29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

TFF MSAIDIENI NKOMA KUTIMIZA MIPANGO YAKE

Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

MSEMO wa mipango si matumizi, umekuwa ukijidhihirisha mara nyingi kwa watu wanaoizunguka jamii ya Kitanzania, hili sasa linaweza kumtokea kocha Sebastian Nkoma.

Kocha huyo wa timu ya Taifa ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 ‘Tanzanite Queens’, ameweka wazi mipango na mikakati yake ya kuhakikisha anaandaa wachezaji wazuri watakaoweza kuunda kikosi cha Twiga Stars hapo baadaye.

Nkoma anaweza kuwa na mipango vizuri yenye lengo la kuhakikisha Tanzania inapiga hatua katika soka upande wa wanawake, swali linakuja je, atafanikiwa?

Hivi sasa kocha huyo ameeleza changamoto anazokumbana nazo kuelekea mchezo kati ya Tanzanite na Nigeria, mechi hiyo muhimu kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kufuzu fainali za dunia kwa wanawake wa umri huo chini ya miaka 20.

Changamoto kubwa ni kukosa mechi za kirafiki, ambazo zingeweza kukipima kikosi chake, ukiachilia mbali zoezi gumu alilopitia kuhakikisha kikosi hicho chenye wachezaji 25 kinapatikana.

Ikiwa mwanzo wa kutimiza malengo yake umeanza kuwa mgumu huko mbele itakuwaje, Tanzania kushindwa kuwa na wachezaji wenye umri mdogo watakaoweza kulitangaza taifa katika mashindano mbalimbali upande wa soka ni zao la mfumo mbovu.

Mfumo mbovu umeanza miaka mingi iliyopita, wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiongozwa na viongozi mbalimbali, ambao wamemaliza muda wao na kukabidhi kijiti kwa wengine.

Soka la wanawake limesahaulika, hakuna anayejishughulisha kulizungumzia na hata linapopata nafasi ya kuzungumziwa basi mazungumzo hayo huwa ya muda mfupi tu.

Inashangaza kuona kikosi kikiitwa pindi tu kunapokuwepo na mashindano ya kushiriki, tofauti na ilivyo kwa timu ya wanaume ya Taifa Stars.

Nkoma anaweza kuwa na mawazo mazuri, lakini yatashindwa kutimia sababu kubwa ni mfumo uliokuwa ukitumiwa na bado unaendelea kutumika hadi sasa.

TFF chini ya uongozi mpya inatakiwa kusimama imara ili kuhakikisha kocha huyu mwenye mapenzi mema na soka la Tanzania anatimiza mipango yake, kwani kufanikiwa kwake ni faida kwa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles