25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TDB YAIKOPESHA TANZANIA BIL 900/-

Na BENNY MWAIPAJA – WFM, DAR ES SALAAM


BENKI ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (Trade & Development Bank – TDB), itaikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 400, sawa na Sh bilioni 900, kwa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) na mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa.

Hayo yalisemwa  Dar es Salaam jana na Rais wa benki hiyo, Admassu Tadesse, alipokutana na kufanya mazungunzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani.

Tadesse alisema benki yake imetenga Dola za Marekani milioni 200 kwa ujenzi wa reli ya kati ya kisasa na kiasi kingine kama hicho kwa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa mkoani Lindi.

“Tanzania ni mdau mkubwa wa benki hii, ikiwa inashika nafasi ya saba kati ya nchi na taasisi 37 zinazomiliki hisa zake, inamiliki hisa asilimia 6.4,” alisema Tadesse.

Alisema hadi Machi, mwaka huu, benki yake inatekeleza miradi 11 ya maendeleo katika sekta ya kilimo biashara, huduma za benki na fedha, nishati, ukuzaji miundombinu na viwanda, yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 284.6.

“Tuna miradi mingine iliyoidhinishwa, inayokadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 157, kiasi kingine cha dola milioni 660 ambacho kimepangwa kutolewa kwa Tanzania ili kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za kilimo biashara, ujenzi, kemikali na petroli pamoja na sekta ya nishati,” alisema Adesse.

Naye Waziri Mpango aliipongeza benki hiyo kwa kuendelea kujiimarisha kimtaji na kiuendeshaji na kwamba Tanzania inapokea kwa mikono miwili ahadi yake.

Alisema atahakikisha mazungumzo kuhusu upatikanaji wa mkopo huo nafuu yanakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa ili fedha zipatikane.

Kwa upande wake, Waziri Kalemani, alisema mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa, utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 318 na utaongeza kiwango cha upatikanaji umeme ambacho hivi sasa kimefikia megawati 1,500.

“Lakini pia tuna vijiji 176 vinahitaji umeme ambapo kati yake vijiji 120 viko kwenye visiwa na vinahitaji kupatiwa huduma ya nishati ya umeme na TDB imekubali kusaidia ujenzi wa miradi ya umeme kwa kutumia nguvu ya maji ambapo kila mradi utazalisha megawati 10 za umeme,” alisema Dk. Kalemani

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles