27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA YATAKA KUONGOZA SOKO LA SARUJI

Saruji kutoka Dangote Mtwara.
Saruji kutoka Dangote Mtwara.

Na Joseph Lino,

TANZANIA ina mipango kabambe ya kuzalisha saruji ambayo itaifanya iwe mzalishaji namba moja eneo hili la Afrika Mashariki kama mipango itaenda kama ilivyopangwa na wawekezaji.

Uzalishaji wa Tanzania unatarajia kuongezeka na kuwa mzalishaji mkubwa wa saruji kufikia tani milioni 17 kwa mwaka kutokana na makampuni mapya matatu ambayo yameomba kuwekeza katika sekta hii yenye uhakika wa faida na mahitaji yanayokuwa kila siku kutokana na mahitaji ya madai ya maendeleo na ujenzi wa uchumi.

Kampuni zimepanga kuwekeza kiasi cha Sh trilioni 20 katika miaka michache ijayo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema hayo hivi karibuni katika maonyesho ya kwanza ya viwanda yaliyofanyika wiki iliyopita.

Kampuni hizo ambazo ni EAM, Mamba na Sungura, alisema kuwa EAM imeomba kujenga kiwanda kitakachozalisha tani milioni tatu mkoani Tanga.

“Mwekezaji ana uwezo wa kuzalisha tani milioni saba kama Serikali itamkubalia kuuza nje saruji ambayo wizara tumekubali lakini bado mambo mengine yanahitaji kuwekwa sawa na wazi.”

Waziri alisema Serikali imedhamiria katika uanzishwaji uchumi wa viwanda na hivyo inakaribisha wawekezaji zaidi nchini kutoka duniani kote.

Mwijage aliendelea kusema kampuni za Mamba na Sungura pia zimeonesha nia ya kuwekeza nchini na mazungumzo kati ya Serikali na wawekezaji hao yanaendelea.

Wawekezaji wengine katika sekta ya saruji nchini ni Twiga, Simba, Tembo, Nyati na Ngamia  ambao kwa pamoja wana uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.3, ikimaanisha kwamba wazalishaji wa sasa na ambao huzalisha kwa uwezo wao, ukijumuisha uzalishaji wa EAM wa tani milioni 3, itafikia zaidi ya tani milioni 17.

Dangote Cement Company ni mwekezaji mwingine  mkubwa ambaye shughuli ya uzalishaji ilisitishwa juu ya masuala ya kiufundi na hivi karibuni atarudisha uzalishaji uliokwama. Pamoja na  tani milioni tatu anayozalisha Dangote Cement ndiye mzalishaji mkubwa nchini  na Afrika Mashariki yote hadi Ethiopia.

Kuna Kampuni ya China inayoitwa Hengya Cement imepanga kuzalisha tani milioni 3 kule Tanga na imepanga kuwekeza dola bilioni 3 kwa maelezo ya Clifford Tandari Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na hivyo kuwa moja wa wawekezaji wakubwa hapa nchini.

Mwijage alisema Tanzania ina uwezo hadi sasa wa kuzalisha tani milioni 10.3 za saruji na tani milioni saba zikatumika nyumbani.

Mahitaji ya nchi juu ya saruji kwa mujibu wa waziri, ni tani milioni 10.3.

Mwenendo viwanda vya saruji

Viwanda vya saruji vinachukuwa sura na mwenendo mpya kutokana na kuongezeka kwa ushindani unaotokana na kuongezeka kwa wazalishaji. Hivi basi soko lililopo linabadilika kimwelekeo kutoka lile la wauzaji na kuwa la walaji.

“Kuanzia mwaka huu na kuendelea biashara inategemewa kujaa mikwara mingi na kwa miaka inayofuata,” anasema Ekwabi Majigo Mtafiti wa masuala ya saruji nchini.

Majigo anasema katika ripoti yake ya Mei mwaka huu kuwa takwimu zilizozoeleka za utengenezaji / upatikanaji saruji nchini Tanzania kwa mwaka huu ni tani milioni 8.7 wakati mahitaji ya walaji halisi ni tani milioni 4.1 na ongezeko la mahitaji kila mwaka ni asilimia 10 hadi 12 ukizingatia mahitaji ya miaka minne mfululizo hadi mwaka jana.

“Inavyoonekana ni kuwa kuna uzalishaji wa ziada lakini haujioneshi kwenye soko na hivyo kuleta shaka kuwa saruji nyingi inauzwa kimagendo nchini na hivyo kutia wasiwasi wa ukubwa na uwezo wa soko,” anasema Majigo.

“Mtazamo wa soko ni kuwa kama itaendelea moja kwa moja ni kuwa bei itaanguka na hivyo wazalishaji saruji wanahitaji kujizatiti ili waendelee kuwepo sokoni na hivyo mtazamo wa Tanzania kuongeza uzalishaji ni sahihi kwani anayeongoza soko ndiye anayepanga bei.”

Hali hiyo tete itahitaji kuondokana na mikakati ya awali na mtazamo  wa kutumia majina na kuweko miaka mingi sokoni kwani sasa hivi wateja wanajali chapa na ubora wa ndani na kutupilia mbali wakongwe wa soko na hivyo kudai ubunifu katika soko hili linalokuwa.  

Mahali pa kiwanda

Viwanda vingi na bandari ya kuingiza na kutoa saruji nchini iko Dar es Salaam na hivyo itaathirika sana eneo hilo.  Inathibitisha kuwa kiwanda kilichoko Dar kina changamoto nyingi kutokana na ushindani ukifananisha na vile vya nje ya jiji hilo. Hata hivyo, ni Dar es Salaam ambayo ina soko la uhakika la asilimia 40 ya saruji inayopatikana nchini kimauzo.

Inakisiwa vinahitajika viwanda vidogo vidogo vya kuweka madaraja (grading ) na kuweka mifukoni saruji (packing), lakini wataalamu  wengine wanapinga  dhana hiyo kwa kusema kuwa kwa vile viwanda hivyo vidogo vina  gharama ndogo za uendeshaji vitahimili ushindani na kupambana na viwanda vikubwa kwa kuwa na muundo mdogo wa mfumo wa uendeshaji.

“Hawalipi kodi ya pango la nyumba au kiwanda na mishahara yao si ile ya wataalamu wa nje kama viwanda vikubwa vinavyofanya. Na hali hiyo inawezekana na hata kama watanunua ‘klinka’ ya kutengeneza saruji kutoka hapa hapa nchini kwani wao bajeti yao ni ndogo,” anasisitiza Majigo.

Kimahitaji Tanzania inahitaji saruji kuweza kushughulikia miradi yake mingi ikiwa mkubwa ni ule wa Reli ya Kati (SGR) na ule wa Reli ya Makambako  Mtwara, Upanuzi Bandari ya Mtwara, Bandari ya Bagamoyo, Ujenzi Bomba la  Mafuta Ghafi ya Uganda toka Hoima (Uganda) hadi bandari ya Tanga  Tanzania na barabara zinazojengwa pamoja na viwanja vya ndege nchi nzima kama Waziri Profesa Makame Mbarawa alivyoainisha.

Mpango wa taifa wa kufanya kuwa nchi ya viwanda unahitaji ujenzi wa miundombinu na saruji haina badala yake na hivyo mahitaji yanategemewa  kuongezeka kila wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles