27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania kinara ukuaji uchumi Sadc

ANDREW MSECHU

KATIBU Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), Dk. Stagomena Tax amesema Tanzania pekee ndiyo iliyofanikiwa kuvuka vigezo vya ukuaji uchumi kati ya nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi  wa jumuiya hiyo ulioanza jijini Dar es Salaam jana, Dk. Tax alisema Tanzania imefanikiwa kufikia ukuaji wa uchumi wa asilimia saba, wakati nchi nyingine zikibaki katika wastani wa ukuaji wa asilimia 3.1 mwaka 2018, ikilinganishwa na asilimia tatu mwaka 2017.

“Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Madagascar na Tanzania zimeonekana kuimarika katika ukuaji wa uchumi wake lakini ni Tanzania pekee iliyofanikiwa kufikia ukuaji wa asilimia saba ya GDP kwa mwaka 2018,” alisema.

Alisema hali ya ukuaji uchumi katika ukanda wa Sadc imeendelea kuwa ngumu kutokana na kutofikiwa kwa malengo yaliyowekwa kikanda.

Pamoja na hayo  mazingira ya kiuchumi yameonekana kuendelea kuimarika katika mwaka uliopita.

Dk. Tax alisema uhimilivu wa uchumi ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo kwa nchi wanachama na kuzihamasisha nchi nyingine kukua kiuchumi.

Alisema mataifa yote wanachama, isipokuwa moja, yalirekodi ukuaji mzuri kwa kila Pato la Taifa kwa mwaka wa 2018 na kulikuwepo maboresho kutoka nchi tano wanachama, ambazo ni Botswana, DRC, Mauritius, Shelisheli na Tanzania, ambazo zilirekodi ukuaji mzuri kwa mwaka 2017.

Alieleza kiwango cha mfumko wa bei kilipungua hadi wastani wa asilimia 8.0 mwaka 2018 kutoka asilimia 10.1 mwaka 2017, lakini kushuka kwa mfumuko huo kunahusishwa, miongoni mwa mengine, hali nzuri ya hewa katika baadhi ya nchi wanachama, shinikizo la chini la mahitaji, na utulivu katika viwango vya ubadilishaji.

Botswana, Eswatini, Lesotho, Madagaska, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini na Tanzania zilifikia viwango vya lengo la mfumuko wa bei wa asilimia 3-7.

Alisema pia kuna kushuka kwa uwekezaji na akiba, ulioorodheshwa tangu mwaka 2014, ambao uliendelea kwa mwaka 2018, ambapo kanda hiyo ilirekodi uwekezaji wa asilimia 22.8 ya Pato la Taifa mwaka 2018 ikilinganishwa na asilimia 24.4 mwaka  2017.

“Botswana, Lesotho, Shelisheli, Tanzania na Zambia zilifanya juu ya lengo la kikanda la asilimia 30 ya Pato la Taifa kwa uwekezaji.

Kwa upande wa akiba, ilibaki imegawiwa kwa asilimia 19.9 ya Pato la Taifa mwaka 2018, chini ya asilimia 20.6 iliyotambuliwa mwaka 2017.

“Ni Botswana tu, Msumbiji na Zambia zilizopata lengo la asilimia 30 mwaka 2018,” alisema.

Alisema upungufu katika akiba ya fedha uliongezwa kwa asilimia 3.1 mwama 2018 ikilinganishwa na asilimia 4.3 ya Pato la Taifa 2017.

Angola, DRC, Mauritius, Shelisheli na Tanzania zilifikia lengo la upungufu wa fedha wa asilimia tatu (3) ya Pato la Taifa mwaka 2018.

Alisema deni la Taifa liliendelea kukua katika nchi zote Wanachama mwaka 2018, ambapo deni la Taifa kikanda liliongezeka hadi asilimia 48.8 ya Pato la Taifa, kutoka asilimia 47.8 iliyorekodiwa mwaka 2017.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles