26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TFDA YAFUNGA KIWANDA CHA MAJI

Na MWANDISHI WETU-KAGERA

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), Ofisi ya Kanda ya Ziwa, imekifungia kwa muda kiwanda cha kutengeneza maji ya kunywa cha Kabanga Springs kilichoko Kamachumu, Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

Uamuzi wa kukifungia kiwanda hicho, umechukuliwa baada ya wakaguzi wa chakula wa TFDA Kanda ya Ziwa kubaini uapungufu makubwa ya usafi na utaalamu kinyume na kanuni za uandaaji wa chakula salama za mwaka 2006.

Akizungumza jana, Mkaguzi wa Chakula wa TFDA Kanda ya Ziwa, Nuru Mwasulama aliyataja upungufu huo kuwa ni uwapo wa vumbi katika mashine za kusindika, sakafuni na kwenye kuta za kiwanda hicho, wafanyakazi kutopimwa afya na kukosa sare, kukosekana kwa mfumo wa maji safi katika vyoo hali ambayo ilikuwa inasababisha uchafu katika eneo hilo.

Mwingine, ni uchakavu wa machujio ya maji katika sehemu ya kuchujia maji na kutofanya kazi kwa mfumo wa UV-Light hali ambayo inahatarisha usalama wa maji yanayozalishwa, uchafu uliokithiri katika maabara ya uchunguzi wa maji na kukosekana kwa taarifa zinazoonesha ufuatiliaji na upimaji wa ubora na usalama wa maji.“Kutokana na mapungufu makubwa yaliyoonekana wakati wa ukaguzi na yanayokinzana kwa kiasi kikubwa na kanuni za usindikaji salama wa chakula tumesitisha shughuli zozote za usindikaji wa maji katika kiwanda mpaka watakapo fanya marekebisho muhimu,” alisema Mwasulama.

Alisema mamlaka hiyo,itakuwa tayari kukifungua kiwanda hicho pale ambapo itajiridhisha kuwa maelekezo yote yalitolewa yamefanyiwa kazi.

Aliyataja baadhi ya maelekezo yaliyotolewa kwa wamiliki wa kiwanda  kuwa pamoja na kuwapima afya wafanyakazi, kubadirisha machujio ya maji, kutengeneza mfumo wa UV- Light unaotumika kuangamiza vijidudu hatarishi ili kuhakikisha usalama wa maji yanayozalishwa, kufanya usafi katika chumba cha maabara na kutunza kumbukumbu za maabara, kutafuta mtaalamu wa chakula mara moja kwa ajili ya kusimamia uzalishaji salama wa maji na kuwapatia wafanyakazi sare za kazi.

“Tumemuagiza  atutaarifu  kwa maandishi pale atakapo maliza utekelezaji wa maagizo yote tuliyompatia.  Tutakapo jiridhisha kuwa ametekeleza maagizo ya mamlaka tutamfungulia ili aendelee na uzalishaji,” alisema Mwasulama.

Mwisho

Mbaroni kwa kumpaka mtoto kinyesi cha mbuzi

Na JUDITH NYANGE-MWANZA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Chakechake, Sospeter Rajabu (42), kwa kosa la kumpaka kinyesi  cha mbuzi kwenye majeraha yaliyotokana kuungua   moto  mtoto wake, Neema Sospeter (10) mwanafunzi wa darasa la  kwanza na kusababisha hali yake kuwa mbaya.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi jana, ilisema mtuhumiwa  alikamatwa juzi  saa 10:30 jioni  Mtaa wa Chakechake  wilayani  Nyamagana.

Alisema Sospeter anatuhumiwa  kumpaka mavi ya mbuzi  mtoto wake kwenye majeraha ya moto aliyoungua maeneo ya mapaja ya miguu yote miwili kwa muda wa wiki mbili na kusababisha  majeruhi kuwa na hali mbaya kiafya ambapo  wananchi walitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo, askari walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi maeneo hayo na kufanikiwa kumkuta mtoto akiwa kwenye hali mbaya na  kushirikiana na wananchi kumkimbiza hospitali na  kumkamata baba wa mtoto.

“Huyu mtoto aliungua moto Agosti 4, mwaka huu saa 1:45 usiku  Mtaa wa Kitangiri wilayani Iilemela ambapo alikuwa akiishi na mama yake kwani wazazi wake walitengana kwa muda mrefu, inadaiwa alimwagikiwa na mafuta ya taa alipokuwa akiweka kwenye  kibatari na kuwasha  na njiti ya kibiriti na  moto kulilipuka kisha  kumuunguza.

“Baada ya mama yake  kukosa fedha za matibabu, aliamua kumpeleka  kwa baba yake Mtaa wa Chakechake alipokua akiishi na mke mwingine ili amsaidie mtoto apate matibabu, lakini baada ya mtoto kufikishwa kwa baba yake hakupelekwa hospitali na  badala yake alikuwa akipakwa mavi ya mbuzi na kusababisha  hali yake kuzidi kuwa mbaya,” alisema Kamanda Msangi.

Alisema polisi wapo kwenye upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa dhidi ya ukatili aliyokuwa akimtendea mwanae pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani, majeruhi amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza  Sekou Toure akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles