22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA YA 14 KWA UNYWAJI POMBE AFRIKA – WHO

Na Said Salim –  dar es salaam


SHIRIKA la Afya la Kimataifa (WHO) limeitaja Tanzania kushika nafasi ya 14 katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa unywaji pombe barani Afrika kati ya nchi 46 zilizofanyiwa utafiti mwaka 2016.

Kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya hali ya kiafya kulingana na viashiria vya malengo endelevu ya milenia (SDG) ya mwaka jana, Tanzania ni ya nne miongoni mwa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati na ya 49 duniani.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa wakati wa utafiti huo, kiwango cha pombe halisi kinachonywewa na Mtanzania mmoja mmoja mwenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea, kilikuwa lita 6.3 kwa mwaka.

WHO imesema kuwa ripoti hiyo imeandaliwa kwa kutumia takwimu zinazozalishwa na kuhifadhiwa na shirika hilo au mashirika mengine ya kimataifa ambayo ni mwanachama.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Uganda ndiyo inayoshika nafasi ya kwanza ikiwa na wastani wa unywaji wa lita 11.8 kwa mtu mmoja mmoja kwa mwaka ikifuatiwa na Rwanda (lita 11.5), Burundi (6.9) na Kenya ni ya tano kwa lita 4.4.

Mbali ya kuongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na kiwango kikubwa cha unywaji pombe, Uganda pia imeshika nafasi ya kwanza Afrika na ya 11 duniani ikilingana na Namibia, huku Mauritania na Libya zikiwa na kiwango kidogo kuliko nchi zote duniani cha lita 0.1 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Lithuania ndiyo inayoongoza kwa kiwango cha unywaji pombe duniani, ikiwa na wastani wa lita 18.2 ikifuatiwa na Belarus lita 16.4, Jamhuri ya Maldova (lita 15.6) na Urusi lita 13.9.

Miongoni mwa nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi (MEDCs), Ujerumani inashika nafasi ya 15 duniani ikiwa na wastani wa lita 11.4, Denmark nafasi ya 23 (lita 10.1), Uswisi nafasi ya 24 sawa na Canada (lita 10.0), Marekani nafasi ya 27 (lita 9.3) na Uholanzi nafasi ya 33 (lita 8.7).

Akizungumzia na Mtanzania kuhusu takwimu hizo za WHO, Mtanzania anayefanya PHD ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Udaktari Tokyo cha Japan, Dk. Isaac Maro, alisema ingawa kiwango cha unywaji pombe kwa Tanzania kimeonekana kuwa ni kidogo kuliko nchi nyingi za Afrika Mashariki, bado ni kikubwa kwa wastani, hivyo kinapaswa kupunguzwa ikizingatiwa kuwa pombe ni hatari kwa afya ya binadamu.

“Unywaji wa pombe uliokithiri unatambulika kuwa moja ya sababu ya maradhi mengi yasiyo ya kuambukiza kama vile maradhi ya mfumo wa damu (shinikizo la juu la damu na maradhi ya moyo) pamoja na maradhi ya mifumo kama vile kisukari.

“Takwimu hizo zimeonyesha kuongezeka kwa kiwango cha maradhi haya miongoni mwa Watanzania ambapo Watanzania 33,064,128 walionekana kuhitaji ushauri au matibabu dhidi ya maradhi yasiyo ya kuambukiza kwa mwaka 2015.

“Utafiti huo pia ulionyesha kuwa uwezekano wa kufariki kutokana na maradhi yasiyo ya kuambukizwa pamoja na saratani kwa Watanzania walio na umri wa kati ya miaka 30 na 70 ulikuwa asilimia 17.8 kwa mwaka 2016,” alisema Dk. Maro anayefanya kipindi cha Afya Check na Clouds Media.

Machi 15, 2016, Rais Dk. John Magufuli wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa wapya, aliwataka viongozi hao  kuhakikisha vijana wanaacha vitendo vya unywaji pombe, mchezo wa pool na michezo mingine wakati wa saa za kazi kama mkakati wa kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki shughuli ya uzalishaji mali katika eneo lake.

Kauli hiyo ya Magufuli iliungwa mkono na wakuu wa mikoa mbalimbali kwa kuendesha operesheni za kuwakamata watu waliokuwa wakinywa pombe saa za kazi na kuwachukulia hatua za kisheria.

Katika kupunguza matumizi ya pombe nchini, Februari 16, mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza amri ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashiwa pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’ kuanzia Machi mosi, mwaka jana.

“Sasa hivi viroba vimeenea kila kona, hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye,” alisema.

Majaliwa alikuwa akikazia kauli ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla, aliyoitoa bungeni mjini Dodoma Februari 7, mwaka jana.

Katika mkutano huo wa Bunge, wakati akijibu hoja za wabunge waliokuwa wakilalamikia kilevi hicho kinavyopunguza nguvu kazi ya Taifa, Dk. Kigwangalla alisema Serikali iliamua kupiga marufuku kutengenezwa au kuingizwa nchini kwa viroba pamoja na kuziba mianya yote ya uingizaji wa kilevi hicho kwa sababu kilikuwa kikiharibu nguvu kazi ya Taifa.

Miongoni mwa wabunge waliolalamikia viroba ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko ambaye alilieleza Bunge kuwa pombe hiyo inasababisha vifo vya vijana wengi nchini ambao ndio tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa.

“Katika kipindi hiki kifupi cha likizo yangu, nilikuwa jimboni kwangu na tumezika vijana wanne waliofariki kwa matumizi ya viroba.

“Hivyo wananchi wa jimbo langu wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari za pombe hiyo ili tuweze kujadili na kuona namna gani ya kuliokoa Taifa, hasa vijana kutoka katika janga hilo,” alifafanua Matiko.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles