27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TCAA yatumia Sh bil 82 kuboresha mifumo

Leornard Mang’oha Na Erick Mugisha -Dar es salaam

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imetumia zaidi ya Sh bilioni 82 kununua na kuboresha mifumo ya kufuatilia na kuongozea ndege na kudhibiti masuala ya usalama kwa miaka minne.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari aliitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na ununuzi wa rada nne zilizofungwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mwanza na Songwe kwa gharama ya Sh bilioni 67.3.

Mingine ni mfumo wa kuongoza ndege kwa njia ya sauti (VHF) kwa Sh bilioni 1.7, mfumo wa kuandaa ankara kwa Sh bilioni 1.7, mfumo wa kusaidia rada (ADSB) Sh bilioni 2.2, mfumo wa mawasiliano ya sauti baina ya kituo na kituo au rubani kwa rubani Sh bilioni moja.

Pia fedha hizo zimetumika kufunga mfumo wa kuruhusu ndege kutua katika hali yoyote ya hewa (ILS) uliogharimu Sh bilioni 4.6, mfumo wa kukusanya data katika usafiri wa anga (AMHS) kwa gharama ya Sh bilioni 1.5, kuanzishwa kwa mfumo wa Simleta ili kuongeza udahili wa wanafunzi wa kimataifa Chuo cha Usafiri wa Anga cha mamlaka hiyo kwa gharama ya Sh bilioni 1.8 na mnara wa kuongozea ndege Uwanja wa Ndege wa Pemba.

“Tunapoboresha hii mifumo ya ufuatiliaji na ‘movement’ zikaongezeka, hata mapato yataongezeka kwa sababu ndege zinazoruka katika anga la Tanzania zitaongezeka lakini hata zile zinazotua huko sehemu nyingine na migodini tutakuwa na uwezo wa kuziona,” alisema Johari.

Alisema Mkataba wa Kimataifa wa Chicago, Shirika la Usafiri wa Anga Duniani wa mwaka 1944, ulielekeza wanachama wake kuhakikisha wanapandisha maksi zinazotokana na masuala mbalimbali yanayohusu usafiri wa anga walau kufikia 60 ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwako baadhi ya mashirika kutoruhusiwa kutua.

Johari alisema kutokana na maagizo hayo, Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zilizosaidia kuongeza maksi hizo kutoka 37.8 mwaka 2015 hadi 64.4 mwaka 2017, huku wakitarajia kufikia maksi 85 hadi 90 mwaka 2021, utakapofanyika ukaguzi mwingine.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) iko mbioni kuwezesha Uwanja wa Ndege wa Arusha kupokea ndege kubwa za kuanzia abiria 70.

Mkurugezi wa Uhandisi na Huduma za Ufundi wa TAA, Mbila Mdemu, alisema miongoni mwa maeneo yanayotarajiwa kuboreshwa katika uwanja huo ni pamoja na kuongeza kipande cha mita 200 katika njia ya kuruka na kutua ndege ili kufikia urefu wa kilomita 1.8.

Alisema maeneo mengine yanayotarajiwa kuboreshwa ni pamoja na mageuzio ya ndege yatakayowezesha hadi ndege 30 kupaki, pamoja na maegesho ya magari ili kuongeza mapato.

“Pia tumeweza kufanya marekebisho ya kusimika taa za kuongozea ndege usiku mkoani Tabora na tumeshasaini mikataba ya ukarabati ya majengo ya abiria ya uwanja wa ndege pamoja maegesho wa magari mikoa kama Tabora na Shinyanga,” alisema Mdemu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles