31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tatizo la waamuzi linavyotesa soka la Tanzania

pg-6

Na MARTIN MAZUGWA,

SUALA la waamuzi limekuwa kilio kwa timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kutokana na maamuzi yao ya kushindwa kufuata sheria 17 za mchezo wa soka.

Hivi sasa umekuwa ni wimbo kwa makocha na viongozi wa timu zinazoshiriki ligi hiyo tatizo linaloonekana kuwa sugu na lisipofanyiwa kazi mapema litakuwa na athari kubwa hapo baadaye.

Waamuzi wamekuwa wakitupiwa lawama mara kwa mara huku wengi wao wakishutumiwa kupokea kitu kidogo jambo linaloibua hasira kwa mashabiki.

Kwa aina ya waamuzi tulionao tusahau kabisa kuwaona wakichezesha michezo ya kimataifa kutokana na makosa wanayoyafanya, kitendo cha kuyafumbia macho haya yatazidi kudhoofisha soka hapa nchini.

Huwa nashindwa kuelewa ni wapi waamuzi wanaochezesha ligi ya hapa nyumbani wanapoteleza, kuwa ni tamaa ya fedha au mapenzi na timu fulani.

Napata mashaka kama kweli waamuzi wetu huwa wanafuzu vigezo vinavyotumiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na kupokea beji za shirikisho hilo kubwa.

Inashangaza kuona refa aliyepitia kozi za FIFA akifanya mambo ya ajabu kama waamuzi wanaochezesha ligi za mchangani ambao wanachezesha soka kwa utashi wao.

Ligi Kuu Tanzania Bara imekosa waamuzi wenye msimamo pamoja na hali ya kujiamini kitu kinachosababisha washindwe kutoa maamuzi sahihi hasa pale mchezo unapokuwa na presha kubwa.

Mmoja wa waamuzi  bora wa VPL msimu wa 2011/12, Martin Saanya wa Morogoro, aliwahi kufungiwa msimu mzima baada ya kutoa penalti kwa Coastal Union iliyozaa bao la kusawazisha katika mechi ya kwanza Agosti 24, 2013, huku Yanga wakitoka sare dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa.

Saanya aliokolewa na msamaha kwa wafungwa wa TFF uliotolewa na Rais Jamal Malinzi muda mfupi baada ya kushinda kiti cha urais wa shirikisho hilo usiku wa  Oktoba 28 mwaka 2013.

Mwamuzi huyu ambaye alichezesha pambano la watani wa jadi, Yanga na Simba, pambano lililoisha kwa sare lakini likisababisha uharibifu mkubwa wa Uwanja wa Taifa mara baada ya kukubali bao lenye utata lililofungwa na mshambuliaji wa Yanga, Amis Tambwe.

TFF wanapaswa kuwa makini na suala hili la waamuzi kwani hadi sasa timu zaidi ya mbili zmetoa lawama huku baadhi ya viongozi wa timu wakitishia kujiuzulu kutokana na maamuzi yasiyoridhisha yanayotolewa na waamuzi.

Kati ya wahanga wa kupata tatizo la waaamuzi ni kocha mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ambaye amejiuzulu nafasi yake mara baada ya mwamuzi kushindwa kufuata sheria za mchezo wa soka katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City.

Mbali na Julio, pia kocha mkuu wa African Lyon amekumbana na karaha za waamuzi hawa ambao wamekuwa hawafuati sheria 17 za mchezo wa soka, jambo ambalo linafanya soka letu kukumbwa na migogoro isiyokwisha.

Si Saanya pekee aliyewahi kufungiwa mara baada ya kutoa maamuzi yenye utata, wafuatao ni marefa ambao pia wamewahi kukumbana na adhabu  kama aliyopewa mwamuzi huyo.

Wengi wa waamuzi wamekumbana na adhabu ya kufungiwa mara baada ya kuchezesha mechi kubwa hasa zinazohusu klabu kubwa za Simba na Yanga zenye mashabiki wengi hapa nchini.

Mmoja kati ya waamuzi bora kutoka mkoani Mwanza, Mathew Akrama mwenye beji ya Fifa, alikumbana na adhabu ya kufungiwa baada ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya Simba uliochezwa msimu wa 2012-13, baada ya kushindwa kuendana na kasi ya mchezo hali iliyosababisha atoe maamuzi yenye utata.

Mwamuzi Ferdind Chacha ambaye pia alikuwa mmoja ya marefa waliochezesha mchezo uliopita kati ya Yanga na Simba ulioisha kwa sare ya kufungana bao 1-1, aliwahi kukumbana na adhabu ya kufungiwa mwaka mmoja msimu wa 2012-13 baada ya kushindwa kuumudu mchezo wa Simba na African Lyon.

Wengine ni Ephrony Ndissa alikuwa moja ya marefa katika mchezo kati ya Yanga na Simba uliopigwa mwaka 2012/13, alifungiwa kwa kushindwa kwenda na kasi ya mchezo na kutoa maamuzi yenye utata.

Ronald Swai huyu ni mwamuzi aliyefungiwa baada ya kushindwa kwenda na kasi ya mchezo wa Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro uliochezwa katika Uwanja wa Taifa msimu wa 2012-13 .

Alex Mahagi huyu ni mwamuzi aliyefungiwa mara baada ya kushindwa kwenda na kasi ya mchezo kati ya klabu ya Simba na JKT Ruvu.

Waamuzi wengine waliowahi kufungiwa baada ya kuchezesha chini ya viwango katika michezo isiyozihusisha klabu za Simba na Yanga.

Methusela Musebula, Lingstone Lwiza hawa walichezesha mchezo kati ya Toto Africans ‘Wanakisha mapanda’ dhidi ya Coastal Union ‘Wagosi wa kaya’ uliochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Wengine ni Idd Mikongoti na Samson Kobe waliochezesha pambano kati ya Toto Africans na Mtibwa Sugar lililopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba.

TFF wanapaswa kuangalia kwa makini suala la waamuzi ili kuepusha lawama kwa klabu zinazoshiriki ligi kuu msimu huu ambazo zimekuwa zikitoa lawama kila kukicha kuhusu waamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles