33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania kupata umeme kutoka Ethiopia

power

Na Mwandishi wetu,

Umeme ni kani inayotakiwa katika mahitaji ya kuwa na ufanisi katika uchumi  wa viwanda ambao hutumia sana nishati hiyo kuendesha mitambo na utengenezaji wa bidhaa na kila nchi inafanya juhudi ili kuwanayo ya kutosha.

Tanzania na nchi nyingine za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) hivi karibuni zitakutana mjini Arusha na kutia saini mkataba mkubwa wa kuunganisha nchi hizo na chanzo cha umeme kutoka Ethiopia.

Kutokana na mkataba huo azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda itafikiwa mapema kwani wengi waliotaka kuanzisha viwanda nchini walisongwa na wazo la kukosekana umeme wa uhakika.

Mkurugenzi wa Tanesco Injinia Felchesmi Mramba aliviambia vyombo vya habari nchini kuwa Tanzania inafanya mapitio ya mkataba wa kuwezesha kupata na kununua umeme wa megawati 400 kutoka Ethiopia ambao utaunganishwa kwenye gridi ya Taifa kutegemea na mhitaji.

Mamlaka ya Umeme ya Ethiopia**** imethibitisha kuweko mpango huu na kusema nchi hiyo inayo uwezo wa kutekeleza mahitaji hayo kwani ina ziada ya umeme na inaendelea kuwekeza kwenye sekta hiyo ili iweze kuwa zao lake la kupata fedha za nje na kutumika kwenye viwanda vyake ambavyo  vinajengwa kwa ushirikiano na serikali ya China.

China imezichagua Tanzania, Kenya na Ethiopia kama nchi za mfano wa uwekezaji wake kwa Afrika ya Viwanda sio kwa makosa bali kuzingatia hali halisi ya matakwa ya viwanda.

Jumuia ya Afrika Mashariki inatarajia kuwa  na muingiliano mkubwa wa uchumi na viwanda na hivyo kutumia ziada ya umeme iliyopatikana kutoka Ethiopia kama ilivyoanishwa katika mradi wa Umoja wa Afrika (AU-NEPAD)ambao unataka mwunganiko wa umeme kikanda  na hivyo kufanya nchi zaidi ya kumi za eneo hili kuwa na umeme uliotangamana kwa hali na mali.

Mramba anasema kuwa kuweka miundombinu ya uzalishaji umeme na usafirishaji wake utawezesha kukua kwa uchumi na kufanya mengi ya maendeleo na kufanya Tanzania kama nchi ifikie malengo yake ya kuwa na viwanda  kufikika kirahisi nayo kuchangia vilivyo kwenye umoja huo kwa kuchakata umeme wake wa gesi asilia.

Nchi zinazoshiriki mpango huu ni Ethiopia, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na Sudan. Nchi nyingine ni Misri, Demokrati ya Congo (DRC), Eritrea na Tanzania. Nchi kama Eritrea, Ethiopia na Sudan zimeshanufaika na mpango huu kuntu ambao unaleta matumaini ya maendeleo ya haraka ikizingatiwa kuwa umeme unaotumika ni kutokana na maporomoko makubwa ya maji nchini Ethiopia na hivyo kwa bei ni rahisi, unarejeleka na wa kuaminika mradi kusiwe na mabadiliko makali ya hali ya nchi lakini kwa sasa unatosheleza  na katika miaka 25 ijayo.

Kenya imeshaanza kutandaza nyaya kuelekea huko na ndipo Tanzania itapata fursa ya kuunganisha halafu Rwanda na Burundi kwenye kile kinachotegemewa kuwa ni Eastern Africa Power Pool (EAPP) nayo itaunganishwa na Zambia kwenye South  Africa Power Pool (SAPP); kupitia Tunduma kwenda Dodoma hadi Arusha na Namanga hadi Kenya.

Hivyo ni kuleta maendeleo EAC na SADC na  kwayo kukamilisha kile inachoitwa East Africa Power Master Plan ambayo inapata fedha kutoka NEPAD Infrastructure  Project Preparatory Facility (NEPAD –IPPF)  kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika mfumo wa ushirikiano wa Umma na Wafanyabiashara Binafsi (PPP).

“Mwunganisho Mtandao wa umeme ni kuainisha kwa kuunganisha mitandao ya umeme ambapo eneo lilio na umeme mwingi  kiinchi na kikawaida litafidia kwa kupeleka kule ambako kuna upungufu kwenye nchi nyingine; na kinyume chake kwa kuzingatia mahitaji halisi na hivyo kuleta dhamana ya uhakika wa upatinaji umeme kwa bei nafuu na inayotabirika kwenye eneo husika,” alisema Mramba.

Taarifa zilizopo na kutumika kwenye suala hilo ni kuwa Ethiopia ina uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme ambapo kani ya Megawati 45,000 ipo na imeshafanyiwa kazi  ni megawati 6,000 na hizo zitafikia megawati 37,000  mwaka 2037 na hivyo nchi hiyo kuwa mwuzaji mkuu wa umeme nje ya nchi na bado kuna vyanzo vingine bwerere vya kuchakata umeme. Vyanzo hivyo ikiwamo ule wa nguvujoto ya ardhini, nguvu jua na ile ya upepo na mafuta.

Tanzania nako mambo sio haba kwani inavyanzo  6 vya umeme wa maji vikiwemo vya Mtera, Kidatu, Hale , Pangani Falls, Nyumba ya Mungu na Kihansi vyenye jumla ya uwezo wa Megawati 1, 700 kutokana na gesi asilia, maji, nguvu joto ardhi na petroli.

Gesi inayotumika ni kutoka Songosongo na Mtwara na huletwa Dar es Salaam kwa bomba kubwa la gesi liliotandazwa kilometa zaidi ya 542 liliogharimu zaidi ya dola bilioni 1.2.

Tanzania kutokana na hayo inampango mkakati wa kusafirisha umeme nje ya nchi na hivyo kufaidika ilivyo na gesi asilia iliyonayo ambayo mpaka sasa imefikia futi ujazo wa trilioni 57.2 nyingi ya hizo ziko kilometa 100 baharini.

Wachunguzi wa mambo ya uchumi wanahadhari kuwa Tanzania iwe macho sasa na mipango yake ya kuchakata umeme isije ikabambikwa miradi mingi na baadaye kukosa kuutumia vilivyo utajiri wake kutokana na kubanwa na mikataba hiyo au kugeuka kuwa soko tu la wengine kwani ni mikataba ya muda mrefu. Siku zote ujanja ni kuwahi sokoni.

Katika maendeleo mengine yanonesha kuwa Tanzania imeendelea kupunguza uagizaji wa umeme kutoka Kenya katika mji wa Namanga na kufikia kiasi cha asilimia 67 hadi mwezi Machi mwaka huu. Vilevile hata mali kutoka Kenya zimeendelea kupungua ambapo bidhaa  za kiasi cha dola milioni 52 ziliingizwa toka Kenya ukilinganisha na dola milioni 57 za mwaka jana na dola milioni 100 mwaka 2012 kwa mwezi wa Machi.

Taarifa rasmi zinaonesha umeme toka Kenya umepungua kwa kiasi cha asilimia 67.3 ambazo ni sawa na 170,000 kWh kwa miezi mitatu ya mwaka huu hadi Machi.

Kenya na Tanzania wanamaelewano ya kupeana umeme kwenye miji  ya pembezoni ambayo haijaunganishwa kwenye gridi ya taifa.  Joseph Oketch ni Mkurugenzi wa Energy Regulatory Authority (ERC) wa Kenya amethibitisha hali hiyo mipakani mwa nchi hizi mbili ikiwa ni kule Namanga na Lungalunga.

“Ni biashara ndogo mipakani kwani hakuna nyaya kubwa  zilizounganishwa kati ya nchi hizi mbili kuelekea huko na hivyo sio jambo kubwa,” alielezea Oketch.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles