25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TCU yatoa mwongozo kujiunga vyuo vikuu

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

SIKU chache baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Nacte) kutangaza matokeo ya kidato cha sita, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la udahili awamu ya kwanza kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu nchini kwa mwaka 2019/20.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, alisema udahili huo utaanza Jumatatu na utakwenda sambamba na maonesho ya vyuo vikuu nchini.

Profesa Kihampa alisema udahili huo utahusisha wanafunzi waliomaliza kidato cha sita, diploma na wale waliokuwa wanasoma kozi ya msingi (foundation) katika Chuo Kikuu Huria (OUT) kwa sababu ndicho kinachokubalika kisheria kutoa masomo ya kozi hiyo.

Kuhusu wanafunzi hao wa kozi ya msingi, alisema ni wale waliopata GPA 3 na kupata daraja C katika masomo ya Sanaa, Sayansi na Biashara.

“Kila mwenye sifa anapaswa kuomba nafasi kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Serikali kwa mujibu wa sheria,” alisema Profesa Kihampa.

Alisema wanafunzi wanapaswa kuingia tovuti ya TCU na kuomba moja kwa moja kwenye chuo wanachokitaka kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa na Serikali ili kupunguza usumbufu wa kuomba mara mbili kwenye vyuo tofauti.

Aliongeza kuwa wanafunzi waliomaliza nje ya nchi, wanapaswa kuwasiliana moja kwa moja na Necta au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) kulingana na kiwango cha elimu aliyonayo ili waweze kuhakikiwa kabla ya kujiunga na vyuo vikuu.

Ili kuepusha usumbufu kwa wanafunzi, Profesa Kihampa alisema TCU iliweza kutoa elimu kwa makamu wakuu wa vyuo vikuu nchini ili kuweka mazingira rafiki ya wanafunzi pindi wanapokuwa katika udahili.

Alisema lakini pia TCU iliweza kushirikiana na Wizara ya Mafunzo ya Elimu na Amali ya Zanzibar ili kutoa elimu kwa wakuu wa vyuo Unguja na Pemba.

Pia waliweza kupita kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako kuna baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wamejiunga na kambi hizo na kuwapa elimu.

“Huu ni udahili wa awamu ya kwanza kwa wanafunzi hao, tutafunga dirisha la udahili ifikapo Agosti 10, mwaka huu na kuangalia changamoto zilizojitokeza ili tuweze kuzifanyia kazi kabla ya kuingia kwenye udahili wa awamu ya pili,” alisema.

Aliongeza kuwa wiki ya maonyesho ya vyuo vikuu inaanza Jumatatu, hivyo wanafunzi, wazazi na walezi wanaweza kujitokeza viwanja vya Mnazi Mmoja ambako vyuo vyote vitakuwepo kutoa elimu kwa wananchi.

“Tunawaomba wazazi, walezi na wanafunzi wajitokeze kwenye viwanja vya Mnazi mmoja kwa ajili ya kupata elimu ya jinsi ya kujiunga na vyuo vikuu nchini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles