30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TIC YATAKA MAENEO ZAIDI YA UWEKEZAJI MIKOANI

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe, amemtaka Kamishna wa Ardhi nchini kuhakikisha anapeleka hati za ardhi katika kituo hicho ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo kwa wawekezaji wanapohitaji.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, katika kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali kujadili namna ya kufanikisha malengo ya uchumi wa kati ya miaka mitano na azma ya Rais ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

“Tutatumia mfumo wa kutoa haki ya kutumia ardhi wakati hati tukiwa nayo sisi, lengo hapa ni kuhakikisha wanapata maeneo ya kuwekeza haraka kuliko kwenda yeye mwenyewe kwa wananchi kununua maeneo ambapo anaweza kujikuta anatumia miaka miwili kupata ardhi,” alisema Mwenda.

Aliwataka wakuu wa mikoa yote nchini kuendelea kutenga maeneo ya shughuli mbalimbali za uwekezaji, ikiwamo kilimo, ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo yanapohitajika.

Alisema wanahakikisha TIC inakuwa taasisi ya utafiti yenye uwezo wa kufahamu aina ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini sambamba na kumwona mwekezaji kama mteja ambaye mfanyabiashara hapaswi kumpoteza.

“Lazima tufahamu, wasiwe wenye lengo la udanganyifu, kiasi cha ajira alichosema atazalisha ni kweli anazalisha na aina ya kazi wanazoomba kufanya ndizo wanazofanya.

“Tutafanikisha haya pia kwa kupunguza mlolongo wa nyaraka za maombi ya uwekezaji kwa kutumia mfumo wa kituo cha pamoja ambapo atakuwa na uwezo wa kupata huduma zote hapa, ikiwamo vibali vya kuishi nchini,” alisema Mwenda.

Alisema kuanzishwa kwa shughuli za viwanda, hususan vya uchakataji wa mazao ya kilimo kutahakikisha upatikanaji wa masoko kwa wakulima na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

“Kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji kutaongeza makusanyo ya kodi kutoka asilimia 15 za sasa walau kufikia 25 ya kiwango cha uzalishaji, tulenge kuzalisha bidhaa ambazo tumekuwa tukiagiza kutoka nje na kuongeza usafirishaji wa bidhaa zetu nje ya nchi,” alisema Mwenda.

Alisema kuongezeka kwa shughuli za viwanda kutakuza ujasiriamali kwa wananchi kufanya biashara ya kukusanya mazao kama vile ngozi na kuzipeleka viwandani, huku na wao pia wakitoa ajira watu wanakofanya kazi ya kukusanya ngozi hizo.

Alisema TIC ina jukumu la kubeba mzigo wa kuhakikisha viwanda vingi vinaanzishwa na ikiwa watashindwa kufanya hivyo, wawekezaji watakwenda katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na kuitumia Tanzania kama soko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles