Derick Milton, Simiyu
Uongozi wa Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Simiyu, umesema kuwa shirika hilo limeendelea kutekeleza maagizo ya Waziri Merdad Kalemani na Naibu Waziri Subira Mgalu la kuwaunganishia wananchi wa mkoa huo umeme kwa gharama ya Sh 27,000.
Shirika hilo limesema kwa kipindi cha nusu mwaka, limefanikiwa kuwaunganishia wateja 2000 kwa gharama hiyo kama agizo la viongozi wao walivyolitoa na wengine zaidi ya 1000 wakiunganishwa kupitia mradi wa REA.
Hatua ya Tanesco kutoa kauli hiyo imekuja zikiwa zimepita siku nne, tangu wananachi wa mkoa huo wamlalamikie Meneja wa Mkoa, Rehema Mashinji kuwa amekuwa akikataa kutekeleza maagizo ya viongozi hao.
Wananchi hao walimlalamikia Meneja huyo, kuwa amekuwa wakikataa kuwaunganishia umeme kwa gharama hizo kama ambavyo Waziri na Naibu Waziri wamekuwa wakiagiza.
Mbele ya waandishi wa habari leo Ofisa Mahusiano wa Shirika hilo Mkoa Beni Kilumba, amesema kuwa siyo kweli kuwa Meneja amekuwa akikataa kutekeleza maagizo hayo kwani zaidi ya nusu ya walengwa wamepatiwa umeme kwa gharama hiyo.
“Lengo letu lilikuwa kuwaunganishia wateja 4,523 ambapo mpaka sasa tumewaunganishia zaidi ya wateja 3,000 kwa gharama ya Sh 27,000, ambapo 1,000 kati ya hao wako wako kwenye mradi wa REA, ni 2,000 wale ambao wake nje ya mradi huo na wameunganishiwa kwa gharama ya 27,000,” amesema Beni.
Aidha amewataka wananchi wa mkoa huo waliombali na miundombinu ya umeme na wanahitaji kupata huduma kwa gharama hizo, kuendelea kuwa wavumilivu wakati shirika hilo likiendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wanapata umeme.