27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TEF wamshukia RC Hapi, Iringa wampa siku saba

Na WAANDISHI WETU

-DAR/IRINGA

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limesema hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kuwaingiza waandishi wa habari katika orodha ya wanaotakiwa kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali, inaashiria kuwa kiongozi huyo anatindikiwa uelewa wa sheria za nchi.

Mapema wiki hii, Hapi alitoa taarifa yenye orodha ya makundi yanayotakiwa kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali wakiwemo waandishi wa habari.

Kutokana na hilo, jana TEF kupitia Kaimu mwenyekiti wake, Deodatus Balile ilitoa tamko huku wakimtaka Hapi arekebishe agizo lake.

“TEF imesikitishwa zaidi na kauli ya Hapi kuwa amefikia uamuzi huo kuhakikisha kila mtu analipa kodi. Ifahamike kuwa Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kutoza mtu kodi.

“Chombo pekee chenye mamlaka ya kutoza kodi ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na si vinginevyo. Kauli hii inaleta wasiwasi kuwa Hapi na wenzake ikiwa nia yake katika vitambulisho ni kulipisha kodi, basi amerejesha kodi ya kichwa iliyofutwa mwaka 2004 kupitia mlango wa nyuma.

“Waandishi wa habari wanaotajwa kwenye orodha hiyo katika namba 36, ifahamike hawana bidhaa wanazouza.

“Agizo la Hapi la kuwaingiza waandishi wa habari kwenye orodha hiyo linaashiria kuwa kiongozi huyu ama anatindikiwa uelewa wa sheria za nchi, hakuomba ushauri wa kisheria au amejielekeza vibaya.

“Kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (MSA 2016) na kanuni zake za mwaka 2017 kinatambua taaluma ya uandishi wa habari na waandishi wa habari. Kazi za waandishi wa habari ni kukusanya, kuchakata, kuhariri na kuchapisha habari na taarifa.

“MSA imeweka utaratibu rasmi wa vitambulisho vya kazi kwa waandishi wa habari (press card) kutoka Idara ya Habari (Maelezo) kwa kulipia ada ya Sh 30,000 kila mwaka.

“Utaratibu huu ulikuwako tangu Sheria ya Magazeti Na 3 ya mwaka 1976 ilipotungwa.

“Ikumbukwe uandishi wa habari ni mhimili wa nne wa dola, hivyo si vyema kuushusha hadhi kwa kuugeuza kuwa ni kazi isiyo rasmi.

“Kwa kuzingatia ukweli huu wa kisheria si haki hata kidogo kuwataka waandishi wa habari wa nchi hii, bila kujali maeneo yao ya kijiografia, katika kutimiza wajibu wao wanunue vitambulisho vya watu wanaojishughulisha na sekta isiyo rasmi.

“Tungependa kumkumbusha Hapi kuwa waandishi wa habari wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria na si kupitia maagizo na matamko.

“Tunaamini kwa maelezo haya, Hapi atatambua kwamba amejielekeza vibaya katika agizo lake la kuwataka waandishi wa habari wakanunue vitambulisho vya watu wanaojishughulisha na sekta isiyo rasmi, hivyo atarekebisha agizo lake kwani linakwaza, linasumbua na kuleta mkanganyiko kwa waandishi wa habari mkoani Iringa,” ilisema taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC) kimempa Hapi siku saba kuwaomba radhi.

Akizungumza jana Mwenyekiti wa IPC, Frank Leornad, alisema kauli ya Hapi inadhalilisha taaluma ya habari.

Alisema kuwa waandishi wa habari mkoani hapa wamefanya majadiliano na kuazimia mambo sita watakayoyawasilisha katika ofisi yake na kutaka yajibiwe mapema iwezekanyo ili kuondoa sintofahamu hiyo.

“Tumesikitishwa kuwekwa katika kapu moja linalolinganisha taaluma ya habari na wafanyabiashara jambo ambalo sio sahihi na hajatutendea haki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles