33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TIC KUTENGA MAENEO UJENZI WA VIWANDA

Na MANENO SELANYIKA-DAR ES SALAAM


KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesema kipo katika mchakato wa kutenga maeneo maalumu hapa nchini kwa ajili ya kujenga viwanda ili kuunga mkono sera ya Serikali ya kuimarisha na kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Kauli hiyo imebainishwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe, kwenye kikao kilichoshirikisha wakuu na wawakilishi wa taasisi za mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.

Mkurugenzi huyo alisema lengo la kituo hicho ni kuhakikisha wawekezaji wanawekeza bila kuwa na vikwazo ili kuongeza uchumi na Pato la Taifa.

“Tumekutana hapa ili kujadili mkakati wa kujenga maeneo ya viwanda ‘Industrial Parks’ baada ya tathmini iliyofanywa na kituo hiki na kubaini kuwepo kwa changamoto zinazokwamisha uwekezaji nchini, ikiwemo ukosefu wa maeneo tengefu ya kutosha ya uwekezaji sambamba na uhitaji wa wawekezaji kwenye maeneo hayo yenye miundombinu wezeshi kwa ajili ya uwekezaji,” alisema.

Alisema hali hiyo inakwamisha juhudi za kuvutia uwekezaji nchini kutokana na ukweli kwamba wawekezaji wamekuwa wakikaribishwa nchini kuwekeza na wengi wao wanapofika wanakuta hakuna huduma wezeshi ikiwamo upatikanaji wa ardhi iliyo tayari kwa uwekezaji sambamba na miundombinu kama ilivyo kwa nchi nyingine.

Mwambe alisema hali hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa wawekezaji wenye nia madhubuti ya kuanzisha miradi nchini ili kuunga mkono dhana ya Rais Magufuli ya Tanzania ya kuelekea uchumi wa viwanda kulingana na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17–2020/21.

Akichangia katika kikao, Mtaalamu wa Uchumi kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSPF, Hamidu Ngororo, alisema mpango ni mzuri na katika utekelezaji wake, inapaswa kushirikisha sekta binafsi ambazo zina nafasi kubwa ya kuisaidia Serikali katika kuimarisha uwekezaji nchini.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, Xavier Lukuvi, alisema katika kuandaa maeneo ya uwekezaji, suala la kuwekwa miundombinu ni muhimu kwa kuwa ni kiungo kikubwa katika maeneo hayo.

Akichangia hoja hiyo, Meneja wa Mipango na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF, Benedict Mahona, alisema katika kutekeleza mpango huu ni vema tukaanza na maeneo machache ‘pilot study’ ili kuona matokeo badala ya kueneza maeneo yote kabla ya kuona ufanisi wake kulingana na rasilimali zilizopo.

Mbali na kituo hicho, taasisi nyingine zilizoshiriki kwenye kikao hicho ni pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii NSSF, Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Mfuko wa Pensheni wa PPF na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles