31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TATIZO LA KENYA NI UTAWALA AMA RAILA?

Na Leah Mwainyekule

JIRANI zetu Kenya si wageni wa sarakasi za kabla na baada ya uchaguzi mkuu.  Hata hivyo, tofauti yao na sisi ni namna sarakasi hizo zinavyoenda kuishia na matokeo yanayotokana na malumbano yoyote waliyonayo.  Tuliyashuhudia hayo katika chaguzi zilizopita, hasa katika uchaguzi mkuu miaka kumi iliyopita ambao ulisababisha mauaji ambayo hayakutarajiwa.

Kilichotokea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, huenda kikawa na dalili za kutokea tena hivi sasa.  Uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 mwaka huu ulifutwa na mahakama nchini Kenya, baada ya kuthibitishwa kwamba ulikuwa na kasoro mbalimbali ambazo zilisababisha matokeo yasiwe huru wala haki.  Baada ya hukumu hiyo mahakama iliamuru kuwa uchaguzi wa marudio ya kiti cha urais kufanyika ndani ya siku 60 na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya imeshatoa tarehe ya uchaguzi huo kufanyika wiki ijayo, yaani Oktoba 26.

Hata hivyo, mpinzani mkuu wa Serikali ya Kenya ambaye pia ni mgombea Urais kupitia chama cha NASA, Raila Odinga, amejiondoa kwenye uchaguzi huo wa marudio akidai kwamba hawezi kushiriki uchaguzi ambao bado utakuwa na kasoro zile zile zilizoainishwa na mahakama, kutokana na Tume ya Uchaguzi kutofanya mabadiliko yoyote.

Kujitoa kwa Raila katika kinyang’anyiro hicho, ndicho kinachotia hofu.  Tayari Rais wa sasa ambaye anagombea nafasi hiyo kwa kipindi cha pili, Uhuru Kenyatta, amemshutumu Raila na kusisitiza kwamba uchaguzi utakuwa pale pale, hata kama mpinzani huyo ameamua kutoshiriki.

Wakati huo huo, wafuasi wa Raila wameamua kuandamana ili kushinikiza mabadiliko katika tume.  Raila mwenyewe anabembeleza Jumuiya ya Kimaaifa kuingilia kati ili kuwe na mazungumzo ya kusaidia kufanikisha kutatua mgogoro uliopo, kabla haujawa mbaya zaidi.

Wakati hayo yakiendelea, Rais Kenyatta amezitahadharisha nchi za kigeni kutoingilia kinachoendelea Kenya na kudai kwamba tatizo pekee lililopo Kenya ni mtu mmoja aitwaye Raila Odinga na kamwe hawatawaruhusu wazungu kuwaambia cha kufanya, bali waendelee tu kutembelea nchini humo kama watalii.

Sasa kwa hali inavyoendelea nchini Kenya, ni vigumu kuainisha hasa tatizo liko wapi.  Ni kweli kwamba kuna mgogoro Kenya na ni mazungumzo ya kuratibiwa na nchi zingine ndiyo yatakayotoa suluhisho? Au ni kweli kwamba Raila ndiye tatizo lililopo Kenya na hakuna haja ya kukaa kuzungumza naye kwakuwa anatafuta huruma?

Si rahisi sana kujua kwa kinagaubaga tatizo hasa la Kenya ni lipi, kati ya uchaguzi usiokuwa huru ama Raila Odinga.  Ni kweli kwamba siku zote Raila amekuwa mtu wa kulalamikia kila kitu na kuhama hama vyama vya siasa alimradi tu apate kuwa mgombea wa kiti cha urais.  Ni kweli vile vile kwamba wakati mwingine ukimsikiliza Raila na kujaribu kutafuta maendeleo hasa anayoyaahidi kwa Wakenya, unaishia kugundua kwamba lengo lake hasa ni kuupata tu urais ili auburudishe moyo wake.

Lakini wakati huomhuo, ni kweli kwamba uchaguzi wa mwaka 2007 ulikuwa na kila aina ya kasoro kiasi cha kusababisha mapigano yasiyokuwa ya lazima na mgogoro baadaye kusuluhishwa kwa mazungumzo pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Taifa.  Ni kweli pia kwamba katika uchaguzi uliofanyika Agosti mwaka huu, kasoro zilikuwapo na ndio maana mahakama ikaamua kuwe na marudio ya uchaguzi kwa kiti cha Urais.

Sasa hapo ndipo baadhi ya watu tunapojiuliza, tatizo la kweli la Kenya ni lipi?  Ukiachilia mbali sababu za kupenda sana madaraka kwa Raila, sababu ya Rais Kenyatta kutotaka kufanya naye mazungumzo na kugawanyika kwa Kenya kwa minajili ya nani anatokea wapi, lipo tatizo ambalo nadhani halizungumzwi, lakini ambalo ndilo kiini cha yote hayo.

Naomba tu niwatahadharishe Wakenya kwamba ifike mahala wao wenyewe wayatatue matatizo yao, kwani wanayajua.  Ifike mahala pia wananchi wa Kenya wafahamu kwamba nchi ni ya kwao na si tu ya viongozi wao wanaowatawala ama wale wanaotaka kuwatawala.

Wakati hao wananchi wakipigana na kuuana, viongozi wao ambao hao wananchi wanapigana kwa ajili yao watakuwa wamestarehe wakifuatilia kila kitu kupitia vyombo vya habari na kuchekelea kwamba wapo wafuasi wanaojitolea kwa ajili yao.  Jirani zangu, tuamke!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles