23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TFF, BMT MSITUFIKISHE KWENYE MABADILIKO YA SIMBA, YANGA

Na ZAINAB IDDY

JUMATATU ya wiki iliyopita Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Revocatus Kuuli, alitangaza kuanza mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa shirikisho hilo, uliopangwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu mjini Dodoma, huku Juni 16 zoezi la uchukuaji fomu kwa watu wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali ndani ya TFF likianza.

Siku moja, baada ya kamati hiyo kutangaza  kuanza mchakato wa uchaguzi, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia kwa Kaimu katibu wake mkuu, Mohamed Kiganja alitoa tamko la kusitisha zoezi hilo kwa kile alichodai BMT hawana taarifa juu ya kuanza mchakato huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kiganja alisema, wameusimamisha uchaguzi wa TFF kwa kuwa shirikisho hilo limekiuka kanuni zinazoipa BMT, mamlaka pekee ya kusimamia chaguzi wa vyama vya michezo nchini na TFF ni mwanachama wa BMT.

Kwa mantiki hiyo uchaguzi umesimamishwa hadi pale BMT itakapokutana na Kamati ya Utendaji ya TFF Julai mosi, kujadili na kupanga taratibu za kufanikisha jambo hilo bila ya kuvunja  kanuni, sheria na taratibu za nchi zilizopo.

Pongezi kwa TFF kupitia kwa  katibu wake mkuu Mwesigwa Selestine, aliyeiomba BMT kuruhusu mchakato wa uchaguzi uendelee  lakini pia kutaka uomba kukutana haraka na baraza kabla ya muda waliopanga ili kutovuruga ratiba ya uchaguzi.

Kiroho safi inaungana na TFF kwa kuwataka wakutane haraka iwezekanavyo na BMT na kuweka sawa mkanganyiko unaodaiwa kujitokeza, ili kusiweze kuvuruga jambo hilo muhimu kwenye tasnia ya soka ya Tanzania.

Ni wazi kuwa BMT na TFF ni waelewa , hivyo kukutana kwao hakutaweza kuleta migongano na migororo mingine, itakayolazimisha kusimamishwa kwa uchaguzi kama ilivyokuwa kwenye suala la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kwenye klabu za Simba na Yanga.

Hadi leo hakuna anayefahamu ni lini mchakato wa mabadiliko kwenye klabu za Simba na Yanga utaendelea na hii ilisababishwa na mvutano, baina ya BMT na klabu hizo kongwe nchini.

Ni wazi kuwa iwapo kama yatatokea yale yaliojitokeza katika mchakato wa mabadiliko ya kimfumo ya uendeshaji wa timu za Simba na Yanga, kunaweza kuleta mvurugano mkubwa wa kikalenda na hata kusababisha mambo muhimu kutofanyika kwa wakati.

Katika kalenda ya TFF inafahamika kunamatukio makubwa kama mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza, Kombe la Shirikisho(FA), Ligi ya Vijana, Ligi ya Wanawake Taifa na hata maandalizi ya timu za taifa kwa maana ile ya Serengeti boys , Taifa Stars, Ngorongoro na Twiga Stars, ambazo zinakabiliwa na mashindano makubwa ya kimataifa huku zote zikitegemea mipango mikakati ya TFF ingawa kunakamati zake zilizoundwa.

Ni jambo jema lililofanywa na TFF kutaka kufanyika kwa uchaguzi huo, kabla ya mashindo ya ligi mbalimbali za Tanzania kuanza ili kutoa fursa kwa viongozi wapya watakaopata nafasi ya kuingia madarakani kuanza  majukumu hayo mara tu, baada ya kukabidhiwa madaraka.

Iwapo kama TFF na BMT watashindwa kukutana kwa wakati ni wazi uchaguzi utasimama, hivyo kuendelea kutoa majukumu kwa viongozia ambayo tayari wameshamaliza muda wao na hawapaswi kupewa majukumu hayo.

TFF na BMT wanauwezo mkubwa wa kukutana mapema na kuelewana ili kuharakisha uchaguzi kwa muda uliopangwa, Kiroho Safi haitegemei kukutana kwa pande hizo kunaweza kuzaa yale yaliojitokeza katika mchakato wa mabadiliko ya mifumo ya uendeshaji kwa timu za Simba na Yanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles