33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tasaf ilivyookoa maisha ya mama aliyetelekezwa na mume

Na CHRISTINA GAULUHANGA-NJOMBE

WAPO wanawake ambao wamejikuta wakipoteza mwelekeo wa maisha kwa sababu mbalimbali ikiwamo ugumu wa maisha, kukosa mtaji, kufiwa na waume zao na wengine kutelekezwa.

Pia baadhi ya wanawake wamejikuta wakiendelea kuteseka kwa sababu ya mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zina mnyima fursa ya kumiliki ardhi au mali.

Vitendo kama hivyo na vinginevyo vimesababisha kila kukicha kundi hili kurudi nyuma kimaendeleo na kuonekana  kama ni watu wa kupewa misaada au kuwezeshwa katika mahitaji yao au ya kifamilia kila kukicha. 

Kukithiri kwa matukio kama haya na mengineyo, kulizifanya  asasi za kiraia na za serikali kulivalia njuga jambo hili na kudhamiria kwa dhati kuwashika mkono wanawake kwa kutoa elimu ya ujasiriamali na hata kuwawezesha kupata mikopo au mitaji yenye riba nafuu ili waweze kujikwamua hatimaye kuondokana na unyanyapaa ndani ya jamii. 

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ulio chini ya Serikali, ni mojawapo ya wadau ambao waliamua kuziwezesha kaya maskini, vikundi vya kijamii na jamii kwa ujumla ili kufikia maendeleo endelevu yenye tija kuanzia ngazi ya mtu mmoja mmoja.

Mwanamke Aurelia Kiwale, mkazi wa Kijiji Cha Msetule, Makambako, ni miongoni mwa wanawake ambao wanaweza kusimama hadharani kuelezea ujasiri, changamoto na mafanikio kadhaa waliyoyapata baada ya kutelekezwa na mumewe tangu mwaka 2008 hadi sasa. 

Anasema alibahatika kupata watoto watatu aliozaa na mumewe, ambaye hakutaka kumtaja jina, lakini hadi leo hafahamu alipo na hajawahi kutuma fedha yoyote kwa ajili ya kujikimu wala salaam.

“Niliachwa na mume huyu akidai anakwenda kutafuta maisha Mlimba, mkoani Morogoro, mwaka 2008, akisema atarudi lakini hadi leo sijui alipo.

“Tangu aondoke hajawahi kupiga simu wala kutuma fedha ya matumizi hivyo, niliamua kuanza kupambana na watoto wangu ili niweze kuwajengea misingi imara ya maisha,” anasema Aurelia.

Anasema aliamua kuanza kufanya vibarua kwenye mashamba ya watu huku akiishi kwenye mapori katika nyumba za nyasi na watoto wake hao ambao walikuwa hawajaanza hata shule.

Anasema kuwa baada ya muda mfupi alifanikiwa kununua mbuzi wawili na kuanza kuwafuga na baadae alipata fursa ya kusaidiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao walimwongezea mbuzi sita wakawa jumla nane na akaendelea kuwafuga kwa lengo la biashara.

“Namshukuru Mungu TASAF imenitoa mbali kwani sikutegemea kama hadi leo mimi na familia yangu tungekuwa hai kwakuwa tumepitia mapito mengi ikiwamo kulala porini kwa sababu ya kukosa mwelekeo, lakini leo hii nina inuka kifua mbele kwa sababu nina mradi wangu wa mbuzi ambao umeniokoa na kunisababishia watoto wangu wapate mahitaji muhimu ya chakula, mavazi na elimu,” anasema Aurelia.

Anasema kwa sasa ana mbuzi wa kutosha na kuku na amefanikiwa kujenga nyumba ya matofali ambayo imemuondolea adha ya kutangatanga porini kutafuta mahali pa kuishi na watoto wake.

Aurelia anakumbuka wakati mume huyo anamtekeleza alikuwa na watoto wadogo watatu ambao hawajaanza shule lakini kwa sasa ameweza kumudu kuwapeleka shule na kukidhi gharama za masomo.

“Kwa sasa ninachokiangalia ni watoto wangu na mifugo kwani ndio kila kitu katika maisha yangu, namuomba Mungu Tasaf iendelee kutuangalia sisi wanyonge kwa sababu inatusaidia kujikomboa kimaisha pamoja na kutufungulia ufahamu kuwa maisha ukihangaika kumbe yanawezekana,” anasema Aurelia.

Naye Yuditha Mkane (52), Mkazi wa Kijiji cha Msetule, Halmashauri ya Mji wa Makambako, Njombe, anasema anaweza kuandika historia ya maisha kutokana na ugumu wa maisha aliyopitia hapo awali na jinsi walivyopambana kuhakikisha familia haiteteleki na watoto wanapata haki zao za msingi ikiwamo elimu.

Yuditha anasema aliolewa  na mwanamume mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, aliyefariki mwaka 2004 na kumwachiwa watoto wanne wakiwa wadogo hawajaanza hata shule.

Anasema tangu afiwe na muewe alianza kuishi maishi ya kutangatanga na kulala porini kwa sababu ya kukosa mahitaji muhimu ya kijamii ikiwamo chakula na malazi.

“Kwa mara ya kwanza nilijikuta nachanganyikiwa kwa sababu sikuwa na mtaji wala hakuna ndugu aliyeweza kunishika mkono hasa ukizingatia kuwa mume wangu kwao alizaliwa peke yake.

“Hali hiyo ilisababisha nianze kufanya vibarua kwenye mashamba ya watu kila kukicha ili nipate angalau fedha ya kula na watoto,” anasema Yuditha.

Anaongeza kuwa ilipofika mwaka 2015 akaona fursa katika Mfuko wa Tasaf ambao walikuwa wakiwezesha kaya maskini na ndipo alipojitosa kuomba mkopo wa kuku na kuanza shughuli za ufufugaji, ambayo imemsaidia kujenga nyumba pamoja na kusomesha watoto wake.

Yuditha anamshukuru Mungu kwa sasa ameweza kujenga nyumba na watoto wake wengine wamekuwa wakubwa wanaweza kujimudu wao wenyewe.

Anasema alipitia changamoto ambazo zilimkatisha tamaa lakini aliinuka na kusonga mbele hivyo, anawatia moyo wanawake wengine kutokukata tamaa pindi wanapokumbwa na matatizo mbalimbali.

Anaiomba Serikali ijitahidi kuendelea kuziwezesha jamii hasa za vijijini kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu na elimu ya ujasiriamali ili waweze kujikomboa katika hali duni inayowakabili.

Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi ya TASAF Halmashauri ya Mji wa Njombe, Edwin Mlowe, anasema ni vema jamii ikajenga mazoea ya kutokukata tamaa ili iweze kujikwamua.

Anasema wanawake hao ni miongoni mwa wanawake ambao unaweza ukajifunza mengi kutoka kwao kwa sababu ya kujishughulisha na ufugaji kupitia mradi walionufaika nao wa TASAF. 

“Wanawake hawa unaweza ukajifunza kitu kutoka kwao kwa sababu awali walikuwa wamekata tamaa ya kimaisha lakini kwa sasa wanafurahia maisha yao na kuwa mfano kwa wengine  kwa sababu ya kujiamini na kutokata tamaa,” anasema Mlowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles