27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TCAA:Uwezo wetu kudhibiti usalamawa anga umepanda

Na CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema matokeo ya ukaguzi uliofanywa mwaka jana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga  Duniani (ICAO), unaonyesha Tanzania imepanda katika uwezo wa kusimamia na kudhibiti usalama wa sekta kutoka asilimia 37.8 (2013 ) hadi kufikia asilimia 64.35 (2017).

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga Duniani (ICAD), Mkurugenzi Huduma za Mamlaka wa TCAA, Mbutolwe Kabeta, alisema jitihada za TCAA za kuboresha miundombinu na rasilimali watu zimeanza kuzaa matunda na alama hizo zinaifanya Tanzania kuwa juu ya kiwango cha wastani wa asilimia 60 kilichowekwa na ICAO.

Kabeta aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari, alisema lengo ni kuendelea kuimarisha uwezo wao wa kudhibiti sekta ili iweze kwenda juu.

Alisema TCAA imeweza kuongeza idadi ya wataalamu wa udhibiti katika maeneo ya usalama.

“Wakati tunasherehekea maadhimisho ya dunia (ICAD) inayoadhimishwa kila mwaka Desemba 7, yenye kauli mbiu ya hakuna nchi itakayoachwa nyuma, TCAA tunayo mengi ya kujivunia kwa sababu ya kujipanga vyema,” alisema Kabeta.

Pia alisema wanaendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ikiwamo utekelezaji wa miradi mikubwa minne ya ufungaji wa rada nne za kuongoza ndege.

Kabeta alisema mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 67.3 utakapokamilika, utawezesha anga yote kuonekana katika mfumo wa rada.

“Mfumo huu pia mbali ya kuongoza ndege utasaidia pia kuimarisha usalama wa anga,” alisema Kabeta.

Alisema ujenzi wa rada unaoendelea katika Kiwanja cha Ndege cha Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), umekamilika na tayari mtambo wa rada umewasili na utaanza kufungwa wakati wowote kuanzia sasa.

Pia alisema TCAA inaendelea kuboresha Chuo cha Mafunzo ya Usafiri wa Anga (CATC) kinachotoa mafunzo kwa wataalamu walioko katika sekta pamoja na wanaotaka kujiunga na sekta hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles