24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TANESCO YAZALIWA UPYA

Na Khamis Mkotya


tanescoSHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limefanya ukarabati mkubwa wa miundombinu yake katika jiji la Dar es Salaam.

Uwekezaji huo mkubwa unaogharimu mabilioni ya fedha, umelenga kumaliza tatizo la kukatika umeme mara kwa mara katika jiji hilo, ambalo limekuwa likisababishwa na ukongwe wa miundombinu.

Katika mpango huo, mifumo ya zamani ya analojia inabadilishwa katika vituo mbalimbali na kuwekwa mifumo mipya ya kisasa ya dijitali yenye ufanisi, ambayo itagharimu zaidi ya Sh trilioni 5 nchini kote.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesm Mramba alitoa taarifa hiyo Dar es Salaam juzi wakati wa majumuisho, baada ya ziara ya wahariri wa vyombo vya habari kutembelea miradi ya shirika hilo inayokarabatiwa.

Mramba alisema, mbali na kumaliza tatizo la ukatikaji wa umeme jijini humo, uwekezaji huo mkubwa pia unalenga kukidhi azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda.

“Hii itasaidia kuondoa dhana kuwa Tanesco haifanyi kazi, nchi inaweza kuwa na uchumi wa viwanda kama kuna uwekezaji katika umeme.

“Uwekezaji wa umeme haimanishi kwenye generation (uzalishaji) pekee yake. Uwekezaji ni katika mifumo yote, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji.

“Dhana ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda siyo dhana ya kufikirika ni dhana inayotekelezeka na ushahidi wa wazi ni uwekezaji huu mkubwa uliofanyika katika sekta ya umeme,” alisema.

Kwa mujibu wa Mramba, tatizo la ukatikaji wa umeme halihusiani na mfumo wa uzalishaji au usafirishaji, bali hujitokeza katika mfumo wa usambazaji na ndiyo maana shirika limeamua kufanya ukarabati huo.

Mramba ambaye aliongozana na wataalamu wa shirika hilo alisema, hadi kufikia Aprili mwakani tatizo la kukatika umeme mara kwa mara katika jiji la Dar es Salaam litakuwa historia.

Alisema katika teknolojia mpya umeme unaingia na kutolewa katika vituo vya usambazaji kwa njia zaidi ya moja, tofauti na mfumo wa sasa ambapo njia inayotumika ni moja na hivyo kusababisha tatizo la umeme kukatika pale njia hiyo inapopata hitilafu.

Miongoni mwa vituo vilivyotembelewa ni pamoja na kituo cha usambazaji cha Muhimbili, ambapo baada ya ukarabati kituo hicho sasa kitazalisha 15 MW wakati mahitaji ya hospitali ni 5MW na pia kitakuwa na mfumo wa njia tatu badala ya moja ya sasa.

Vituo vingine vilivyotembelewa ni New City Center, Sokoine Drive, Ilala na kituo cha udhibiti wa mifumo yote ya usambazaji kilichopo Msasani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles