23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yatoa kauli vurugu Afrika Kusini

Asha Bani -Dar es salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amesikitishwa na hali ya machafuko inayoendelea nchini Afrika Kusini na kusababisha vifo vya watu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kabudi alisema hali inayoendelea kwa sasa haiwezi kueleweka na mtu yeyote bila ya kuwa na uelewa wa historia ya nchi hiyo.

Alisema Afrika Kusini ni nchi ambayo kwa kipindi kirefu walinyimwa haki zao kwa kuwa chini ya ubaguzi wa rangi, ardhi yao ilichukuliwa na kuwa mikononi mwa raia fulani wa nchi hiyo na hata kusababisha wengi kukosa kazi na ajira.

“Hivyo basi hayo yanayoendelea kwa sasa Afrika Kusini  yanaweza kuwa ni visababishi vya hayo ambayo yalikuwa na historia na kushabihiana na yanatokea kwa sasa.

 “Sisi Watanzania mara nyingi sana tunasahau au kujisahaulisha, tunajibeza na kujidharau au tunafifisha mafaniko yetu.

“Tumshukuru sana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mwaka 1961 nchi hii inapata uhuru hakukuwa na mgawanyiko, lilikuwa ni  taifa moja  lenye mkusanyiko wa makabila.

“Na leo Mwalimu (Julius Nyerere), ameifanya nchi hii kufanikiwa kuwa taifa moja na sisi sote hapa tunajiona Watanzania,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema  Afrika Kusini imekuwa na historia ya bahati mbaya, kwamba kwa kipindi kirefu Waafrika walibaguliwa, walinyang’anywa ardhi yao na wengine hadi leo wengi hawana ardhi na hata kukosa ajira.

Aliongeza kuwa katika hali hiyo ya kukata tamaa au ya kuchanganyikiwa, wapo ambao wamechukia na kulaani kwamba waliosababisha hali hiyo ni Waafrika wengine waliokwenda Afrika Kusini baada ya nchi hiyo  kukombolewa, ukombozi ambao pia ni mchango wa nchi nyingi za Afrika, Tanzania ikiwa ni mojawapo.

“Lakini katika suala hili lililotokea, Watanzania wamemsikia Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amekemea na kulaani vikali vitendo vilivyotokea vya baadhi ya raia wa Afrika Kusini kuwashambulia raia wengine wa nchi za Afrika waliopo nchini humo kwa madai kwamba wamechukua kazi zao na baadhi yao shughuli zao za biashara kuvurugwa.

“Rais Ramaphosa hakukaa kimya, alisimama hadharani na kulihutubia taifa hilo kwenye televisheni na vyombo vingine, pia amelaani kitendo hicho na kukemea, amesema asilani sio kitendo ambacho Serikali na watu wa Afrika Kusini watavumilia,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema Tanzania inaunga mkono matamshi hayo ya Rais Ramaphosa ya kulaani na kukemea vikali vitendo hivyo.

Profesa Kabudi alisema Serikali ya Tanzania inaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu na Serikali ya Afrika Kusini na kumpa moyo Rais Ramaphosa katika kauli zake na hatua alizochukua za kukabiliana na kitendo hicho.

Alizungumzia hali ya wananchi wa Tanzania waishio nchini humo kwamba hadi sasa hakuna aliyeuawa na endapo atapata taarifa hizo ataeleza.

Pia alisema wananchi wa Afrika Kusini wanatakiwa kuelewa kuwa adui yao si Waafrika wenzao bali ni ubaguzi wa rangi  uliokuwepo katika kipindi hicho.

Alisema kwa sasa ni wakati wa Waafrika Kusini kukaa chini, kutafakari na kuelewa kwamba hali waliyonayo haichangiwi na Waafrika bali ni mfumo wa uchumi ambao awali ulikuwa katika ubaguzi wa rangi.

“Sisi Watanzania tulitoa mchango wetu kwa hali na mali kuhakikisha wanapata uhuru, lakini si kwamba wana deni kwetu, hapana, deni walilonalo wao wanatakiwa kuwalipa wananchi wote wanaoishi nchini humo ambao ni Waafrika,’’ alisema Profesa Kabudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles