25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA YATAKA KUWA KINARA UZALISHAJI SARUJI

 

Na Amina Omari-Tanga

TANZANIA ipo katika mkakati wa kuhakikisha inakuwa kinara wa uzalishaji wa saruji katika nchi zilizoko chini ya Jangwa la Sahara kutokana  na uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda hivyo unaoendelea kwa sasa.

Kutokana na uwekezaji huo mkubwa  nchini, viwanda vinatarajiwa kuongeza  uzalishaji  maradufu kutoka tani milioni 10.8 za sasa  hadi kufikia tani  milioni 20 kwa mwaka.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, akiwa katika ziara ya kikazi  mkoani Tanga  hivi karibuni, ameeleza mikakati  hiyo  ya Serikali katika kufanikisha azma ya sera ya viwanda katika kuchochea uchumi wa  nchi.

Amesema kwa hatua hiyo ya uwekezaji inaonyesha ni namna gani Serikali imedhamiria kuwekeza kwenye uchumi wa viwanda ili kuhakikisha lengo la uchumi wa kati linafikiwa mwaka 2025.

Anafafanua kuwa kwa sasa hapa nchini kuna viwanda vya kuzalisha saruji  takribani 11 ambavyo vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.8 wakati hitaji  halisi la nchini pekee ni tani milioni 4.7 kwa mwaka.

Anasema kuongezeka kwa uwezo wa uzalishaji wa tani za ziada umelenga  katika kuhakikisha wanayateka masoko yaliyoko katika nchi za Afrika
pamoja na Arabuni.

“Mikakati yetu ni kuhakikisha tunajikita katika ujenzi wa viwanda vya  kuzalishaji bidhaa za saruji, bati na nondo kwa ajili ya masoko ya  ndani ya nchi na kuuza nchi za nje.

Mwijage anasema kwa Mkoa wa Tanga unatarajiwa kupata uwekezaji mkubwa wa ujenzi  wa kiwanda kikubwa cha saruji kutoka Kampuni ya Kichina ya  Sinoma na Kampuni ya Hengya Cement (T) Ltd.
Waziri Mwijage anasema kampuni hiyo inatarajiwa kuzalisha  tani milioni  3 kwa mwaka wakiwa  wamelenga kuuza bidhaa yao katika masoko yao  makubwa duniani.
Amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni fursa kubwa kwa sababu utaenda  sambamba na ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima – Tanga na kwamba  saruji ambayo itatengenezwa itapata soko la uhakika.

Amesema licha ya  mkoa huo kuwa na viwanda vingine vya saruji, bado  mahitaji ya saruji nchini ni makubwa na kwamba ongezeko la viwanda litapaswa lisaidie kushusha bei ya saruji.

“Tunahitaji kuwa na viwanda vingi zaidi ili bei ya mfuko wa saruji  ishuke na wananchi wa kawaida  waweze kumudu bei na kuweza kununua kwa  kwa ajili ya kujenga nyumba za kisasa,” amesema Waziri huyo.

Vile vile anasema kuwa  kuendelea kuwepo kwa viwanda vingi katika mkoa  huo ni tija kwa nchi, kwani mkoa huo ulikuwa na viwanda vingi kama ilivyo kwa Dar es Salaam na Morogoro, lakini vikafa kutokana na  mabadiliko ya teknolojia na kwa vile wenye viwanda hawakuwa tayari
kuendana na kasi hiyo ya mabadiliko.

“Wawekezaji wa sasa wako tayari kwenda na teknolojia ya kisasa kwa  hiyo Watanzania wawe tayari kuwapokea wawekezaji ili tushirikiane nao  kukuza uchumi wetu na Tanzania itoke hapa ilipo na kwenda kwenye  uchumi wa kati,” amesema.

Licha ya kuongezeka kwa uzalishaji huo, Mwijage anasema malengo ya Tanzania ni kuhakikisha bidhaa ya saruji inayozalishwa hapa nchini  inawafikia wateja kwa haraka na gharama nafuu.

“Kwa sasa Serikali inaendelea kujiimarisha kimiundombinu kwa kufanya  upanuzi wa bandari zetu, kurekebisha miundombinu ya reli na barabara  ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa viwandani,” anasema  Waziri huyo.

Kwa upande wake, Ofisa Uzalishaji wa Kiwanda cha Saruji cha  Kilimanjaro, Hashim Hafidhi, anasema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.8 kwa mwaka  ambapo kiwanda hicho kimejikita katika uzalishaji wa saruji kwa ajili  ya matumizi ya kawaida ya kujengea pamoja na saruji maalumu kwa ajili  ya ujenzi wa barabara,  madaraja pamoja na majengo makubwa.

Hata hivyo, anasema  kwa sasa soko kuu la bidhaa yao  lipo nchini  wakati wakiendelea kufanya mazungumzo katika masoko ya nje ya nchi ili  waweze kuona namna nzuri ya kuyafikia masoko hayo.

“Tunatarajia  kutumia Bahari ya Hindi kusafirisha saruji yetu kwenda  Somalia, Kenya na Msumbiji, lakini pia ziko nchi za Sudan, DRC na  Uganda ambao wako tayari kuchukua saruji tutakayozalisha.”

Licha ya mafanikio hayo ya uanzishwaji wa viwanda, lakini uingiaji wa  saruji kutoka nje kwa njia ya magendo imekuwa ni  sugu na ni kilio cha muda kwa  wamiliki wa viwanda vya saruji hapa nchini.

Hafidhi anasema changamoto hiyo imekuwa ikiathiri kwa  kiasi kikubwa soko lao na kusababisha ushindani kuwa mkubwa sokoni kutokana  na saruji ya magendo kuuzwa kwa bei ya chini zaidi kwani hawalipi kodi.

“Serikali tunaomba ione namna bora ya kudhibiti uingiaji wa saruji kutoka nje ya nchi kwani unaathiri soko la ndani kwa kiasi kikubwa na  kudidimiza uchumi wa viwanda,” anabainisha Hafidhi.

Kiwanda cha Saruji cha Tanga ni moja ya kiwanda kikongwe cha  kuzalisha saruji hapa nchini ambapo kwa upande wao wamegusia  changamoto ya  miundombinu katika usafirishaji wa bidhaa  wanazozalisha.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Saruji Tanga, Reinhardt Swart, ameishauri Serikali  kuboresha miundombinu ya  reli na bandari ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa  hapa nchini.

Amesema ili sera ya viwanda iweze kutekelezeka kwa vitendo, Serikali ni vema ingewekeza nguvu nyingi katika uboreshaji wa  miundombinu ya bandari na reli ili kurahisisha usafirishaji wa  malighafi pamoja na bidhaa.

Amesema wazalishaji wanalazimika kutumia gharama kubwa  katika usafirishaji wa mizigo yao kwa kutumia njia ya barabara ambayo  ina changamoto nyingi ikiwemo ajali pamoja na uharibifu wa barabara.

“Serikali ione umuhimu wa kuboresha bandari zetu kwani mizigo mingi  itaweza kupita huko pamoja na  reli inaweza kubeba shehena kubwa za mizigo,  kama kuna uwezekano Serikali ingepeleka reli katika  maeneo ambayo hayana miundombinu hiyo,” amesema Swart.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesema katika kuhakikisha  wanakabiliana na ushindani wa ujio wa viwanda vya saruji jijini Tanga, watahakikisha wanazalisha bidhaa zao kwa ubora na ufanisi mkubwa.

Ujio wa viwanda vipya

Mkurugenzi Swart anasema katika fursa ya biashara ya viwanda huwezi kutegemea kiwanda kimoja pekee kwa ajili ya uzalishaji kuweza  kukidhi  mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi pekee.

Anasema kuwa kutokana na mapinduzi ya viwanda sambamba na teknolojia  kukua, walitegemea uwepo wa ushindani wa kibiashara katika bidhaa hiyo,
hivyo wapo tayari kwa ajili ya  kuendelea kujiimarisha kiuzalishaji
zaidi.

“Hatutishwi na ujio wa viwanda vipya bali tutahakikisha tunalinda  ubora wa bidhaa zetu  na ziwe zenye viwango madhubuti muda  wote,” anaongeza Mkurugenzi huyo.

Anasema ubora wa bidhaa zao ndio kitambulisho pekee ambacho  wataendelea kuhakikisha wanakilinda ikiwemo kudhibiti bei ya bidhaa  zao, kwa kuhakikisha ile imani waliyopewa na wananchi inaendelea  kudumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles