30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tetemeko la ardhi latikisa Mbeya

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

TETEMEKO la ardhi lililodumu kwa takribani dakika moja jana mchana lilitikisa mikoa ya nyanda za juu kusini, huku wananchi wakijikuta wakikumbwa na taharuki.

Maeneo ambayo yalipigwa na tetemeko hilo ni mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi, jambo ambalo lilisababisha wananchi kukimbia na wengine wakiuliza bila kuwa na majibu ya kishindo kikubwa kilichopita kwenye makazi yao.

Akizungumzia tetemeko hilo jana, Mkurugenzi wa Jiolojia wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), Maruvuko Msechu, alisema tetemeko hilo lenye ukubwa wa ritcha 5.1 lilitokea majira ya mchana jana.

Alisema japokuwa limegusa maeneo mengi ya nyanda za juu kusini likianzia maeneo ya Ziwa Rukwa, lakini kitovu chake ni kilometa 40 kaskazini mashariki mwa mji wa Sumbawanga.

“Kwa kipimo hicho, kitaalamu ni tetemeko linaloweza kuwafanya watu waliosikia kukimbia kwa hofu kutoka nje ya majengo, kusababisha uharibifu wa majengo kutegemeana na ubora wa majengo hayo. Pia ukubwa unaweza kusikika kwa waendeshaji wa vyombo vya moto.

 “Kimsingi hili ni tetemeko kubwa lakini hadi sasa hakuna madhara makubwa yaliyoripotiwa. Tunawaomba wananchi watulie, wasitaharuki wakati wa matetemeko ya ardhi.

“Zaidi wachukue tu tahadhari, wasikimbie ovyo kwani wanaweza kujisababishia madhara ya kuumizana na kupata mshtuko. Pia wajiepushe kukaa chini ya miti mirefu,” alisema Msechu.

Alisema kwa mujibu wa taarifaza mashuhuda, tetemeko hilo lilisikika katika maeneo ya miji ya Sumbawanga, Chunya, Jiji la Mbeya, Mpanda na sehemu ya mkoa wa Songwe.

Katika taarifa yake, Msechu alieleza kuwa eneo hilo lililoguswa liko kwenye ukanda wa Bonde la Ufa Afrika Mashariki kwenye mkondo wa Magharibi ambao ni njia kubwa ya matetemeko ya ardhi.

Alisema GST inaendela kuwahadharisha wananchi kuzingatia ujenzi wa nyumba imara zinazoweza kukbiliana na athari za tetemeko ya ardhi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Awali, taarifa zilieleza kuwa tetemeko hilo lilizua taharuki katika Jiji la Mbeya huku baadhi ya wananchi na wafanyakazi katika ofisi mbalimbali wakitimua mbio.

Baadhi ya wafanyakazi katika maeneo ya jiji hilo waliokuwa kwenye majengo binafsi na ya Serikali walilazimika kuacha ofisi zao huku waliopo nyumbani nao wakitoka nje ya nyumba zao.

Gazeti hili lilishuhudia Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, James Kasusura na Meya wa Jiji hilo, David Mwashilindi na wafanyakazi wengine wa ofisi zilizopo uhindini wakitimua mbio.

“Kumbe na wewe unajua kukimbia, aisee Mungu mkubwa. Tulikuwa na maongezi na meya wangu lakini nikashangaa viti vinasogea ikanibidi nichukue hatua kukimbia ila cha kushangaza wakati natoka sijamwona meya katoka kupitia njia gani,”  alisikika akitamka Kasusura akimtania Mwashilindi

Hata hivyo nao watumishi wa kampuni na mashirika ya umma yenye ofisi zake jijini hapa walionekana kukaa vikundi na kuzungumza kuhusu tetemeko hilo.

Tetemeko la Bukoba

Septemba 10, 2016 tetemeko lenye ukubwa wa kipimo cha richta 5.7 liliripotiwa kutokea katika mji wa Bukoba mkoani Kagera, likiacha madhara makuwa ya maisha na mali.

Tetemeko hilo liliripotiwa kutokea kilometa 40 chini ya uso wa ardhi katika mazingira ya Kata ya Nsunga karibu na mpaka wa Uganda.

Iliripotiwa kuwa mshtuko wa tetemeko hilo ulisikika Uganda, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Kenya.

Katika tetemeko hilo, zaidi ya watu 16 waliripotiwa kufariki dunia nchini Tanzania na 203 kujeruhiwa, hasa mjini Bukoba ambako shule moja pia iliporomoka.

Zaidi ya nyumba 270 ziliripotiwa kuharibiwa na tetemeko hilo katika mji wa Bukoba pekee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles