25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

TENGA MUDA WA KUMSIKILIZA MTOTO

Na Aziza Masoud

ASILIMIA kubwa ya watoto wanaoharibika kitabia huchangiwa na mazingira pamoja na aina ya malezi anayopatiwa na mzazi au mlezi.

Wapo baadhi ya watoto wanaharibika kitabia kwa sababu ya mzazi kutokuwa makini, hasa wale wanaofanya shughuli za kujitafutia kipato mbali na maeneo wanayoishi, hivyo wanakosa muda wa kuangalia watoto kwa ukaribu.

Wazazi wanaofanya kazi ama shughuli mbali na maeneo ya makazi yao mara nyingi huwaacha watoto wao nyumbani na kulelewa na dada wa kazi na wengine hulelewa na ndugu ambao wanatoka katika familia husika.

Hali hii huchangia watoto kujifunza mambo mengi, yakiwamo mazuri na mabaya kulingana na tabia ya mtu anayekuwa naye kwa muda mrefu.

Kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wa kiume na wa kike ambao wanajiingiza katika vitendo vichafu, ikiwamo kujihusisha na mapenzi wakiwa katika umri mdogo.

Jambo hili lina sababu mbili, zipo ambazo zinachangiwa na mtoto husika kuwa mtukutu, lakini sababu nyingine ni uangalizi mbovu wa wazazi.

Mazingira ya maisha ya siku hizi mzazi anakuwa na shughuli nyingi zinazomfanya kuondoka nyumbani asubuhi na mapema na kurudi usiku.

Mbali na kuwahi kuamka, pia muda wa kurudi nyumbani nao unakuwa si rafiki, kwakuwa wapo ambao hurejea kuanzia saa mbili usiku, hivyo anakuta mtoto akiwa amelala.

Ratiba za namna hii zinafanya mzazi kutopata muda wa kutosha wa kukaa na mtoto ili kujadili mambo mbalimbali ambayo mengine yanakuwa yanamfurahisha ama kumkwaza.

Kama mzazi ni mtu wa kujishughulisha  muda mwingi, ni vizuri ukaanzisha utaratibu wa kutenga muda wa kukaa na mtoto wako kipindi cha mwishoni mwa juma.

Hii itakusaidia kumjua mtoto wako jinsi anavyoishi na watu wake na hivyo kumwepusha na makundi ya watoto wenye tabia mbaya ambazo zinaweza kuchangia kumharibu.

Kikawaida mtoto ni mtu wa kuongea endapo utamuwekea mazingira ya kuwa karibu naye, wazazi tunapaswa kufahamu kuwa, ukaribu wa mama na motto, hasa nyakati za jioni ni muhimu sana na huenda ukamwokoa mtoto katika kufanya mambo mabaya.

Mzazi unapaswa kuwa na ratiba ya kuongea na mtoto kila siku za jioni huku ukimuuliza mambo mbalimbali aliyoyafanya na kuyaona kwa siku nzima.

Njia hii inaweza ikamwokoa, kwakuwa watoto wengi hawana ujasiri wa kuficha siri kama anafanyiwa mambo tofauti na aliyoyazoea.

Wazazi tunapaswa kufahamu kuwa, dunia imebadilika, mtoto anatunzwa na mzazi husika, si dada wa kazi wala ndugu, tuwe na utaratibu wa kuongea na watoto ili tuwaepushe kuingizwa katika tabia hizi zisizofaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles