27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yaupa kisogo Umoja wa Ulaya

Balozi Dk. Aziz Mlima
Balozi Dk. Aziz Mlima

Na Harrieth Mandari,

SERIKALI ya Tanzania imesita kusaini majadiliano ya mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi (EPA) baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU).

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwapo hali ya sintofahamu ndani ya EU baada ya wananchi wa Uingereza kupiga kura ya kujiondoa kwenye umoja huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kikanda na Afrika Mashariki, Balozi Dk. Aziz Mlima, alisema dhamira kuu ya Serikali ni kujenga uchumi wa viwanda na biashara na kwamba makubaliano hayalisaidii taifa kiuchumi.

Dk. Mlima alisema imebainika kuwa makubaliano hayo yanaweza kuwa na madhara ya kiuchumi kwa nchi changa ambazo zimegeuzwa soko la bidhaa za mataifa yaliyoendelea.

“Nia na madhumuni yetu ni kuwa nchi iliyoendelea kiuchumi kwa kuwa na viwanda vyetu vya kisasa ambavyo vitaleta maendeleo kiuchumi,” alisema Dk. Mlima.

Hata hivyo, alisema msimamo wa nchi nyingine wanachama wa EAC kuhusu makubaliano haujafahamika.

Juni 23 mwaka huu Uingereza ilijitoa EU hatua iliyoibua hofu kwa baadhi ya wadau wa uchumi nchini lakini Dk. Mlima jana alieleza kuwa bado hakuna takwimu za athari za kujiondoa kwa Uingereza ndani ya umoja huo kwa sababu muda bado ni mfupi kufanyia utafiti.

“Kwa sasa ni muda mfupi sana kutathmini iwapo kuna athari yoyote kiuchumi kwa upande wa Tanzania kwa sababu ni kama wiki mbili tu tangu taarifa hiyo ya kujitoa ilipotangazwa,” alisema Dk. Mlima.

Wakati Tanzania ikichukua msimamo huo, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta wiki iliyopita alikaririwa akieleza kuwa nchi yake inaunga mkono uamuzi wa Uingereza kujiondoa EU.

Kwa mujibu wa jarida la The Star linalochapishwa nchini Kenya lililokariri taarifa ya Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta alisema wataendelea kudumisha uhusiano wa kihistoria wa nchi yake na Uingereza huku pia Serikali yake ikiendelea kushirikiana na EU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles