27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TCRA UDHIBITI KWENYE SEKTA YA MAWASILIANO

Na Mwandishi Wetu


UDHIBITI ukifanywa vizuri na kwa nia njema huleta tija kwa wadau wake, kwani ushindani huwa murua kwa kupata tambarare ya kuchezea na kufanya shughuli husika.

Hali hiyo imejitokeza sana kwenye sekta ya mawasiliano na hususani ya simu za mkononi, ambapo uwekezaji unakua, kiwango cha bei kupiga  simu hupungua kwa wateja na uwekezaji hugombewa.

 

Kutokana na kuwepo miundombinu ya kusimamia mwenendo mwema wa simu, sekta hiyo imeanza kutoa picha nzuri ya tija kwa wadau wake na hivyo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeona haja ya kupunguza bei za miito ya simu na kuagiza utendaji wake kwa watoa huduma za simu kubadilisha kiwango cha utozaji wa upigaji simu wao kwa wao na wateja wao ili faida iliyopatikana iwafikie wateja na wadau wa mawasiliano.

Gharama simu za mkononi zote zapunguzwa

TCRA imepunguza viwango vya gharama za mawasiliano ya simu kwa dakika kutoka Sh26.96 hadi Sh 15.60  kuanzia Januari mosi mwaka huu, jambo ambalo limeshangiliwa na watumiaji wa simu.

Hayo yanatendeka ili kuongeza ufanisi katika sekta ya mawasiliano kwa miaka mitano ijayo na itaendelea kupungua kila mwaka.

Hatua hiyo ya TCRA pia inawanufaisha watumiaji wa simu kwa kuwa zitaendelea kupungua kila mwaka hadi kufikia Sh 2.00 kwa dakika ifikapo mwaka 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, alisema jijini Mwanza kuwa hatua hiyo inatokana na mafanikio katika udhibiti wa sekta ya mawasiliano nchini. Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mamlaka ilifanya tathmini juu ya kupunguzwa kwa kiwango hicho ikiwa ni moja ya sehemu ya kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia huduma za mawasiliano.

“Kwa kuzingatia kwamba viwango vya mwingiliano vya sasa vilifikia ukomo Desemba 31, mwaka jana, TCRA imetoa uamuzi mwingine wa viwango vipya vitakavyodumu kwa kipindi kingine cha miaka mitano kuanzia Januari mosi, 2018 hadi Desemba 2022.”

Alisema mwaka 2018 itakuwa Sh 15.60, mwaka 2019 Sh 10.40, mwaka 2020 Sh 5.20, mwaka 2021 Sh 2.60 na mwaka 2022 itakuwa Sh 2.00 kwa dakika.

Mhandisi Kilaba aliwataka watoa huduma za mawasiliano ya simu nchini kutokana na punguzo hilo kuzingatia viwango vipya vya gharama za mwingiliano wa mitandao ya simu na kuhakikisha vinaanza kutumika Januari mosi kwa mujibu wa sheria inavyotaka.

Ukiachia tija, gharama za kudumu za uwekezaji na uendeshaji wa kampuni husika zimekuwa zikipungua kadiri muda unavyopita na hivyo huu ni wakati mwafaka kwa kiwango cha tozo za simu kupungua kwa wateja wake.

 

Chaneli za taifa kuwa bure

Mkurugenzi Mkuu hakuridhika na mwenendo wa baadhi ya watoa huduma za ‘multiplex’ ambao wanawatoza huduma za matangazo zile chaneli za taifa ambazo ni za bure (FTA).

 

Kuhusu kutozwa fedha kwa watazamaji ili kuona chaneli za bure za runinga, alisema Desemba 22, mwaka jana, waliitoza Kampuni ya Star Media Tanzania Limited faini ya Sh milioni 100 baada ya kubainika kuwatoza fedha watazamaji wake kwa chaneli zinazotakiwa kuonekana bure kupitia king’amuzi chake cha Star Times (ST).

 

“TCRA inaendelea kufuatilia ili kuhakikisha ving’amuzi vya Star Times, Continental, Digitek na Ting, vinaendelea kuonyesha chaneli zote za kitaifa na FTA bure kwa mujibu wa sheria kwenye chaneli za TBC1, ITV, EATV, Channel Ten, Star TV na Clouds TV,” alisema Kilaba kwa msisitizo.

 

Mkurugenzi Mkuu aliwaasa Watanzania kupokea  na kutumia maendeleo ya mawasiliano kwa mtazamo chanya ili kuendelea kutafuta na kupata taarifa sahihi na kutojaribu kubadilisha namba za utambulisho (IMEI reprogramming) katika vyombo vya mawasiliano zikiwamo simu ili kukwepa uhalisia wa mambo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles