Na Shermarx Ngahemera
TANZANITE ni mwiba kwa masuala ya madini Tanzania na ina umaarufu wa kipekee kwa sababu madini hayo ya vito yanapatikana nchini pekee na hivyo kubeba mnyambuliko wa jina la nchi.
Ni fahari na heshima kwa nchi lakini ni aghalabu kukuta Watanzania wa kawaida wanayajua madini hayo yalivyo na hivyo kukosa ulinzi wa kwanza kutoka kwa wananchi wenyewe. Ni aibu kubwa na Serikali inabidi ifanye juhudi kurekebisha kasoro hiyo ya wazi.
Kama nchi Tanzania inahitaji kufanya marekebisho mengi ili eneo hilo la Kata ya Naisinyai linalotajwa kuwa na Tanzanite nyingi lakini cha ajabu nchi nyingine hasa Kenya, Afrika Kusini na India ndizo zinaendelea kunufaika huku Serikali ikipata asilimia tano tu inayotokana na madini hayo kama mrahaba wakati rasilimali ni yake. Kwanini ile rojo badala ya dikodiko?
Tokea ugunduzi wa madini hayo miaka ya sabini na Juma Ngoma wa Makanya watu wengi wamewahi kukamatwa na wengine kufungwa au kupoteza maisha katika awamu zote tano za utawala wa nchi yetu na hivyo kuendelea kuwa maarufu kwa mema na mabaya.
Kuna watu wengi wana kesi mahakamani na mauaji mengi yametokea chanzo kikiwa tanzanite. Tukubaliane na hali hiyo kwani Waingereza wanaamini kuwa palipo na hazina hapakosi uhalifu, vitu hivi hutangamana kwani Mirerani na vitongoji vyake vimeshamiri uhalifu na dhuluma ya kila namna.
Msimamo huo anao hata Rais Magufuli na aliuelezea kwa kina alipokuwepo kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro eneo la mji mdogo wa Mirerani katika ufunguzi wa barabara ya lami ya urefu wa kilomita 26 kuelekea eneo hilo la utajiri mkubwa wa madini ya tanzanite na vito vingine vya sapphire, green tourmaline na graphite kwani kabla ya tanzanite (zoisite kwa jina lake la kikemikali) eneo hilo lilikuwa muhimu kwa uchimbaji wa ‘graphite’ kama koti la kufichia mali.
Akiwepo Naisinyai Rais Magufuli pia aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwaachia wawekezaji ‘wenye umuhimu’ katika migodi ya Tanzanite ili wakakae na kamati ya kujadili madini chini ya Waziri wa Sheria na Katiba kurekebisha mkataba uliopo uwe na faida kwa Serikali na si wa kiunyonyaji pekee.
Wawekezaji hao walikamatwa hivi karibuni kwa ajili ya kusaidia kutoa taarifa nyeti kuhusu madini ya Tanzanite na Kampuni ya Tanzanite One ambayo baadaye ilionekana hata usajili wa kampuni yao ulitiliwa shaka.
Rais Magufuli hakumung’unya maneno pale aliposema kinagaubaga kuwa wizi umetamalaki kwenye biashara na uchimbaji wa Tanzanite.
“Sina sababu ya kumung’unya maneno, madini ya Tanzanite yanaibwa sana, ni shamba la bibi; tena la mabibi waliokufa miaka mingi kama vile hakuna mwenyewe,” alisisitiza.
“Watu wanachukua kuliko hata shamba la bibi. Mgodini kuna wawekezaji wameingia ubia na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kila mtu ana asilimia 50, lakini bado mali inasombwa na Serikali kugeuzwa kuwa mtazamaji,” alisema Magufuli kwa masikitiko na kushangaa njama na hujuma hizo.
Kutokana na hujuma inayofanyika kwenye Tanzanite, Wakurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One, Faisal Juma na Hussein Gonga, wanaochimba Tanzanite kwa ubia na Stamico, walikamatwa kwa mahojiano ikiwa ni siku chache tangu Kamati ya Bunge itoe taarifa yake ya uchunguzi wa madini hayo na yale ya almasi iliyosomwa mbele ya Rais Dk. Magufuli, Ikulu Dar es Salaam ambayo iliibua uozo na hujuma nyingi katika mwenendo mzima wa madini hayo mawili unaofanana na ule wa makinikia ya Acacia.
Karibu wadau wote walionekana kuihujumu Serikali kwa namna moja au nyingine. Alitoa wito kwa vyombo husika ikiwamo Stamico. Benki Kuu, wawekezaji na vyombo vya ulinzi na usalama kuanzisha mustakabali mpya wa utendaji kazi kuinufaisha Serikali na jamii yote kwa ujumla.
Stamico iliyolazwa
Akielezea ushiriki wa shirika hilo kusimamia madini ya tanzanite kwa kufanya biashara badala yake kama mwakilishi na hivyo mbia kwa Tanzanite One, Rais Magufuli aliagiza watu walioshiriki kufanya mambo ya ovyo waondolewe mara moja kwani waliingia njama na upande mwingine kuidhulumu Serikali kwa kutokuwa makini na kuanza kujinufaisha wao binafsi.
Rais alisema kama Taifa inabidi kujipanga upya na vizuri. Akaagiza vyombo vya ulinzi, polisi na usalama kuwa vihakikishe madini ya Tanzanite haivushwi kinyemela na ovyo ovyo ila kuwashughulikia wote wanaoendesha hujuma hiyo. Hayo yalisikika na kushuhudiwa mubashara kwenye redio na runinga zote nchini.
“Atakayetoka na Tanzanite kwenda nje ya nchi iwe halali amelipia kila kitu na aende zake salama na apewe vibali sahihi.” Alipambanua mustakabali wanchi na kudai mabadiliko.
“Tupokwenye vita kubwa ya kubadilisha hii nchi, tumechezewa mno na yale ninayoyaona kule Ikulu ni maajabu mengi. Ikumbukwe kuwa nilipoingia madarakani mnafahamu tulifanya nini watumishi, wanafunzi, tumekuta hewa,” alieleza Rais kwa masikitiko makubwa.
Benki Kuu
Kwa mara nyingine, aliiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutengeneza mkakati wa kushiriki ununuzi wa tanzanite kwa sababu madini hayo si rahisi kudanganya kama inavyoweza kufanywa kwenye dhahabu. Alitaka benki iwe macho kulinda rasilimali za taifa na si fedha tu kwa kuwa wabunifu kutambua na kubaini mianya ya upotevu wa mapato kama benki ya uwekezaji na sio ‘central bank pekee’. Ni benki inayotunza hazina ya serikali kwa maana ya fedha, vito na rasilimali muhimu na adimu za umma kwa faida ya umma wenyewe.
Wawekezaji
Rais Dk. Magufuli, alisema anawakaribisha wawekezaji kuja nchini na Serikali inawahitaji wawekezaji wenye nia njema na si wawekezaji wanaopanga kuiibia nchi na kujinufaisha wao pekee. Anataka faida kwa wote.
“Kama kutakuwa na mwekezaji anayetaka kuja nchini kutuibia basi huyo asije kabisa atakuwa amekula wa chuya kwani wakati huu hataiba bali atalia. Na hili nalisema kwa wazi, tumeamua kupambana kwa vita ya uchumi wa taifa letu.
“Nchi yetu ni tajiri, juzi tumekamata madini ya almasi yenye thamani ya fedha nyingi, kwenye madini ya dhahabu ndiyo usiombe ni uozo mtupu, ovyo,” alisema
Ujenzi wa ukuta
Katika mazingira yasiyotegemewa na wengi na kuonesha anakisimamia kile anachokisema na kuamini, Rais alifanya uamuzi mgumu wa kujenga ukuta kuzunguka eneo lote linalosadikiwa kuwa na madini hayo kam ule ukuta wa Kibiblia wa Jerusalem au ule Ukuta Mkuu wa China (The Great Wall).
Anataka biashara ya madini ya vito iwe rasmi kwa wahusika wote ili kujua nani anafanya nini na mapato hayo ili Serikali ipate kodi yake bila kutumia nguvu nyingi na kwa uhakika zaidi kwa kurasimisha mengi yanayohusu madini hayo. Mifumo ikiwa madhubuti na rasmi itawezesha upatikanaji mapato sadifu na ya kutosha .
Kama Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Tanzania akaliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia kuisimamia SUMA JKT kuanza haraka ujenzi wa ukuta katika eneo lote la uchimbaji wa Tanzanite kutoka vitalu A mpaka D, lenye eneo la kilomita za mraba 81.99. Baada ya siku tatu wanajeshi wakafika na kupiga kambi eneo husika na kuendelea na utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa ukuta kama Kamanda Mkuu alivyoamrsisha.
Wadadisi wa mambo wanataka tathmini sadifu ifanyike kwenye madini hayo isije ikawa yale ya ‘rhodolite’ kujirudia ambayo ilikuwa adimu na haipatikani lakini baadaye Brazil ikagundua machimbo kwa uwingi ambayo yakafanya madini hayo kukosa thamani. Malkia Elizabeth aliyatumia madini hayo na kuweka mbele ya taji lake (crown) kitu ambacho sasa anakiona kuwa dhalili na kupunguza thamani halisi ya taji lake.
Kwa vile Tanzanite ina historia fupi isije ikatokea kama ilivyotokea kama kwa ‘rhodolite’ iliposhuka thamani yake na kufanya uwekezaji wa ukuta kuonekana kuwa hatukuwa makini katika kushughulikia kikamilifu suala hilo muhimu kiuchumi.
Rais Magufuli aliyeonekana kuumizwa na hujuma ya wizi wa Tanzanite, alisema ameona ni vema kuanza na hatua hiyo huku akiwa na matumaini kuwa mwekezaji wa Tanzanite One na wawekezaji wengine watakaa na Serikali kutengeneza mkataba mwingine wenye faida kwa pande zote mbili zinazohusika.
Suala hili ni kuntu baada ya Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni Waziri wa Sheria na Katiba kukamilisha mazungumzo ya mapitio ya mikataba ya madini yenye mafanikio makubwa kwa nchi kuhusu suala zima la madini na makinikia.
Rais anataka mkataba mpya kwa uchimbaji wa Tanzanite ili wadau wawajibike vilivyo.
“Wapitie kwa pamoja mkataba huu waurekebishe wasaini upya ili asilimia kubwa ya fedha zibakie hapa. Fedha hizo zitakapopatikana tuanze mpango wa kuweka maji na miundombinu mingine ya umma ya uhakika hapa Simanjiro.” Alisisitiza kutokea mabadiliko katika mahusiano na mali hiyo kunufaisha zaidi wanyonge.
“Nimesema hapana, ndani ya mamlaka yangu lazima tujipange vizuri. Hili suala naona linafikia mwisho, tumechezewa vya kutosha. Najua kulikuwa na watu wanafaidika, biashara ya Tanzanite haijazuiliwa bali tunaitoa kwenye magendo na kuwa biashara halali.
Simanjiro vs Arusha
Arusha ni tanzanite na tanzanite ni Arusha, ni msemo ambao Rais anataka kufanyia mabadiliko na badala yake iwe Simanjiro ni tanzanite.
“Nataka Tanzanite iwe halali na si haramu, wachimbaji wadogo chimbeni, ukipata mali yako ukiwa ndani ya uzio kauze unavyotaka. “Tunataka soko la Tanzanite liwe Simanjiro si Arusha, wanaotoka Marekani na India waje wanunue hapa, akishuka na ndege hapo KIA aje kwa gari hapa anunue Tanzanite akauze anakojua,” alisema.
Dhana ya Arusha kama Blue City ikiwa na maana ya rangi ya tanzanite inabidi ipitiwe upya kwani kwa muda mrefu watu wa Simanjiro wamenyonywa na wale wa Arusha wakati madini hayo ni mali hayo na kuamrisha minada ifanyike Mirerani na kuipa Mirerani hadhi ya Mji wa uwekezaji wa EPZA na kutaka Wizara husika kutekeleza yanayotakiwa kufanifanikisha maamuzi hayo ili haki itendeke kwa watu wa Mirerani.
Alishangazwa na kitendo cha kuona mji wa Mirerani uko nyuma kimaendeleo ya mengi wakati ndio eneo mama kwa madini adimu ya tanzanite ambayo duniani yanapatikana katika Kata hiyo tu. Aliingiza matakwa ya Mungu kwa suala hilo akiuliza na kutoa majibu mwenyewe.
“Hivi ni kwa nini Mungu atupe Tanzanite sisi peke yetu halafu hata gari la wagonjwa hamna? Hiyo gari nitawaletea mimi, na kuhusu suala la maji hilo pia niachieni nalifanyia kazi,” alisema Magufuli.
Viongozi waliokuwepo akiwamo Mbunge Millya aliyepewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo pamoja na wabunge wengine kutoka mikoa ya Manyara na Arusha, walimuomba Rais Magufuli kuhakikisha anaacha alama ya uongozi wake katika maisha ya wananchi wa Simanjiro.
“Nawashukuru kwa kumchagua Millya, ni mchapakazi amelelewa na CCM…ukimwona sura yake ni kama Chadema lakini moyo wake ni CCM kabisa,” alisema Magufuli huku akisisitiza kwamba ujenzi wa ukuta Mirerani utakuwa na kamera (CCTV) na vifaa maalumu vya kubaini wizi wa madini hayo.
Magufuli alisema kutakuwa na mlango mmoja wa kuingilia ili kudhibiti utoroshaji. “Hata ukimeza Tanzanite tumboni au kuficha kwenye viatu, itaonekana. Ndugu zangu viongozi waliopewa mamlaka ya kusimamia rasilimali hizi kama wangezisimamia vizuri leo hii Watanzania wasingekuwa masikini.”
Alishangaa kwa ufisadi kutawala maeneo mengi ya utendaji kazi.
“Kubwa linafanyika kwa sisi viongozi tunaopewa mamlaka ya kusimamia tunakuwa sehemu ya mafisadi wa kuwaumiza Watanzania masikini, viongozi tunasahau tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Tanzanite hii haitakaa miaka yote, katika uongozi wangu nimeamua kuiongoza hii vita.”