30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TCRA: Tumezima vifaa, simu feki laki 6

Simu-feki*Wasema zoezi bado linaendelea, usiku wake kama mwaka mpya

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mawasiliano Nchini, (TCRA) jana imezima namba tambulishi (IMEI) 603,000 sawa na asilimia 2.9 ya vifaa vya mawasiliano ikiwa ni pamoja na simu feki zinazotumika nchini.

Kuzimwa kwa vifaa hivyo ni utekelezaji wa agizo la serikali la kuondoa  bidhaa  feki za mawasiliano kuanzia Juni 16.

Akizungumza  na gazeti hili,  Ofisa Uhusiano wa TCRA, Innocent Mungy, alisema vifaa  vya mawasiliano vilivyozimwa ni pamoja na simu za mkononi, ipad, tableti na modemu.

“Watu wanapaswa kujua zilizozimwa si simu feki tu, kuna vifaa vingi feki  vya mawasiliano na vinatumia laini za simu na vingine vinatumika bila laini vyote tumevizima,” alisema Mungy.

Alisema kati ya vifaa 603,000 vilivyozimwa kuanzia saa sita usiku wa kuamkia jana, idadi ya simu za mkononi bado haijapatikana kwakuwa namba ya utambulisho inayozimwa huwa  haionyeshi kifaa husika  kama ni simu, modemu au kitu kingine jamii ya hivyo.

Akifafanua uvumi kuwa simu zenye namba tambulishi zaidi ya mbili ni feki, Mungy alisema si kweli kwakuwa kuwapo kwa kifaa chenye namba hizo zaidi ya moja kunategemea na kampuni iliyotengeneza.

Mungy pia alisema namba tambulishi nyingi zilizozimwa zimeonekana zilikuwa zikitumika katika maeneo ya mijini  wakati  vifaa vichache vimezimwa  vijijini.

“Mtu  wa kijijini hawezi kutumia simu feki wale wanataka wanunue kitu kikae muda mrefu, tatizo lipo mijini watu wananunua vifaa vya mawasiliano kwa matumizi ya dharura anaamini atanunua nyingine baadaye, lakini wapo wale wanaopenda kutumia vitu vizuri  lakini hawana fedha bidhaa feki kwa bei nafuu,” alisema Mungy.

Alisema simu zote zilizozimwa ni feki  bila kujali nchi zilizotengenezwa na kusisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu nchini kwamba wale ambao bado simu zao hazijazimwa watarajie kuzimiwa wakati wowote.

Alisema   TCRA haijatumia gharama yoyote kutekeleza zoezi hilo kwakuwa mtambo wa kufanya kazi hiyo  ulinunuliwa na kuzinduliwa tangu mwaka  2014.

“Hatujatumia gharama yoyote kuzima   vifaa hivyo, tumetumia  software(program) ambayo ipo katika mtambo huo,” alisema Mungy.

Alisema mtambo huo ulinunuliwa  na serikali Desemba 2013 kwa  gharama ya dola za Kimarekani milioni 25 (sawa na shilingi za kitanzania Sh bilioni 54)  na kuzinduliwa Februari 2014 na rais wa awamu ya nne,  Jakaya Kikwete.

Alisema siku 90 kabla ya kuzimwa vifaa hivyo feki, TCRA ilitoa maelekezo kwa kampuni za simu kuhakikisha inafanya uhakiki na kukusanya simu feki  pamoja na kugawa bure simu halisi.

Alisisitiza utaratibu wa kukusanya simu feki kwa watumiaji utakwenda sambamba na kuziondoa sokoni ambapo TCRA kupitia Baraza la Mazingira nchini litafanya utaratibu  wa kuhakikisha wanaziteketeza.

 

Usiku wa kuzima simu feki

Joto la wasiwasi lilianza kupanda kuanzia Juni 15 na Juni 16 iliyokuwa siku ya mwisho ya kutumia vifaa hivyo visivyo na ubora lilizidi.

Usiku wa kuamkia jana ulikuwa wa aina yake, wengine waliufananisha na mkesha kama ule wa mwaka mpya baada ya watu wengi kuonekana wakisubiri igonge saa sita kamili ili kujua hatima za simu zao.

Watumiaji wa mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Whatsapp, Telegram, Facebook na Twitter walionekana kutumia muda mwingi kutaniana kwa meseji, mashairi na picha dhidi ya wale wenye simu feki.

Wapo ambao hawakufanya uhakiki na hata wale waliofanya pamoja na majibu waliyokuwa wamepata bado walitaka kushuhudia kitendo hicho.

Akizungumza na gazeti hili jana, Godfrey Nanzaro, alisema simu yake ilionyesha mapema kwamba ni feki lakini usiku wa kuamkia jana hakulala mapema na hata alipoamka asubuhi alihakikisha simu yake lakini bado ilikuwa haijazimwa.

Siku ya jana ilitumika kwa ajili ya kupeana pole kwa waliozimiwa simu na kupongezana, katika mitandao ya kijamii hususani makundi ya Whatsapp kulikuwa na utani mwingi ikiwa ni pamoja na kuitisha majina kuona kama kuna yeyote amekosekana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles