24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

TDC Global wanapaswa kutuambia mchango wao kwa Taifa kwanza

TAYARI kuna video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazoonesha miongoni mwa viongozi wa Kamati ya Diaspora ya Dunia (TDC), wakiwatangazia Diaspora wa Tanzania wanaoishi kwenye nchi mbalimbali  duniani kujisajili na kukutana nchini Sweden kwa lengo la kujadili hatima yao.

Tangazo lile lilinipa tabu kulielewa kwani baadhi ya kauli ya mtoa taarifa anasema wakiwa nchini Sweden mwanzoni mwa April mwaka huu miongoni mwa watakayojadili ni sheria ya Diaspora iliyopo nchini Tanzania hususani kwenye suala la Uraia Pacha.

Sioni tatizo Diaspora kukutana na kupanga mambao yao hiyo inaonesha ukomavu wao, lakini napata tabu na mojawapo ya ajenda ambayo kama sikosei nimeisikia inayokwenda kujadiliwa ya Uraia Pacha.

Ikumbukwe kwamba suala la Uraia Pacha tayari limeshatolewa maelezo na viongozi wetu ndani na nje ya nchi tena kwenye mikutano iliyoandaliwa na Diaspora wenyewe, sasa kwenda kulijadili tenanchini Sweden inaoekana TDC hawaridhiki na majibu yaliyokwishatolewa na viongozi ambao ni wawakilishi wetu wa Serikali.

Tanzania imeweka wazi kwamba haitaruhusu Uraia Pacha kwa wakati huu lakini Diaspora wetu ambao waliamua kuukana uraia wa Tanzania kwa nia njema kabisa wanayo haki ya kutambuliwa kuwekeza katika nchi yao ya Mama waliyozaliwa.

 Yapo mambo  yanaendelea kwenye majadiliano ambayo kimsingi yatawapa haki Diaspora wa Tanzania na bila shaka haya yalijadiliwa hata kwenye Bunge la Katiba.

Hili linalokwenda kufanyika Sweden ni sasa na kutaka kuishinikiza Serikali kwamba ni lazima itoe haki ya Uraia Pacha jambo ambalo kimsingi ni kuvunja sheria za nchi yetu Tanzania. Ikiwa Waziri mwenye dhamana amekwishalitolea tamko suala hili Diaspora wanapaswa kuwa na hekima.

Mchango wa Diaspora kwa ustawi wa familia zao ni mkubwa mno hili liko wazi, lakini pia wapo Diaspora wanaotoa misaada ya elimu na afya kwa jamii zao katika maeneo wanayotoka hili linaeleweka lakini kwa sasa wanaotaka kushinikiza Serikali iwape haki ya Uraia Pacha ni lazima watueleze mchango wao kwa Taifa ni upi?

Baadhi ya Diaspora wetu wamekuwa mstari wa mbele unapofika wakati wa uchaguzi kurudi nyumbani kuweka kambi  kutaka kuwania nafasi  za uongozi lakini Diaspora hawa huwaoni kuzisaidia jamii zao wanazotoka. Hapa kuna swali wana niagani hawa.

Diaspora wengine wenye uwezo mkubwa wa ushawishi katika nchi wanazoishi Ughaibuni, hawatumii fursa hiyo kushawishi uwekezaji badala yake wanapopata fursa huipaka matope Serikali yetu, Hawa nao utawaweka kwenye kundi gani?

Ninaipongeza Serikali, kwenye suala hili la Uraia Pacha,  wakati bado haujafika na wala Diaspora wenyewe hawajaonesha nia ya dhati kuishawishi Serikali kuwapa Uraia Pacha. Ni lazima kwanza waoneshe ukomavu wao wa kizalendo kwenye nchi zao Mama waliyotoka.

Unaweza kumkuta Diaspora wa Tanzania akiizungumzia Tanzania kama vile hakuzaliwa Tanzania, hana wazazi au ndugu Tanzania aliowaacha. Sababu tu ameona ‘’Ameukata’ unaweza kujiuliza  huyu jamaa anaiwazia nini Tanzania.

Nimetoa mfano michache kuonesha ni kwanini Uraia Pacha bado Tanzania. Lakini niseme yanayotokea sasa sio kwamba yanawagusa Diaspora wote, ukiangalia Diaspora wa Sweden ni mfano wa kuigwa . wakati fulani nilitembelea nchi za NORDIC, nikabahatika kukutana na aliyekuwa  Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden na katika nchi za NORDIC, Jacob Msekwa, ambaye nilijadiliana naye mambo mbalimbali yanayohusiana na mchango wa Diaspora wa Sweden kwa nchi yao.

Tulijadiliana juu ya malalamiko ya Diaspora wengi niliobahatika kukutana nao wanaohitaji  kuja kuwekeza nchini lakini wanakumbana na vipingamizi vingi ikiwamo kutakiwa kutoa rushwa wakidhaniwa kuwa wana fedha nyingi na mwisho hukata tamaa

Msekwa alijibu vyema kwamba wanajaribu kuwasiliana na makao makuu, kuwaambia wajaribu kuangalia kutafua njia ya kuwasaidia kwa sababu hawa watu wanafanya hivyo kwa mapenzi ya nchi yao.

Alisema jukumu lao kubwa ni kuwapa moyo juu ya changamoto na matatizo wanazokutana nazo nyumbani na kuwaeleza wasivunjike moyo, alitanabaisha kuwa  hayo mambo yanaanza kubadilika na somo la Diaspora limeanza kueleweka.

Msekwa pia alieleza mchango wa Jumuiya ya Diaspora wa Sweden ilivyojipanga kupeleka maendeleo nyumbani licha ya changamoto mbalimbali.

Lakini Msekwa alisisitiza kuwa kama walivyoona katika Rasimu ya Katiba Mpya kwamba suala la uraia pacha kwa sasa hivi halitakuwapo, lakini mtu yeyote mwenye unasaba na Utanzania atakapokwenda Tanzania atapewa hati ya Ukaazi wa kudumu (Resident Permanent) ambayo itatungiwa sheria ya jinsi itakavyotumika na mipaka yako itatafsiriwa katika sheria ile itakayotungwa. Maoni yanaweza kuwa kwamba mtu anaweza kuwa na haki zote isipokuwa labda kupiga kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles