfano, juzi mamlaka imetoa taarifa ya kuwapo mvua katika mikoa mitano. Siku iliyofuata, wakazi wa Dar es Salaam ni mashahidi, kulionekana mabadiliko ya hali ya hewa kuanzia alfajiri na mvua ilianza kunyesha.

Lakini pia wiki iliyopita mamlaka hii iliwapa taarifa Watanzania kwamba kutakuwa na joto kali mikoa ya pembezoni mwa Bahari ya Hindi, ikiwamo Dar es Salaam ambayo  inaendelea kupata joto kali katika kipindi cha Januari na Februari.

Mkurugenzi wa Utabiri wa mamlaka hii, Samweli Mbuya anasema hali hiyo inatokana na kuisha kwa mvua za vuli.

Anasema joto litaendelea kuwa juu kwa kipindi hiki ambapo dunia itakuwa na jua la utosi kwa sababu linakuwa karibu zaidi na dunia.

Mbuya anasema viwango vya joto vitaendelea kutofautiana kulingana na hali ya hewa itakavyokuwa kulingana na mwenendo wa siku husika.

Anasema hali hiyo itakuwa katika maeneo ya ukanda wa mashariki na pwani ambako mvua za vuli zimekwisha.

Mbuya anasema wastani wa viwango vya juu vya joto la dunia utafikia asilimia moja na nusu hadi mbili.

Anasema joto litaanza kupungua Machi, baada ya mvua kuanza kunyesha  mikoa husika.

Tunaamini kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi  na timu yake inafaa kupongezwa kutokana na mabadiliko haya.

Yawezekana kabisa Dk. Kijazi na wasaidizi wake, wamefikia mafanikio makubwa haya baada ya kuwezeshwa na Serikali kwa kupata vifaa vya kisasa vya kupimia  hali ya hewa tofauti na zamani.

Lakini pia wafanyakazi wake kuwajibika vizuri kama timu moja, kumesaidia kuwapo na mabadiliko haya makubwa ambayo hakika kila mtu anapaswa kuyatumia kwa manufaa yake.

Sisi MTANZANIA, kutokana na kazi nzuri hii ya TMA, tunawasihi Watanzania kujenga utamaduni wa kufuatilia utabiri wa hali ya hewa kila siku ili waweze  kuepuka maafa ambayo yanaweza kutokea, ambayo wakati mwingine yanaepukika.

Pia tunawasihi wananchi wanaoishi mabondeni kuondoka maeneo hayo kwa sababu dalili zinaonyesha kuanzia Machi, kutakuwa na mvua kubwa za masika.

Tunamalizia kwa kusema TMA endeleeni kuchapa kazi kwani sasa mmezaliwa upya. Utabiri wenu unaendana na uhalisia wa hali ya hewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles