27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tanesco kuuza umeme Afrika Kusini

UKIJIOGRAFIA Tanzania imebarikiwa kwa mengi na hivyo ule wimbo maarufu wa “Tazama Ramani” ni haki kabisa na kujivunia nchi hii kwani ni kweli tupu asilimia 100.

Mwaka 1974  Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikumbushwa hali hiyo kule Japan ambapo alionyeshwa video na Mfalme Hirohito wa Japan video iliokuwa ikiandamana na wimbo wa Tazama Ramani huku ikioneshwa kwa uhalisia, maneno yote na kushahabiana  kwani samaki walikuwa wanarukaruka kwenye mito iliyokuwa inatiririsha maji kwenye maziwa huku watanzania wakifanya kazi.

Ilionekana kuwa ni nchi iliyojaaliwa kwa maji na ardhi yenye rutuba lakini kasoro yake ujumbe wa Tanzania ulienda  Japan kuomba chakula ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya kutangazia dunia kuwa ina neema kubwa  na ya ziada (bumper harvest).

Tanzania  ni kama daraja Afrika ukitokea kusini kwenda kaskazini (Cape to Cairo Route phenomenon ); na kutoka ndani ya bara Afrika kwenda Bahari ya Hindi Trans Africa Highway (West to East Africa)

Miundombinu

Miundo mbinu hufuatia mfumo wa kijiografia na hivyo kuifanya katika kushiriki Tanzania kuwa kwenye miradi mingi inayotandawaa nje ya nchi kama ilivyo kwenye miradi ya nishati mingi inayoendelea kujengwa.

Dalili zote zinaonesha kuwa itakapofika mwaka 2025Tanzania itakuwa na umeme wa kutosha na ziada ya kuuza nje na hivyo kukamilisha kiu yake ya maendeleo na kuhakikisha viwanda vinavyojengwa vina umeme tosha na wa uhakika na hivyo kutegemewa na wengi.

Kwa jumla, ndani ya muda mfupi, Tanzania itakuwa imejitosheleza kwa umeme wa uhakika na kuwa na ziada ya kuuza nje ya nchi baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa 22 na midogo.

Hali hiyo imekuwa bayana zaidi baada ya mradi wa umeme wa maji katika Mto Rufiji (Stiegler Gorge) kutiwa saini na kukabidhiwa kwa mkandarasi ukiwa ni ubia wa Kampuni ya Arab Contractors anashuguhulikia ujenzi  wa bwawa na (Osman A. Osman Co na Elsewedy Electric) zote Kampuni za Misri na kazi imeanza rasmi ya mradi wa ujenzi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji. Nchi inategemea kupata umeme wa MW 2100 ukiwa ni mradi mkubwa na wa nne kwa ukubwa Afrika.

Mradi huu utajenga bwawa kubwa lenye mita za ujazo bilioni 34 na kituo cha kufua umeme kitakachokuwa na mashine tisa za kuzalisha umeme zenye uwezo wa megawati 2,115, hivyo Tanzania kuwa na umeme mwingi.

Huu ni mradi uliobuniwa katika awamu ya kwanza mwaka 1974 ya uongozi chini ya Mwalimu Julius Nyerere, lakini ukashindwa kutekelezwa kwa muda mrefu na sasa chini ya Rais John Magufuli, serikali inatekeleza ndoto hiyo.

Miradi 22 ya umeme

Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), inatekeleza na kusimamia miradi mikubwa ya umeme ipatayo 22 katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiwamo yale ambayo kwa sasa hayana umeme wa uhakika na wa kutosha, pengine kwa sababu ya kutounganishwa na Gridi ya Taifa.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ile ya kuipatia umeme wa uhakika mikoa ya Magharibi mwa Tanzania ikiwamo Kigoma, Tabora, Katavi  na Bukoba  ambayo kwa muda mrefu imekuwa haina umeme wa uhakika kutoka katika Gridi ya Taifa.

Moja ya miradi hiyo ni mradi  mkakati  na mkubwa wa kuunganisha umeme katika Jumuiya ya Afrika Mashariki  (EAPP) East Africa Power Pool na nchi za Kusini mwa Afrika (SAPP) Southern Afrika Power Pool,  ambao ukikamilika, nchi itauza na kununua umeme mwingi kutoka Limpopo (Caborra Bassa) na Victoria Falls ya Zambia.

Mradi huo pia utakuwa na faida nyingine zikiwamo kuongeza usambazaji umeme kwa mikoa ya Kusini mwa Tanzania, kuimarisha uwezo wa taasisi za Tanzania katika biashara ya umeme na kupata sehemu ya kununua umeme au kubadilishana.

Mradi pia utachangia katika kuboresha usambazaji umeme kwa nchi za Afrika Mashariki na kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme, na utazisaidia Kenya na Tanzania kuondokana na umeme wa gharama kubwa unaofuliwa kwa gesi na kutumia wa gharama nafuu wa maji, hivyo kupunguza uchafuzi wa kemikali zinazotokana na ukaa na gesi.

Mradi huo unafahamika kwa jina la Kenya – Tanzania Power Interconnector Project (KTPIP)/ZTK au Mradi wa Laini ya Msongo wa Kilovolti 400 wa Isinya – Namanga – Singida, utakaokamilika mwakani.

Utekelezaji wa mradi huu umeanza mwishoni mwa mwaka jana, na kwa mujibu wa Mratibu wa Mradi Mhandisi Peter Kigadye, gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 258.82 (takribani Sh bilioni 600).

Kigadye anasema mradi unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Serikali ya Tanzania.

“Kampuni ya Usambazaji ya Umeme ya Kenya (KETRACO) na Tanesco kwa sasa wanatekeleza mradi huu wa kuunganisha umeme kati ya Kenya na Tanzania, na sehemu yote ya Kusini mwa Afrika,” anasema Kigadye katika mazungumzo na wahariri wa vyombo vya habari  eneo la Nanja,  Monduli mkoani Arusha.

Kigadye anasema mradi huo ni sehemu ya mpango wa maendeleo ya sekta ya nishati ambao Serikali ya Tanzania inakusudia kuunganisha Gridi ya Taifa na nchi za Kenya na Zambia na mwishowe Ethiopia utakapokamilika mradi wa Millenium.

Anasema mpango huo utaiwezesha Tanzania kuingiza umeme wa bei rahisi kutoka Ethiopia kupitia Kenya hadi Zambia kwa mpango unaojulikana kama Southern African Power Pool (SAPP).

Kwa mujibu wa Kigadye, mradi huo wa KTPIP utakuwa na urefu wa kilometa 510.7, na kati ya hizo, Tanzania itakuwa na kilometa 414.7 na Kenya kilometa 96.

Anasema na kuanisha gharama zitakazobebwa na kila nchi na utaanzia mkoani Singida kutoka katika mradi mwingine mkubwa  wa TANESCO maarufu kama Backbone, utakaounganishwa kupitia Babati-Arusha-Namanga hadi Isinya, Kenya.

Anasema tayari kipande cha Singida hadi Babati (kilometa 150), mkandarasi ni Kampuni ya Kalpataru Power Transmission ya India kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 34.84 na Sh bilioni 17.982.

Kwa kipande cha Babati hadi Arusha cha kilometa 150, mkandarasi ni Bouygues Energies & Services (BYES) ya Ufaransa kwa gharama ya Dola milioni 36.89 na Sh bilioni 22.354. Eneo la Nanja ndiko ambako kampuni hiyo ya Ufaransa imeweka vifaa vyake na inaendelea na utekelezaji wa mradi kwa kasi kubwa.

Kipande cha tatu ni Arusha hadi Namanga mpakani na Kenya chenye urefu wa kilometa 114.7, kinachojengwa na kampuni za Energoinvest & EMC (CEE) kutoka Bosnia-Herzegovina na India, kwa gharama ya Dola milioni 30.65 na Sh bilioni 18.97.

Mratibu wa Mradi huo anasema kutakuwa pia na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha kilovolti 400 Lemugur jijini Arusha na ukarabati wa kituo kingine cha Singida cha kilovolti 220/33.

Anasema Tanzania imelipa fidia ya Dola za Marekani milioni 40 (zaidi ya Sh Bilioni 80) kwa wananchi walioathiriwa na mradi huo ambao sasa utaifungua mikoa ya Magharibi utakapopita katika mikoa yao kuelekea nchi za Kusini mwa Afrika.

Mikoa  ya Magharibi  watafaidika kutokana na utekelezaji wa miradi ya Geita-Nyakanazi kilovolti 220 kilometa 144, njia kuu ya umeme kilovolti 220 Rusumo – Nyakanazi kilometa 98, njia kuu ya umeme ya kilovolti 400 Iringa – Mbeya – Tunduma – Sumbawanga kilometa 624, njia kuu ya umeme ya kilovolti 400 Nyakanazi-Kigoma kilometa 280 na Kigoma – Sumbawanga kilovolti 400 kilometa 280. Mradi wa Rusumo

Meneja Mwandamizi wa Miradi wa Tanesco, Emmanuel Manirabona anasema vifaa  vingi kwa ajili ya mradi huo vimeshawasili na makandarasi wanaendelea na kazi yao vizuri.

Mkandarasi Bouygues Energies & Services na wafanyakazi wake walionekana wakiendelea na kazi ya kumwaga zege ili kusimika minara ya umeme ambao kwa kipande cha Babati-Arusha itakuwa 383.

Meneja Mkazi wa Mradi wa kampuni hiyo ya Kifaransa, Christophe Bartholome anasema wanatarajia kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kwani wako kamili kivifaa, na pia wasingependa kutozwa faini kwa kuchelewesha kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka anasema miradi hiyo ni ya kusogeza miundombinu katika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme, lakini pia kukarabati miundombinu chakavu au kuzidiwa katika maeneo yaliyokwishafikiwa na umeme.

Anasema: “Hakuna kipindi ambacho kuna miradi mingi ya umeme kama hiki cha awamu ya tano. Katika historia ya Tanesco hatujawahi kuwa na miradi mikubwa 22 kwa wakati mmoja kama sasa ikiwamo Stiegler’s Gorge.”

Kati ya miradi hiyo, ipo itakayokamilika mwaka huu, wakati itakayochukua muda mrefu itakamilika mwaka 2023 NA HIVYO kuwa kama ilivyopangwa kuishia yote kabla ya 2025 na hivyo kufungua ukurasa mpya wa utekelezaji.

Miradi inayotarajiwa kukamilika mwakani ni upanuzi wa umeme wa gesi wa Kinyerezi I wa megawati 185 uliofikia asilimia 82, na TEDAP (Mradi wa Kukarabati na Kuimarisha Mifumo ya Umeme) ambao ni ujenzi wa kilometa 51.7 za njia kuu ya umeme wa kilovolti 132 Ubungo-Kurasini-Mbagala-Gongo la Mboto-Kipawa.

Kadhalika, ujenzi wa vituo vya kupoza umeme wa kilovolti 132/33 vya KIA, Kiyungi, Kurasini, Mbagala na Gongo la Mboto na ujenzi wa vituo 19 vya usambazaji kilovolti 33/11 (Dar es Salaam vituo 11, Arusha sita na Kilimanjaro vituo viwili.

Kwa mujibu wa Dk Mwinuka, utekelezaji wa mradi huu wa TEDAP umekamilika kwa asilimia 98 na vituo vyote vinatumika sasa, ukiacha kituo cha Kurasini na kuvusha nyaya eneo la Mzinga Creek.

Miradi inayotarajiwa kukamilika mwakani ni pamoja na Nishati Jadidifu, Jua megawati 150 na upepo megawati 200 na umeme wa makaa ya mawe megawati 600 (uchambuzi wa zabuni kushindanisha wawekezaji binafsi unaendelea).

Mwingine ni mradi wa njia kuu ya umeme wa kilovolti 400 Singida-Namanga kilometa 510 maarufu KTPIP ambao makandarasi wote watatu wameanza kazi. Makandarasi hao ni Kalpataru Power Transmission Limited ya India, Bouygues Energies & Services ya Ufaransa na Energoinvest & EMC (CEE) za Bosnia Herzegovina na India.

Miradi mingine ni wa njia kuu ya kilovolti 220 Bulyanhulu – Geita kilometa 55 (mkandarasi ameshaanza utekelezaji wa mradi), njia kuu ya umeme ya kilovolti 220 Geita – Nyakanazi kilometa 144 (mkataba wa utekelezaji unasubiri kusainiwa mwezi ujao) na njia kuu ya umeme kilovolti 220 Rusumo-Nyakanazi kilometa 98 (mkataba wa utekelezaji umepata kibali cha kusainiwa Januari 2019).

Miradi inayotarajiwa kukamilika mwaka 2021 ni njia kuu ya umeme kilovolti 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma kilometa 504 (upembuzi yakinifu Chalinze – Dodoma ulishakamilika na Rufiji – Chalinze umeanza), njia kuu ya umeme kilovolti 400 Kinyerezi – Chalinze kilometa 115 (upembuzi yakinifu umeanza).

Katika miradi hiyo 22, ipo itakayokamilika mwaka 2022 ambayo ni pamoja na ule wa maji ya Maporomoko ya Mto Rufiji maarufu Stiegler’s Gorge wa megawati 2,100 ambao mkandarasi ameanza hatua za awali za utekelezaji, na mradi wa njia kuu ya umeme ya kilovolti 400 Iringa – Mbeya – Tunduma – Sumbawanga kilometa 624 (fedha za utekelezaji zimeshapatikana Dola za Marekani milioni 455).

Kwenye umeme wa gesi Mtwara megawati 300 (upembuzi yakinifu utakamilika 2019), njia kuu ya umeme ya kilovolti 400 Nyakanazi – Kigoma kilometa 280 (fedha za kutekeleza mradi zimeshapatikana, Dola za Marekani milioni 187) na njia kuu ya umeme ya kilovolti 400 Mtwara – Somanga kilometa 250 (upembuzi yakinifu kukamilika 2019).

Aidha, miradi itakayokamilika mwaka 2023 ni umeme wa maji Kakono megawati 87 (upembuzi yakinifu kukamilika 2019), umeme wa maji Ruhudji MW 358, umeme wa maji wa Rumakali MW 222 (Yote mapitio ya upembuzi yakinifu kukamilika 2019).

Dk Mwinuka pia alieleza kuwa Tanesco ipo katika hatua za awali za kutekeleza miradi mingine mingi ya kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kama vile kuongeza transfoma ya megawati 300 katika kituo cha kupoza umeme cha Ubungo (kazi inatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi huu) na ukarabati wa vituo 10 vya kupoza umeme vya Mbeya, Mufindi, Mlandizi, Chalinze, Same, Tabora, Mwanza, Musoma, Bukoba na Dodoma.

Hii inadhihirisha wazi kuwa TANESCO  ni shirika kubwa na sio la mchezo kwani sio rahisi kuwa na miradi yote hii na kuweza kuikamilisha kwa usalama. Kinachofurahisha zaidi ni kuwa miradi hiyo inasimamiwa kwa ufanisi na wahandisi ambao ni watanzania. Ni kweli tunaweza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles